Waziri wa uchukuzi Prof. Harrison Mwakyembe
alimtaja mshukiwa mmoja wa dawa za kulevya aitaye Nassoro Mangunga na kuwataka
polisi wamtie nguvuni popote atakapoonekana....
Hata hivyo, mshukiwa huyu pamoja na picha zake
alishaandikwa na gazeti la SANI katika toleo lake la Agosti 7-9, 2013 (toleo la
1042) pamoja na namna alivyosafirisha mzigo pamoja na akina Masogange.
Hii ni taarifa ya gazeti hilo:
Unaweza kukimbia lakini huwezi kujificha. Msemo huu
unaonekana kutimia kwa kijana anayedaiwa kuambatana na watuhumiwa wa dawa za
kulevya waliokamatwa Julai 5 mwaka huu nchini Afrika Kusini, Agness Gerald
'Masogange' (25) na Melisa Edward (24), kunaswa na gazeti hili.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti hili,
wasichana hao, Masogange na Melisa walisafiri ndege moja na kijana
anayejulikana kwa jina la Nassoro Mangunga wakitoka Dar es Salaam kwenda Afrika
Kusini, wakisafiri na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA), yenye
namba SA 189.
Wakiwa katika ndege hiyo Mangunga, Agness na Melisa
walikaa kwenye viti vilivyo jirani kabisa huku Mangunga akiwa katikati yao,
kwani Agness alikaa kiti namba 23B, Mangunga alikaa kiti namba 23D na Melisa
alikaa kiti namba 23A.
Mangunga ambaye ni rafiki mkubwa wa wanamuziki wa
Bongo Flava, Rashidi Abdallah Makwiro 'Chid Benz', Mgaza Pembe 'M2theP' na
Albert Keneth Mangweha 'Mangwair', wakati akisafiri na mabinti hao walikuwa na
jumla ya mabegi tisa kama kumbukumbu za nyaraka za shirika hilo la ndege
zinavyoainisha.
Licha ya nyaraka za kusafirishia mabegi hayo
kuonesha jina la Agness Gerald ambaye ni mpenzi wa Mangunga tangu mwanzoni mwa
mwaka jana, kuwa ndiye aliyelipia mabegi hayo, ila kwenye sehemu ya anuani ya
waraka pepe, imeandikwa Mangunga.
Aidha, mabegi hayo, yalikuwa na kilo 150 za dawa za
kulevya lakini kila mmoja alitakiwa kusafiri na kifurushi cha kilo ishirini
kama mzigo wa mkononi ambao husafiri bila malipo, hivyo watatu hao kwa pamoja
walikuwa na kilo sitini wote kwa pamoja, hivyi kubaki kilo 90 ambazo
walizozilipia Dola za Marekani 94 badala ya Dola 450.
Mangunga ambaye licha ya kuishi zaidi nchini Afrika
Kusini, lakini pia ni mkazi wa maeneo ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Agness na Melisa, walikamatwa Julai 5, 2013 katika
Uwanja wa Ndege wa Oliver Thambo, Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya zenye
uzito wa kilo 150 aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya Sh bilioni
6.8 za Kitanzania, na walipotiwa mbaroni, walikuwa na mabegi sita tu kati ya
tisa waliyokuwa nayo wakati wanapanda ndege jijini Dar es Salaam.
Inasemekana mabegi hayo matatu yaliondoka na
Mangunga na kutokomea kusikojulikana...
No comments:
Post a Comment