MWENYEKITI wa kampuni za IPP, Reginald Mengi ametoboa siri kuwa hakuna
mfanyabiashara wa Tanzania aliyefanikiwa katika biashara kubwa kwa kusaidiwa na
serikali bila ya kutoa rushwa.
Mfanyabiashara huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa
Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), alisema yeye aligoma kutoa rushwa kwa
watendaji wa serikali jambo lililosababisha kupoteza fursa nyingi ambazo
zingemfanya awe na maendeleo zaidi ya aliyonayo hivi sasa.
Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaam wakati akichangia mada
katika uzinduzi wa ripoti ya uchumi na maendeleo barani Afrika kwa mwaka 2013,
uzinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Diplomasia.
Alisema kutokanana na kukithiri huko kwa rushwa, maendeleo ya
kibiashara na kijamii hapa nchini hayawezi kufikiwa kama
jitihada za kupambana na rushwa zitapuuzwa.
“Ili ufanikiwe ni lazima uione fursa iliyopo, lakini tatizo liko wapi
mnajua… ni kwa hawa waliopewa dhamana ya kutoa vibali kuendekeza rushwa,”
alisema Mengi.
Alisema ni vigumu katika nchi iliyojaa rushwa kuzungumzia suala la
amani wakati wananchi wanapata huduma mbovu kutokana na watendaji wa serikali,
taasisi na idara zake kuendekeza rushwa.
Alibainisha kuwa idara nyingi za serikali hivi sasa zimegubikwa kwa
rushwa kiasi cha kuathiri huduma mbalimbali zitolewazo huku akitolea mfano wa
matumizi ya bajeti ya serikali ya sh trilioni 18 yaliyoidhinishwa na Bunge hivi
karibuni.
“Tunaweza kuangalia dhamira nzuri ya serikali hasa katika bajeti ya
trilioni 18, manunuzi ya umma ni asilimia 80. Kati ya hizo asilimia 20 -30
zinaweza kuishia katika mianya ya wizi na rushwa, na mambo haya yanaweza
kufanywa na watu wachache huku wengi wakiangamia kwa kukosa huduma muhimu,”
alisema.
Alisema mbali na fedha zinazopotea katika manunuzi ya umma, maeneo
mengine yanayofanya madudu kwa kiasi kikubwa ni sekta ya bandari, TANESCO na
reli ambako alibainisha kuwa wajanja wachache wanatumia fursa walizonazo kujitengenezea
mianya ya kufaidi rushwa ya maeneo hayo.
Aliongeza kuwa mianya ya rushwa isipodhibitiwa Mtanzania wa kipato cha
chini ataendelea kuumia hata kama kipato chake kitaongezeka.
Alisisitiza kuwa tatizo jingine linalochangia rushwa nchini ni Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutokutambuliwa katika katiba
pamoja na kunyimwa uwezo wa kuwashitaki watoaji na wapokeaji wakubwa wa rushwa.
Alisema katika kupambana na rushwa nguvu ya TAKUKURU inaishia katika
kuwashitaki watuhumiwa wadogo, huku wakubwa wakisubiri uamuzi wa Mwendesha
Mashtaka wa Serikali (DPP).
Mengi alisema ana wasiwasi kuwa kwa hali ilivyo sasa kwenye sekta ya
madini nchini hakuna Mtanzania atakayebaki miaka michache ijayo iwapo mambo
hayatabadilishwa.
Alibainisha kuwa sera na kauli zinazotolewa midomoni mwa viongozi
zinaelekeza kumuwezesha Mtanzania katika fursa mbalimbali wakati uhalisia wa
matendo yao hauendani.
“Viongozi wanasema mdomoni kuwa wanataka kuwawezesha Watanzania, lakini
ukweli ni kwamba kuna mkakati wa kuwarudisha nyuma kwa kasi kubwa,” alisema
Mengi.
Awali, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Felix Mosha
akiwasilisha ripoti ya uchumi na maendeleo 2013 kwa bara la Afrika alisema
ukosefu wa miundombinu bora katika bara hilo unachangia kwa kiasi kikubwa
wawekezaji kushindwa kuwekeza katika maeneo yatakayoweza kumkwamua mwananchi wa
kawaida.
Alisema nchi imefanya makosa makubwa kupuuzia kilimo cha kisasa na
kukimbilia kuwekeza katika sekta nyingine huku ikiwaacha watu takribani
asilimia 80 katika mbio za kuelekea katika mafanikio.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani na katika Afrika ni kati ya
tano bora ambayo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa, lakini wananchi wake
wanaendelea kuwa katika hali duni. Hii ni kwa kuwa uwekezaji unafanywa katika
maeneo yasiyowashirikisha wananchi moja kwa moja,” alisema Mosha.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment