Mtoto
apotelea Marekani akiwa mikononi mwa Balozi
Binti Anneth Joseph
Mangawo (25), wa ukoo wa Owenya anayedaiwa kuchukuliwa na Balozi wa sasa wa
Tanzania nchini Zambia, Grace Mujuma, amepotea katika mazingira tatanishi
wakati balozi huyo akifanya kazi ubalozi wa Tanzania jijini New York, Marekani.
Balozi huyo anadaiwa
kumchukua binti huyo kama msichana wa ndani na kwenda naye nchini Marekani
mwaka 2004, ambapo kabla alichukuliwa kutoka kata ya Old Moshi Magharibi,
ambako alikaa Dar es Salaam, na baadaye nchini Marekani.
Baba mdogo wa binti huyo,
Robinson Owenya, akizungumza na NIPASHE Jumapili, anasema kwa kipindi chote
waliwahi kuwasiliana na binti huyo mara moja, hadi Balozi huyo alipomaliza muda
wake wa kukaa nchini humo wa miaka minne na kurejea Tanzania mwaka 2008, bila
binti huyo.
Taarifa zinadai kuwa,
mwanzoni mwa mwaka 2012, Balozi Grace akiwa ameshateuliwa na Rais kuwa Balozi
wa Zambia, alikuja kwenye msiba wa baba yake mzazi eneo la Old Moshi, mkoani
Kilimanjaro.
“Tulimfuata kumuuliza juu
ya mtoto wetu, majibu aliyotupa ni kuwa alikuwa ananyanyasa watoto wake na mama
wa Anneth akamuuliza kwa nini hakumpakia kwenye ndege arudi, alidai kuwa
alimpeleka shule akajifunze Kiigereza na ndipo akaiba pasi ya kusafiria na
vitambulisho na akaondoka,” alisema Owenya.
Alisema walikwenda kwa
baba yake mdogo, anayemtaja kwa jina la Fredy Maro, ambapo waliondoka pamoja na
kwenda kwa kaka yake, Dk. Prosper Maro, ambaye alimtetea dada yake na kueleza
kwamba wakifuatilia kisheria, binti yao atakamatwa nchini humo na kupelekwa
gerezani na hatarudi hadi baada ya kifungo.
“Nilimweleza ninachotaka
ni binti yetu apatikane akiwa hai, kama ambavyo alichukuliwa, hatuna mkataba na
Mungu,” alisema.
Aliongeza, “alinipa namba
za simu za Balozi Grace, ili mama wa Anneth aweze kupata fedha kidogo,
nilikataa na kumueleza shida si fedha bali mtoto wetu, akasema hana la
kunisaidia.”
Alisema haiingii akilini
kuwa mhusika (Grace Fanuel Maro ambaye kwa sasa anaitwa Grace Mujuma), anajenga
hoja ya kumhusisha binti huyo na unyanyasaji wa watoto kwenye nchi ya kigeni.
Alisema alitoa taarifa
polisi mkoani Kilimanjaro, na kufungua kesi namba KR/CID/PE/03/2012 Januari 16,
mwaka huu, ambapo walimtuma kwenda kuichunguza nyumba ambayo inaelezwa Balozi
Grace alikuwepo, eneo la Shanty Town, na kuwapa taarifa polisi.
Alisema polisi
waliambatana naye hadi eneo hilo, lakini hawakufanikiwa kumkuta kwani muda
mfupi alikuwa ameshaondoka kurudi Dar es Salaam.
Alisema waliacha maagizo
kwa mama yake (Grace) afike kituo cha polisi na kuandika maelezo ambapo
alifanya hivyo na kuweka namba za simu za mwanaye.
“Nilikaa kwa muda, askari
mmoja akatumwa Dar es Salaam kufuatilia, ambapo alikuta Grace ameshaapishwa
kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia na wakati anamchukua binti yetu alikuwa
Afisa wa Ubalozi,” alisema.
Hivyo, alisema askari
polisi hawana uwezo wa kumkamata kwa kuwa anakinga ya kibalozi na kibali cha
kumkamata kinatoka kwa Rais,” alisema.
Alisema alikwenda kwenye
kituo cha msaada wa sheria na haki za binadamu jijini Dar es Salaam, ambao
waliahidi kumsaidia ikiwa ni pamoja na kutoa kwenye vyombo vya habari lakini
hatua hiyo haijafanyika.
“Nimeamua kuyasema haya
nikijua kwamba hakuna mwenye mkataba na Mungu, nimefanya hivi ili ifahamike,”
alisema.
“Ninamuomba Rais Jakaya
Kikwete kuingilia kati suala hili, kwani aliyechukua binti yetu ni Balozi wake
na kumekuwa na ubabaishaji mkubwa, familia yetu ni Maskini…”
“Mama yake hajiwezi lakini
tunachangishana kupata fedha za kufuatilia suala hili, hatujui tulie msiba au
tufanye nini, kama alikufa tungeona hata mwili wake au kujulishwa,” alisema.
Mama mzazi wa Anneth,
Judica Owenya, alisema dada yake, Edora Maro, (ambaye ameolewa na baba mkubwa
wa Grace), alikwenda nyumbani kwake na kumuomba binti huyo kwa ajili ya kwenda
kufanya kazi.
Akizungumza huku akilia,
alisema mwanaye huyo ni uzao wake wa saba, na kwamba anajisikia vibaya kwani
hajui kama yupo hai au la, Hivyo kuiomba serikali kumsaidia kumtafuta mwanaye
ambaye hata kwenye msiba wa baba yake mzazi hakufika.
Aidha, kwa mujibu wa barua
ya Machi 16, mwaka huu, kutoka kwa kampuni ya uwakili ya Rex Attorneys, yenye
kumbukumbu namba REX/GMM/171/12 ambao ni mawakili wa Balozi Grace, akijibu
barua ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Barua ya LHRC yenye
kumbukumbu LHRC/LAC.VOL.XVII/9 ya Februari 27, mwaka huu, ambapo Grace
alithibitisha kumchukua binti huyo na kwenda naye Marekani kwa ajili ya kufanya
kazi za ndani nyumbani kwake.
Alisema baada ya kufika
alifanya kazi kwa mwaka mmoja, ambapo mnamo Desemba 2, 2005, alitoroka baada ya
kuchukua hati yake ya kusafiria na vitambulisho vyake vingine, ambapo alitoa
taarifakwa polisi wa nchini Marekani (New York Police Department), ambao
walisema kwa mujibu wa sheria za Marekani kwa kuwa binti huyo ana umri wa mtu
mzima hawana la kufanya bali wanahisi kuwa amepata mpenzi na kwenda kukaa naye.
Alisema pia alitoa taarifa
za tukio hilo kwa mjomba wake, ambaye kwa sasa ni marehemu, ambapo baada ya
miezi nane kupita tangu kupotea kwake alitoa taarifa kwa vyombo husika kufuta
visa yake, ambapo Januari, mwaka 2012 kwa barua ya kumbukumbu namba
CID/HQ/PE/16/ 2012 alitoa taarifa kwa Kitengo cha Polisi wa Kimataifa
(Interpol) na mnamo Januari 13, mwaka huu, aliieleza familia ya Anneth.
Hata hivyo, Owenya alisema
mnamo Julai 14, mwaka huu, aliitwa jijini Dar es Salaam na kukutanishwa na
Grace akiwa na mawakili wake wawili, ambapo baada ya mazungumzo ambayo mengine
yalikuwa na utata kutokana na muda mwingi walitumia lugha ya kiingireza
asiyoifahamu.
Alisema walimshinikiza
kuandika barua Interpol kuomba wamsaidie kumtafuta binti yake, lakini alikataa
na kueleza kuwa anayemdai ni Grace kwa kuwa ndiye aliyemchukua kijijini na hata
walipomuuliza aliwajibu jeuri mara baada ya kukutana kwenye msiba wa baba yake
na endapo wasingeuliza asingewajulisha.
Alisema Agosti 15, mwaka
huu, alitumiwa kwa njia ya mtandao makubaliano yenye maelezo ya malalamiko yake
na sahihi ya Grace na wakili wake, ikiwa na makubaliano yaliyosomeka na
kutakiwa kuyasoma na kuridhika nayo na kisha kuweka sahihi.
“Grace Mujuma ambaye
alikwishatoa taarifa Interpol aendelee kufuatilia kupata taarifa
zitakazowezesha kupatikana kwa Anneth na ashirikiane na kitengo hicho kumtafuta
na kumrudisha kwa wazazi wake mapema iwezekanavyo mara baada ya kupatikana
kwake,”alisema.
Alisema anaiomba serikali
kulifanyia kazi suala hilo kwani linatia utata na hakuna hatua zinazochukuliwa
ili hali muhusika ni mtu mwenye kinga ya kushtakiwa na wenye mtoto ni watu
wanyonge wasio na uwezo wa kifedha.
Jitihada za kuwasiliana na
Grace kupitia simu za ofisi ya ubalozi wa Tanzania nchini Zambia,
hazikufanikiwa kutokana na kuita mara kadhaa pasipo kupokewa.
Chanzo: Gazeti la
Nipashe
No comments:
Post a Comment