Baada ya uchaguzi mkuu Norway wiki mbili zilizopita, Høyre (The Conservative Party), Fremskrittspartiet (The Progress Party), Kristelig Folkeparti (The Christian Democratic Party) na Venstre (The Liberal Party) vilipata ushindi wabunge 96 jumla na kuwa na wingi wa Wabunge kwenye Bunge la Norway Stortinget lenye wabunge 168.
Kwa wiki mbili vyama hivyo vimekuwa na mazungumzo ya kuona kama pana uwezekano wa kuunda serikali ya mseto ya vyama vinne.
Viongozi wa vyama hivyo vinne, Bi. Erna Solberg (Waziri Mkuu mteule toka Høyre, H), Bi.Siv Jensen wa Fremskrittspartiet (FrP), Bi. Trine Skei Grande wa Venstre (V) na Bw. Knut Arild Haraide wa Kristelig Folkepartiet (KrF), jana usiku kwenye mkutano wa vyombo vya habari, wamesema; wamekubaliana na kutia saini kuwa Høyre na Fremskrittspartiet waendelee na mazungumzo ya jinsi gani wataunda serikali ya mseto ya vyama viwili kati ya Høyre na FrP, huku KrF na Venstre vibaki nje ya mseto huo, lakini wawe wanawaunga mkono wenzao kwenye masuala ya kila siku Bungeni ili kwamba mseto huo uweze kudumu angalau kwa miaka minne ijayo hadi uchaguzi mkuu mwaka 2017.
Kiitikadi FrF na Venstre vinafanana fanana lakini viko mbali sana na FrP. Hizo tofauti za kiitikadi ndizo zilizofanya KrF na Venstre kushindwa kukubali kuwa kwenye serikali ya mseto na FrP. (Angalia:
http://www.krf.no/ikbViewer/page/krf/politikk/english na http://www.venstre.no/sentralt/artikkel/981/).
Masuala kadhaa yakiwemo la haki za binadamu wote, wahamiaji na misaada kwa nchi zinazoendelea (KrF) na la mazingira (Venstre) na muhimu kwa vyama hivyo na wako tofauti sana na FrP. FrP kimepata lebo ya kuwa chama kisichopenda watu wenye asili za nchi zingine wanaoishi Norway na kingependa kuziba vyufa zote zinazowafanya wageni na watu wanaokuja kuomba hifadhi za kikimbizi kuja na kuingia kirahisi hapa Norway.
Licha ya kuwa kuna masuala kadhaa yamefanya KrF na Venstre kuamua kukaa nje ya mseto utakaoundwa, lakini kuna mambo mengi tu yao wamekubaliana na Høyre na FrP kuwa japo watakuwa nje ya mseto, lakini serikali ya mseto iyashughulikie.
Kwenye makubaliano hayo (yako kwenye Kinorwejiani: Avtale mellom mellom Venstre, Kristelig Folkepartiet, Fremskrittspartiet og Høyre), vyama hivyo vimekubaliana mengi, baadhi ni haya:
- Kuhakikisha kuwa serikali ya mseto ya Høyre na Fremskrittspartiet inadumu angalau kwa kipindi hadi uchaguzi mkuu ujao.
- Kushauriana kwa lolote lile kabla serikali ya mseto kuliamua.
- Kupunguza urasimu kwenye ofisi za manispaa na za serikali.
- Kuona kama pana uwezekano wa kupunguza manispaa 428 za Norway
- Kuongeza ubora wa matibabu kwa wanaotumia madawa ya kulevya na kuona uwezekano wa kununua nafasi za matibabu kwenye hospitali na taasisi binafsi.
- Kuhakikisha ubora wa elimu mashuleni na vyuoni.
- Kujenga kwa kasi na kurabati njia za mawasiliano na usafiri.
- Kuongeza uwezo wa usafiri wa umma kwenye miji mikubwa.
- Kuongeza askari kwenye jeshi la polisi.
- Kuona kama pana uwezekano wa kuongeza matumizi ya nchi kutoka kwenye mfuko wa mali asili ya mafuta.
- Kina baba kuongezewa mapumziko ya wiki 10 kama wakizitaka, mama wazazi anapojifungua.
- Kuacha kuendelea na utafiti wa kuangalia kuwepo kwa mafuta na gesi kwenye ukanda wa kaskazini ya Norway.
- Hela za mara moja anazopewa mama mzazi akijifungua kuongezeka.
- Somo kwenye shule za msingi lililokuwa linaitwa RLE (religion, livssyn og etikk = Religion, Lifestyle and Ethics) litabadilishwa na kuitwa KRLE (Kristendom, religion, livssyn og etikk = Christianity, Religion, Lifestyle and Ethics)
Wamekubaliana kuwa watu wote wanaokuja kuomba hifadhi ya kisiasa na kikimbizi hapa Norway watakuwa wanawekwa kwenye kambi za aina mbili.
Moja: Kwa wale ambao wataonekana kuwa wana nafasi ya kukubaliwa hifadhi watawekwa kwenye kambi zao.
Mbili: Wale wanaonekana hawana nafasi ya kupewa hifadhi watawekwa kwenye kambi za aina yao, tayari kwa kurudishwa walikotoka.
Sheria za uhamiaji zitakazwa kamba na kuzibwa nyufa pale patapoonekana pana nyufa.
na
Mwamedi Semboja.
Oslo.
No comments:
Post a Comment