Thursday, September 27, 2012

Tamko la Ismail Jussa kuhusu Muungano wa Jamhuri ya Tanzania.


Ismail Jussa.

TUNATAKA JAMHURI YA WATU WA ZANZIBAR YENYE MAMLAKA KAMILI KITAIFA NA KIMATAIFA ITAKAYOFUATIWA NA MUUNGANO WA MKATABA KATI YAKE NA JAMHURI YA TANGANYIKA

Muungano wa Mkataba maana yake nini?
Muungano wa Mkataba ni MASHIRIKIANO kati ya nchi mbili au zaidi ambazo kila moja huwa inabaki na mamlaka yake kamili ya KIDOLA kitaifa na kimataifa lakini vado zikawa zina mashirikiano katika maeneo maalum zitakazoamua kushirikiana, mahusiano ambayo huwa yanaongozwa na Mkataba.
Muungano wa Mkataba ni tofauti kabisa na Muungano wa Kikatiba ambao huwa unamaanisha kuwepo kwa Serikali ya Muungano inayosimamia mambo ya Muungano. Katika Muungano wa Mkataba, kila nchi hubaki na Serikali yake kamili yenye kusimamia mambo yote. Yale maeneo ya USHIRIKIANO husimamiwa kupitia ama KAMISHENI YA PAMOJA au KAMATI YA PAMOJA kwa kadiri makubaliano yatakavyokuwa yamewekwa kwenye Mkataba.
...
Ni zipi faida za Muungano wa Mkataba:
1.
Hakuna khofu ya nchi moja kuimeza au kuitawalia nchi nyengine.
2. Kila nchi inabaki na uhuru na mamlaka yake kamili kitaifa na kimataifa kuamua mambo yake.
3. Kila nchi mwanachama ina uhuru wa kujitoa katika jambo lolote ililoamua mwanzo kushirikiana pale inapoona hakuna maslahi au faida kuendelea nalo.
4. Huvutia nchi nyingi kuingia katika Muungano wa aina hiyo kwa sababu hakuna khofu ya kupoteza mamlaka au kupunguziwa madaraka au mambo yake kuamuliwa na nchi nyengine.
5. Mahusiano huwa ni ya kirafiki na ya ujirani mwema yanayopelekea kuaminiana na kuondoa kutiliana shaka kusikokwisha.

Zanzibar iwe na mamlaka yepi kitaifa na kimataifa katika Muungano wa Mkataba?
1. Iwe na Serikali kamili yenye Wizara zote ikiwemo Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani na Ulinzi.
2. Iwe na kiti chake Umoja wa Mataifa na pia uanachama wa Jumuiya zote za Kimataifa zikiwemo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika, Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Nchi za Bahari ya Hindi.
3. Iwe na Benki Kuu yake na Sarafu yake.
4. Iwe na mamlaka yote ya kuamua será za fedha na uchumi, kodi na sarafu.
5. Iwe na Uraia wake.
6. Iwe na Paspoti yake na kusimamia Uhamiaji katika nchi yake.
7. Idhibiti Anga yake na Usafiri wa Anga yenyewe.
8. Isimamie Elimu ya Juu yenyewe na kuamua Mitihani gani itumie katika masomo.
9. Isimamie na inufaike na rasilimali zake zote za ardhini na baharini ikiwemo mafuta na gesi asilia.
10. Idhibiti yenyewe eneo la mipaka ya Bahari Kuu (EEZ) katika eneo lote inalopakana nalo.
11. Idhibiti mamlaka mengine yote yanayokuwa yanamilikiwa n anchi kamili.

Ni ipi Mifano ya Muungano wa Mkataba?
- Muungano wa Umoja wa Ulaya wenye nchi wanachama 27.
- Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye wanachama 5 mpaka sasa.
- Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika Magharibi (ECOWAS).

PAMOJA TUNAWEZA

No comments: