Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameamuru
majambazi na wahamiaji haramu wote katika mikoa mitatu nchini kujisalimisha
katika muda wa siku 14 kuanzia, Ijumaa, Julai 26, 2013 kabla ya kuanza kwa
operesheni kubwa kuliko zote katika historia ya Tanzania nyenye lengo la
kukomesha ujambazi katika mikoa hiyo na kukamata wahamiaji haramu.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu
amesema kuwa leo ametoa amri kwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama nchini
kuanza maandalizii ya operesheni hiyo na hatimaye kuiendesha katika Mikoa ya
Kagera, Kigoma na Geita.
“Majambazi wanateka magari, wanaua watu wetu,
wanapora mali zao. Watanzania hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu, woga na taabu
katika nchi yao wenyewe. Tutawasaka majambazi misituni, tutawasaka majumbani,
tutachimbua ardhini kutafuta hata silaha zilizofukiwa chini,” amesema Rais
Kikwete.
Rais Kikwete ametoa amri hiyo mchana wa jana,
Ijumaa, Julai 26, 2013 wakati alipohutubia wananchi wa mjini Biharamulo, Mkoani
Kagera, kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara ya lami kutoka
Kagoma, Wilaya ya Muleba kwenda Lusahuga, Biharamulo.
Rais Kikwete ametoa amri hiyo kufuatia matukio ya
mara kwa mara na yasiyokuwa na mwisho ya majambazi kuteka mabasi, kuua watu na
kupora mali zadi katika mikoa hiyo, hali ambayo imesababisha malalamiko ya
wakazi wa mikoa hiyo.
Rais Kikwete ameaambia wananchi: “Tumeamua
kukomesha upuuzi huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma Geita. Leo nimetoa maagizo
kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama – Jeshi la Wananchi, Jeshi la Polisi,
Uhamiaji na Usalama wa Taifa kuandaa operesheni maalum, operesheni kubwa kuliko
zote tokea tupate uhuru. Upuuzi huu hauwezi kuendelea.”
No comments:
Post a Comment