Waandishi wa
habari wa Tanzania waandamana kulaani mauaji ya Mwandosi
Askari wa kikosi cha kuzuia fujo (FFU) kikiwa tayari kwa mtafaruku na waandishi wa habari.
Waandishi wa habari nchini Tanzania
wameanzisha maandamano kulaani mauwaji ya mwandishi mwenzao, Daudi Mwangosi,
ambaye aliuwawa hivi karibuni wakati akiwa kazini wilayani Mufindi mkoani
Iringa.
Wakiwa na nyuso za huzuni huku wakivalia
nguo nyeusi na kubeba mabango kadhaa, waandishi wa habari wamejitokeza mitaani
kupinga na kulaani vikali tukio la mauwaji ya mwandishu huyo wa habari, ambalo
ni la kwanza la aina yake kutokea nchini Tanzania.
Mikoa kadhaa imeripotiwa kufanikisha maandamano hayo, ikiwemo
mkoani Iringa ambako Daudi aliuwawa na ndiko pia alikokuwa akiendesha shughuli
zake za uandishi wa habari.
Pamoja na mvua za rasha rasha zilizonyesha nyakati za asubuhi
jijini Dar es Salaam, hali hiyo haikuwazuia waandishi habari kujitokeza kwa
wingi wakianzisha maandamano kutoka zilipo ofisi za kituo cha televisheni
Channel Ten ambako Daudi akifanyia kazi mpaka viwanja vya Jangwani vilivyoko
pembezoni kidogo ya katikati ya jiji.
Kwenye kilele cha maandamano hayo kumetolewa matamko ya kulaani
mauwaji hayo, huku mengine yakikosoa mwenendo wa vyombo vya dola. Miongoni mwa
waliotoa matamko hayo ni mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Jackton
Manyerere, na mhariri wa siku nyingi nchini humo, Jesse Kwayu.
Katika hali ya kushangaza,waziri wa mambo ya ndani Emmanuel
Nchimbi alijipenyeza kwenye kusanyiko hilo na baadaye kutoa maelezo kadhaa,
lakini alishindwa kuendelea kutokana na mayowe yaliyomtaka aondoke kwenye eneo
hilo.
Kundi moja la waandishi wa habari limesema linatazamia kuchukua
hatua za kisheria kuwabana askari wote waliohusika kwenye mauwaji hao.
Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Khelef
Chanzo: Idhaa ya Kiswahili, Deutsche Welle
No comments:
Post a Comment