Vincent Josephat Nyerere (Mbunge); Waziri kivuli mambo ya ndani (CHADEMA)
Ndugu wanahabari, kwanza kabisa
napenda kuwashukuru kwa kuitikia wito wangu, ili niweze kuzungumza na
watanzania kupitia kwenu kuhusu hatari kubwa inayolikumba taifa ya madawa ya
kulevya.
Biashara haramu ya dawa za
kulevya imekua kwa kasi sana hapa nchini miaka ya hivi karibuni licha ya kuwa
na vyombo lukuki vya ulinzi na usalama na licha ya kuwa na Tume maalumu ya
kudhibiti madawa ya kulevya chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri
Mkuu Mhe. Mizengo Pinda, iliyosomwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu –
Sera Uratibu na Bunge Mhe. Wiliam Lukuvi tarehe 26 Juni, 2013 siku ya
maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita dawa za kulevya huko Dodoma ni kwamba
katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012 watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa
kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya hapa nchini. Aidha,
watanzania wapatao 240 walikamatwa na madawa ya kulevya katika nchi za Brazil,
Pakistan na Afrika ya kusini na hivyo kutia doa taswira ya Tanzania katika
jumuiya ya kimataifa. Kutokana na kukithiri kwa biashara hii haramu, Serikali
kupitia maadhimisho hayo ya siku ya kupiga vita madawa ya kulevya duniani
ilitangaza kuwa biashara ya dawa za kulevya kuwa ni janga la taifa.
Mtakumbuka pia kwamba hivi
majuzi, muda mfupi baada ya Serikali kutangaza kuwa biashara ya dawa za
kulevya ni janga la taifa , walikamatwa wasichana wawili ambao ni watanzania
huko Afrika ya kusini wakiwa na kilo 150 za madawa ya kulevya yenye thamani ya
zaidi ya randi milioni 42.6 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 6 za
kitanzania.
Ndugu wanahabari, matukio yote
haya yametokea ndani ya kipindi cha miaka sita tu ya utawala wa Serikali ya
awamu ya nne ambapo kuna viongozi wa juu Serikalini ambao waliwahi kusema kuwa
wanawajua watu wanaojishughulisha na biashara haramu ya dawa za kulevya lakini
mpaka sasa hawajawataja wahusika na wala hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa
dhidi ya wahusika.
Ndugu wana habari, miongoni mwa
viongozi wa serikali na taasisi nyingine waliosema kuwa
wanawafahamu wafanya biashara ya madawa ya kulevya ni:-
Rais Jakaya Kikwete, ambaye
alipiga hatua kubwa zaidi na kusema anawajua hata viongozi wa dini wanaofanya
biashara hiyo. Licha ya maaskofu na viongozi wengine wa dini kumtaka Rais awataje
wahusika hao wa madawa ya kulevya ili kuuweka ukweli wazi, Rais hajafanya
hivyo mpaka sasa.
Kamishna wa Tume ya Kudhibiti
Dawa za Kulevya: huyu alisema anayo majina
ya vigogo (kwa maana ya viongozi) wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya
lakini hajaweka majina hayo hadharani na wala haijulikani kama wahusika hao
wamechukuliwa hatua yoyote hadi sasa.
Mbunge wa Mwibara –
Kange Lugola alisema katika bunge la bajeti 2013/2014 kuwa kama Rais na
Kamishna wa tume ya kudhibiti dawa za kulevya wanawajua “kwa majina” watu
wanaojihusisha na biashara za dawa za kulevya na hawataki kuwataja watu hao
wala kuwachulia hatu yamkini watu hao ni miongoni mwa mawaziri ndio maana kuna
kigugumizi cha kuwataja na kuwachukulia hatua. Tangu Mhe. Kange Lugola alihusishe
baraza la Mawaziri na kashfa hiyo ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya
hakuna hatua yoyote ilivyochuliwa na Serikali kuthibitisha au kubatilisha kauli
hiyo.
Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP
Bw. Reginald Mengi aliwahi kutoa taarifa ya wazi kuwa kuna kundi la
matajiri wanaoshirikiana na viongozi wa Jeshi la Polisi waliokuwa wanapanga
njama za kumwekea mtoto wake dawa za kulevya ili wambambikizie kesi ya dawa za
kulevya na hivyo kuchafua heshima ya Bw. Mengi na familia yake. Ndugu mengi
alisisitiza katika taarifa yake kwamba yuko tayari kutoa ushirikiano kwa jeshi
la polisi na mamlaka nyingine zinazohusika ili kubaini njama hizo na kuchukua
hatua stahiki kwa wahusika lakini mpaka leo Ndugu Mengi hakuhojiwa ili
kuthibitisha kauli yake jambo linaloashiria kwamba kuna ukweli katika kauli
yake.
Baada ya matukio yote haya na
baada ya Serikali kukaa kimya kuhusu matukio hayo, mimi kama Waziri Kivuli wa
Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ninatoa tamko kama ifuatavyo:
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
awataje na kuwachukulia hatua watu aliosema anawafahamu wanaojishughulisha na
biashara ya dawa za kulevya la sivyo akubali kubeba shutuma kwamba Serikali
yake ndio Mratibu Mkuu wa biashara ya dawa za kulevya ndio maana anashindwa
kuchukua hatua.
Kamishana wa Tume ya Kudhibiti
Dawa za Kulevya awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma juu ya hatua
alizochukua dhidi ya wahusika wa biashara ya dawa za kulevya aloiosema
anawafahamu la sivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuwashawishi
wananchi kuamini kwamba yamkini na yeye yumo katika mtandao wa wafanya
biashara haramu ya dawa za kulevya ndio maana anasita kuwachukulia hatua
wahusika hao ambao alishakiri kuwa anawafahamu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege awajibike kwa kutoa maelezo kwa umma kuwa ni tatizo gani
linaloikabili mamlaka yake hadi kufanya viwanja vya ndege vya Tanzania kuwa
ndio njia rahisi ya kuingiza na kusafirishia madawa ya kulevya katika
ukanda wa Afrika Mashariki?
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na
Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi wawajibike kwa kutoa maelezo kwa umma
kuwa ni kazi ipi wanayofanya ikiwa madawa ya kulevya yanaingizwa nchini
na kusafirishwa nje ya nchi kwa kasi kubwa zaidi?
HITIMISHO: Ni
vema kama taifa tukatambua madhara ya madawa ya kulevya kwa vijana wetu ambao
ndio nguvu kazi ya taifa. Kupuuzia na kutochukua hatua kwa wahusika wa dawa za
kulevya ni kuangamiza nguvu kazi ya taifa. Nguvu kazi ya taifa ikishaharibiwa
na dawa za kulevya hatuna taifa tena. Hivyo Serikali ifahamu kwamba kuendelea
kulifumbia macho jambo hili kwa manufaa ya mafisadi wachache ni kulihujumu
taifa na huo ni usaliti dhidi ya kiapo ilichokula cha kulitumikia taifa na
kusimamia usitawi wa wananchi wa Tanzania. Aidha, Serikali itambue pia kwamba
kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua yoyote juu ya jambo hili kunatoa
dalili kwamba yamkini ya yenyewe inahusika na biashara hiyo.
MUHIMU: IKIWA SERIKALI ITAENDELEA
KUPUUZIA JAMBO HILI AMBALO LINALIANGAMIZA TAIFA, BASI KAMBI RASMI YA UPINZANI
BUNGENI ITAENDESHA OPERESHENI NCHI NZIMA ILI WANANCHI WAPIGE KURA KWA
WAHUSIKA WAKUU WA BIASHARA YA DAWA ZA KULEVYA, NA BAADA YA ZOEZI HILO,
TUTAANIKA HADHARANI (KWA KUWATAJA MAJINA) WAHUSIKA WA BIASHARA HARAMU YA DAWA
ZA KULEVYA.
______________________________________
Vincent Josephat Nyerere (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA
UPINZANI BUNGENI
NA WAZIRI KIVULI WA MABO YA NDANI
YA NCHI
Imetolewa leo, tarehe 16 Julai,
2013
1 comment:
HIVI KESI YA NYANI HUWA ANAPELEKEWA SOKWE KUAMUA?
Post a Comment