Monday, September 09, 2013

Bi.Erna Solberg, Waziri Mkuu mteule wa Norway. Jens Stoltenberg amekubali kushindwa na amempongeza Bi.Solberg. Tunampongeza Bi.Erna Solberg



Inaelekea kuwa Bi. Erna Solberg wa chama cha wahafidhina "The Conservative" (Høyre kifupi H) atakuwa Waziri Mkuu wa Norway baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatatu, 09.09.2013.

Lakini H hawataweza kuunda serikali peke yao. Itabidi waunde mseto ama na Progressive Party (Fremskrittspartiet kifupi FrP) peke yao au pamoja na Liberal Party (Venstre kifupi V) na Christian Democratic Party (Kristelig Folkeparti kifupi KrF). 

H+FrP+KrF+V wakiunda mseto watakuwa na wingi wa wabunge kwenye Bunge la Norway; Stortinget.

Tatizo moja ni kuwa FrP+KrF+V kimsingi hawapiki chungu kimoja! Kuna mambo mengi ya kimsingi hawaelewani. 

H+KrF+V wanaweza kuunda mseto wenyewe, lakini FrP wamesema bayana kuwa hawataunga mkono mseto huo kama wao hawatashirikishwa! Lazima washirikishwe!

Kuna uwezekano kuwa vyama hivyo vinne vikakaa chini na kuamua kukubali kuunda mseto ili Labour Party (AP) wasipate kuunda serikali wenyewe. Serikali ya AP haitakuwa ya kudumu kwa sababu itategemea sana kupata kuungwa mkono Bungeni kila jambo au mswada utakaopitishwa kitu ambacho kitakuwa taabu. Serikali ya AP pekee ni kitu ambacho hakitegemewi sana.

Hivyo basi Bi. Erna Solberg atakuwa Waziri Mkuu mpya wa Norway. Bi. Solberg atakuwa mwanamke wa pili kuwa waziri mkuu hapa Norway.

Wa kwanza alikuwa Bi. Gro Harlem Brundtland.


No comments: