Rais Jakaya Kikwete akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon alipomtembelea ofisini kwake makao makuu ya umoja huo nchini Marekani, juzi.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana, imeeleza kuwa viongozi hao walikutana jijini New York, Marekani ambapo Katibu Mkuu amesifia jitihada za Tanzania katika kupatia suluhu suala hilo.
“Majuzi nilikutana na Rais Joyce Banda wa Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zenu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi wa amani. Hii ndiyo njia sahihi na UN inaunga mkono njia hiyo,” alisema Ban Ki Moon.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alimweleza Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania bado inaamini kuwa njia sahihi na ya maelewano zaidi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia ya mazungumzo.
“Wazo la awali la kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika ambaye aliniandikia barua ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo kuhusu mzozo huo. Nasi tulikubali. Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza,” alisema Rais Kikwete
Aliendelea:“Mpaka kati ya Malawi na Msumbiji kwenye ziwa hilohilo, umekuwa katikati ya ziwa tangu mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuuweka mpaka huo nje ya ziwa. Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto mkubwa zaidi unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto wenyewe.”
Rais Kikwete alibainisha kuwa kila mahali ambako nchi zinatenganishwa na maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi. “Sisi tunadhani hata kwenye mpaka wetu na Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe katikati ya ziwa,” alisema Rais Kikwete na kuendelea:
“Katika hali ya sasa wananchi wetu wanapokunywa maji ya Ziwa Nyasa wanakunywa maji ya Malawi, kila watu wetu wanaposafiri ndani ya ziwa kufanya shughuli zao wanasafiri kwenye maji ya Malawi. Hili ni jambo linalohitaji majadiliano ya kuliweka vizuri.”
Msimamo wa Malawi
Mazungumzo ya viongozi hao yamekuja huku Rais wa Malawi, Joyce Banda akiwa ametangaza kujitoa kwenye mazungumzo hayo kwa madai kuwa Tanzania imechukua hatua korofi kwa kuchapisha ramani inayoonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo uko katikati.
Rais Banda alitangaza uamuzi huo wakati alipokuwa akilihutubia taifa hilo baada ya kurejea nchini kwake akitokea Umoja wa Mataifa (UN) alikokuwa kwa ziara ya kikazi.
"Wakati naondoka kwenda UN nilidhani suala la mpaka wa Malawi na Tanzania lilikuwa likihitaji mazungumzo, lakini nikiwa huko nikasikia kwamba Tanzania imezindua ramani mpya inayogusa ziwa hilo," alisema Banda na kuendelea;
"Baada ya hatua hiyo wavuvi wa Malawi wameanza kufukuzwa ufukweni na boti zetu zinaondolewa Tanzania. Ni suala zito sasa ambalo tunatakiwa kuchukua hatua nyingine," alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, John Haule alipoulizwa jana kuhusu msimamo wa Tanzania kwa kauli hiyo ya Malawi alisema: "Jana sikumpata Waziri (Membe) kupata ushauri wake, ila ninaendelea kuwasiliana na Balozi wetu Tanzania wa Malawi aifuatilie kauli hiyo kujua kama ni kweli imetolewa na Rais."
Katibu Mku huyo alisema ikithibitika kuwa ni kauli ya Rais Banda, atawasilina na Waziri Membe ambaye kwa sasa yuko nje ya nchi ili baadaye ajadiliane na Rais Kikwete wakiwa huko Canada.
Katika hotuba yake ya mwishoni mwa mwezi Septemba, Rais Jakaya Kikwete alielezea hatua zilizochukuliwa na Serikali yake kushughulikia mzozo huo kuwa tume ya pamoja ilipanga kukutana Septemba 10 hadi 15 mwaka huu, lakini mkutano huo haukufanyika kwa maombi ya Serikali ya Malawi
Chanzo: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment