MWENYEKITI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, Mbunge wa
Sengerema (CCM), William Ngeleja na Mfanyabiashara maarufu, Rostam Aziz,
wamehojiwa kuhusu kuwa na utajiri mkubwa nje ya nchi.
Wanasiasa
hao wamehojiwa na kikosi kazi maalumu kilichoundwa na serikali hivi karibuni
kwa ajili ya kutafuta mali mbalimbali zilizofichwa nje ya nchi na watu
mbalimbai wenye nyadhifa kubwa.
Ingawa
watendaji wakuu wa kikosi kazi hicho wamekataa kuthibitisha au kukana kuhusu
kuhojiwa kwa wanasiasa hao, Raia Mwema limeambiwa wanasiasa hao ni sehemu tu ya
watu zaidi ya 100 wanaochunguzwa na vyombo vya dola.
Kikosi
hicho kiliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na kinaongozwa na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah na wawakilishi
kutoka Jeshi la Polisi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na waatalamu wa masuala ya
kibenki.
Chanzo cha
kuaminika cha kilisema Mbowe ambaye pia ndiye Kiongozi wa Upinzani Bungeni,
alihojiwa kutokana na maelezo kuwa alinunua jumba la kifahari nchini Dubai,
Desemba mwaka 2011.
"Kutokana
na wadhifa wake kwa umma, Mbowe ilibidi achunguzwe kutokana na ununuzi wa
nyumba alioufanya nchini Dubai, Desemba mwaka 2011.
Uchunguzi
wake ni mahususi kwa sababu tumefuatilia akaunti zake na ikaonekana hakuwahi
kutumia njia ya benki kufanya malipo.
"Hii
maana yake ni kwamba kama alifanya malipo, basi alifanya kwa kutumia fedha
taslim (cash).
Sasa ni
lazima ichunguzwe maana si kawaida kwa kiongozi kama yeye kusafiri na mamilioni
yote ya kununua jumba kule Dubai na kulipa cash. Ndiyo maana yeye anafanyiwa
uchunguzi mahususi," kilisema chanzo cha kuaminika cha gazeti hili.
Rostam ni
miongoni mwa wafanyabiashara maarufu hapa nchini na Raia Mwema limeelezwa
kwamba alihojiwa kutokana na kumiliki jumba katika nchi hiyo ya Mashariki ya
Kati na imeelezwa pia kuwa ana akaunti kadhaa nje ya nchi.
Dubai ni
kimbilio la wafanyabiashara wengi kutokana na nafuu ya kodi inayotolewa na
serikali ya nchi hiyo na pia uwepo wa biashara na usalama mkubwa uliopo.
Zaidi ya
kuwa mfanyabiashara maarufu, Rostam aliwahi kuwa mbunge kupitia Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na alipata pia kuwa Mweka Hazina wa chama hicho.
Hadi
tunakwenda mitamboni, gazeti hili lilikuwa halijafahamu ni kwa sababu ya mali
zipi hasa ambazo Ngeleja anazo lakini wakati akiwa Waziri wa Nishati na Madini,
kulikuwa na minong'ono kwamba alikuwa miongoni mwa mawaziri vijana wenye ukwasi
mkubwa alioukwaa ndani ya muda mfupi.
Alipoulizwa
na Raia Mwema kuhusu alichohojiwa alipoitwa na kikosi kazi, Ngeleja alijibu kwa
ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya mkononi; "Samahani, mimi si
msemaji wa suala hilo." Hata alipoombwa na mwandishi walau kukanusha au
kukataa kuwa alihojiwa – Ngeleja alijibu kwa ufupi, "Ahsante."
Kwa sasa,
waziri huyo wa zamani wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete yuko safarini nje ya
nchi.
Alipotafutwa
wiki hii kueleza upande wake kuhusu alichohojiwa, Rostam hakujibu simu wala
ujumbe mfupi wa maneno aliotumiwa na mwandishi.
Mbowe
hakuwa tayari kueleza kuhusu kuhojiwa huko ingawa Ofisa Habari wa CHADEMA,
Tumaini Makene, aliyeeleza kuwa ameagizwa kujibu kwa niaba ya mkuu huyo wa
upinzani, alisema; "si jambo la ajabu kwa Mbowe kuwa na mali nje ya nchi
kwa vile ni mfanyabiashara na ana biashara hadi nje ya nchi."
Kikosi kazi
kinafanya kazi zake katika mazingira ya usiri na tangu kilipoanza kazi mapema
mwaka huu, hakijawahi kutoa taarifa rasmi kuhusu shughuli zake.
Mmoja wa
wajumbe wa kikosi kazi hicho, Dk. Hoseah alikataa kuzungumza chochote kuhusu
watu waliowahoji kwa maelezo kuwa msemaji wa shughuli yao ni Werema.
Werema
hakutaka kukana wala kuthibitisha taarifa hii isipokuwa katika mazungumzo ya
nyuma na vyombo vya habari aliwahi kusema kwamba ni kinyume cha maadili kwa
tume hiyo kutoa taarifa kuhusu watu iliowahoji.
Novemba
mwaka jana, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, alitoa hoja
binafsi bungeni akitaka ufanyike uchunguzi wa fedha na mali haramu kutoka
Tanzania zilizofichwa katika nchimbalimbali duniani.
Kwa mujibu
wa sheria za Tanzania, raia wake hawaruhusiwi kufungua akaunti katika nchi za
kigeni pasipo ruhusa ya ofisi ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Katika hoja
yake binafsi, Zitto alitaka Bunge lipewe nguvu ya kuunda Kamati Teule ambayo
itachunguza na kubaini ni akina nani wanamiliki akaunti na mali ughaibuni
lakini serikali iliamua yenyewe kuwa ndiyo itafuatilia kwa kutumia vyombo vyake.
Chanzo: Raia
Mwema
No comments:
Post a Comment