Mheshimiwa Anne Makinda,
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt.
Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo
Pinda, Waziri Mkuu;
Waheshimiwa Mawaziri na
Naibu Mawaziri;
Mheshimiwa Freeman
Mbowe, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni;
Waheshimiwa Wabunge;
Mabibi na Mabwana;
Nakushukuru sana
Mheshimiwa Spika kwa kukubali ombi langu na kutenga muda wenu ili niweze
kuzungumza na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuhusu masuala muhimu kwa uhai,
ustawi na maendeleo ya nchi yetu na watu wake.
Mheshimiwa Spika;
Nimeambiwa kuwa
taarifa ilipotolewa kuwa ninaomba kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wabunge,
kumekuwepo na dhana mbalimbali. Wapo waliodhani kuwa nakuja kuzungumzia
mchakato wa kuunda Katiba mpya na hasa matukio ya wiki chache zilizopita. Wapo waliodhani nakuja kuzungumzia “Operesheni Tokomeza”. Tena wapo
waliokwenda mbali na kufikiria kuwa nakuja kuwakaripia Waheshimiwa Wabunge
waliotoa maoni yao kuelezea kasoro zilizojitokeza katika utekelezaji wa
Operesheni hii muhimu. Na wapo pia waliodhani ninakuja kuzungumzia ushiriki wa
majeshi yetu ya Tanzania katika Jeshi la Kulinda Amani la Umoja wa Mataifa
nchini Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Hayo si
makusudio yangu. Kinachonileta mbele ya Bunge lako Tukufu ni kuzungumzia
Jumuiya ya Afrika Mashariki na mustakabali wa Tanzania katika Jumuiya
hiyo. Lakini, kwa sababu ya umuhimu wa masuala hayo niliyoyataja na rai
niliyopewa kuwa niyasemee japo kidogo. Nimeona ni vyema nifanye hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu mchakato wa Katiba mpya, napenda
kusema kuwa tumefikia hatua nzuri katika utekelezaji wake. Kama mjuavyo
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imekamilisha, kwa mafanikio, hatua ya mwanzo ya
kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka. Pia walishatoa
Rasimu ya Kwanza ya Katiba na kukamilisha mchakato wa Mabaraza ya Katiba. Kinachosubiriwa kwa hamu na sisi wote, ni Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo
inatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 15 Desemba 2013 au kabla ya hapo.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa
Bunge lako Tukufu, tunategemea kupata mambo mawili kutoka kwenu yatakayowezesha
mchakato kutekelezwa vizuri katika hatua zinazofuata. Jambo la kwanza ni
kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na pili kufanyika kwa marekebisho ya nyongeza
ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kuhusu Bunge Maalum ili kuboresha utekelezaji
wake. Baada ya Bunge kukamilisha kazi yake hiyo itafuatia uteuzi wa
Wajumbe wa Bunge Maalum ili kazi ya kujadili Rasimu ya Pili ya Katiba ifanyike
na kutupatia Rasimu ya Mwisho. Rasimu ambayo ikikubaliwa na wananchi katika
Kura ya Maoni itakayofanyika wakati wo wote mwakani, tutakuwa tumepata Katiba
Mpya. Hivi sasa katika Serikali tunaendelea kufanya tafakuri na
tunachukua hatua za kuwezesha Bunge Maalum na Kura ya Maoni kufanyika kwa
mafanikio.
Operesheni Tokomeza
Mheshimiwa Spika;
Napenda
kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lako Tukufu kuwa sikukasirishwa na
maoni yao kuhusu madai ya kuwepo kasoro katika utekelezaji wa Operesheni
Tokomeza. Shabaha ya Operesheni hii ni kuokoa maliasili za misitu na
wanyamapori dhidi ya uvunaji haramu ambao umefikia kiwango kinachotishia
kutoweka kwa raslimali hizo. Kwa kweli hali inatisha. Miti
inakwisha na ndovu na faru wanaangamia.
Mheshimiwa Spika;
Wakati, tunapata
Uhuru Tanzania ilikuwa na ndovu waliokadiriwa kuwa takribani 350,000.
Lakini, kwa sababu ya ujangili uliokithiri katika miaka ya 1970 na 1980 ilipofika
mwaka1989 kulikuwa na ndovu wapatao 55,000 tu.
Ilipofikia hali hiyo Serikali ikaanzisha Operesheni Uhai iliyohusisha Jeshi la
Ulinzi na kuongozwa na Meja Jenerali John Walden (ambaye sasa ni
marehemu) kuendesha mapambano dhidi ya majangili. Kutokana na hatua hiyo na
uamuzi wa Shirika linalosimamia biashara ya wanyama walioko kwenye hatari ya
kutoweka (CITES) kupiga marufuku biashara ya pembe za ndovu duniani, idadi ya
ndovu nchini iliongezeka na kufikia 110,000 mwaka 2009.
Tumewaomba Fankfurt Zoological Society ambao ni
wabia wetu katika uhifadhi wa wanyama pori kwa miaka mingi wafanye sensa maalum
ya ndovu katika Hifadhi ya Selous na kote nchini ili tujue hali halisi
ikoje. Kazi hiyo inaendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya mwaka 2009 kumezuka
wimbi jipya, tena la nguvu kubwa, la kuua ndovu na faru nchini na kwingineko
katika Bara la Afrika ambako wanyama hao wapo. Idadi kubwa ya meno ya
ndovu yaliyokamatwa na yanaoendelea kukamatwa nchini na kwingineko duniani
inathibitisha ukweli huo. Kwa mfano, kati ya mwaka 2010 na Septemba,
2013, hapa nchini, kwa jitihada zetu vipande 3,899 vya pembe
za ndovu vyenye uzito wa kilo 11,212 na vipande 22 vya
pembe za ndovu zilizochakatwa zenye uzito wa kilo 3,978vilikamatwa.
Aidha, katika kipindi hicho vipande 4,692 vya pembe za ndovu
vilivyotokea Tanzania vyenye uzito wa kilo 17,797vilikamatwa nje ya
nchi.
Mheshimiwa Spika;
Kama
nilivyokwisha sema hapo awali matatizo ya kuuawa kwa wingi kwa ndovu na faru
lipo pia katika nchi nyingine Afrika zenye wanyama hao. Nchi za
Gabon, Kenya, Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Uganda, Zimbabwe,
Zambia na nyinginezo nazo zinakabiliwa na matatizo kama yetu. Tatizo
limekuwa kubwa kiasi cha kuifanya Jumuiya ya Kimataifa kushtuka na kuamua
kuingilia kati kwa namna mbili. Kwanza kuunga mkono juhudi za uhifadhi wa
ndovu na faru katika nchi zenye wanyama hao. Na, pili, kuchukua hatua
thabiti kudhibiti biashara ya meno ya ndovu duniani. Ni ukweli ulio wazi
kuwa kama hakutakuwepo na wanunuzi wa meno ya ndovu na faru hakuna ndovu au
faru atakayeuawa.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na ukweli ulivyo uamuzi wetu wa
kuendesha Operesheni Tokomeza ni sahihi kabisa. Manufaa yaliyopatikana
baada ya Operesheni Uhai ya mwaka 1989 yanatupa imani kuwa na
safari hii pia tutafanikiwa. Tusipochukua hatua kama hii sasa ni sawa na
kuwapa kibali majangili waendelee kumaliza ndovu na faru nchini. Hakika
wanyama hao watakwisha. Itakuwa ni aibu kubwa kwetu na historia
itatuhukumu vibaya.
Mheshimiwa Spika;
Tumeyasikia
maelezo ya Wabunge kuhusu kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika utekelezaji
wa Operesheni Tokomeza. Nawaahidi kuwa tutayafanyia kazi. Serikali
imeahirisha kwa muda Operesheni hii ili kujipa muda wa kurekebisha kasoro hizo
na kujipanga upya. Watendaji wasiokuwa waadilifu na wale wasiokuwa
waaminifu wataondolewa. Halikadhalika, kasoro za kimfumo nazo
zitasahihishwa ili tutakapoanza upya Operesheni itekelezwe kwa mafanikio
yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika;
Miongoni mwa
mambo yaliyozungumzwa kwa uchungu ni ukamataji wa mifugo iliyokutwa kwenye
mapori ya hifadhi za wanyama na vitendo vibaya walivyofanyiwa wenye mifugo na
mifugo yenyewe. Narudia kusisitiza kuwa taarifa zote hizo zitafanyiwa
kazi na waliohusika watachukuliwa hatua zipasazo. Pamoja na hayo, napenda
kuwakumbusha ninyi watunga sheria wetu kuwa sheria ya hifadhi za wanyamapori
hairuhusu mifugo kuchungwa katika maeneo ya hifadhi.
Naomba tuwakumbushe wananchi tunaowaongoza
wajiepushe na kufanya hivyo. Ni uvunjifu wa Sheria za nchi. Naomba
pia, wananchi waelimishwe ili wajue kuwa wakifanya hivyo na kukutwa katika
maeneo hayo na mifugo yao kuna adhabu iliyotamkwa kwenye sheria.
Hivyo tusiwalaumu wala kuwaona maafisa wanyamapori kuwa ni watu wabaya. Wanatekeleza Sheria iliyotungwa na Bunge hili. Pale wanapotenda visivyo
tuseme, watawajibishwa ipasavyo.
Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo
Mheshimiwa Spika;
Mapema mwaka huu
(2013) Umoja wa Mataifa uliomba nchi yetu ichangie kikosi kimoja cha wanajeshi
katika Brigedi Maalum iliyoundwa na Umoja huo kuongeza nguvu ya kudhibiti waasi
Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo la msingi ni
kuiwezesha nchi hiyo kupata amani ya kudumu ambayo imekosekana kwa muda mrefu
kutokana na kuibuka kwa uasi mara kwa mara.
Mheshimiwa Spika;
Tulikubali,
kwani hata kabla ya kuombwa na Umoja wa Mataifa tulishakubali maombi kama hayo
yaliyotolewa kwenye Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Ni miezi saba (tangu
Aprili) sasa tangu wanajeshi wetu waende Kongo na wamekuwa wanatekeleza
majukumu yao vizuri tena kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu. Sifa hiyo
kwa wanajeshi wetu imekuwa inatolewa na viongozi wa juu wa Umoja wa Mataifa,
viongozi wa juu wa Jeshi la Umoja wa Mataifa Kongo (MONUSCO) na viongozi wa juu
wa Serikali ya Kongo.
Mheshimiwa Spika;
Majeshi ya Umoja
wa Mataifa hupewa majukumu na mamlaka ya namna mbili. Yapo yanayopewa
jukumu la kulinda amani tu. Wanajeshi wake huwa hawapewi majukumu ya
kimapigano na hata pale wanaposhambuliwa wanatakiwa kujihami tu. Kwa
kawaida majeshi yenye jukumu hili hupelekwa mahali ambapo kumekuwepo na
makubaliano ya kuacha mapigano. Wanapelekwa kusaidia kuona Mkataba
unatekelezwa ipasavyo.
Aina ya pili ni ile ya majeshi yanayopelekwa
mahali ambapo hakuna amani hivyo wanapewa jukumu la kuchukua hatua za kufanya
amani ipatikane. Majeshi haya hupewa mamlaka ya kutumia nguvu ya kijeshi
dhidi ya wanaosababisha amani ikosekane kama ni lazima kufanya hivyo.
Maana yake ni kwamba wanayo ruhusa kuingia katika mapigano dhidi ya watu au
vikundi vinavyovuruga amani. Tofauti na wenzao wa kundi la kwanza,
wanajeshi wa kundi la pili wako kwenye hatari zaidi ya kupoteza maisha au
kujeruhiwa kuliko wenzao ingawaje wapo wengi nao wameuawa na kujeruhiwa.
Mheshimiwa Spika;
Wanajeshi wetu wamekwenda Kongo chini ya utaratibu
huu wa pili ambao unahusu kuingia kwenye mapigano dhidi ya waasi kama hapana
budi kufanya hivyo. Wametekeleza majukumu yao vyema na kwa ujasiri
mkubwa na weledi wa hali ya juu. Bahati mbaya tumepoteza vijana wetu watatu
shupavu. Daima tutawakumbuka na tutawaenzi ipasavyo mashujaa wetu
hawa. Tuzidi kuwaombea kwa Mola awape mapumziko mema. Ameen.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Spika, napenda kutumia
nafasi hii kumpongeza Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kwa mafanikio ya kihistoria waliyoyapata hivi majuzi dhidi ya waasi wa
M23. Tunamtakia yeye na wananchi wa Kongo kila la heri katika kazi ngumu
iliyo mbele yao ya kujenga upya eneo hilo na kujenga mahusiano mapya miongoni
mwa watu wa Kongo. Pia nawapongeza sana wanajeshi wa Brigedi Maalum ya
Umoja wa Mataifa kwa kazi nzuri waliyoifanya iliyowezesha mafanikio
kupatikana. Wanajeshi hao ni kutoka Afrika Kusini, Tanzania na
Malawi wanaoongozwa na Brigedia Jenerali James Aloisi Mwakibolwa wa JWTZ.
Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyosema
awali, haya mambo matatu siyo hasa makusudio yangu nilipoomba kuja kuzungumza
na Waheshimiwa Wabunge wetu. Nimeyachomekea tu kwa sababu ya umuhimu wake
katika jamii kwa wakati tulio nao. Jambo lililonileta hapa leo ni
kuzungumzia hali ilivyo sasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na nafasi ya
Tanzania katika Jumuiya hiyo. Nimeona nifanye hivyo kutokana na maswali
mengi ambayo Watanzania wanajiuliza kufuatia matukio ya hivi karibuni ya
viongozi wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani Uganda,
Rwanda na Kenya kukutana bila ya ushiriki wa viongozi wa Tanzania na
Burundi. Viongozi wenzangu hao wamefanya mikutano mitatu yaani: tarehe
24-25 Juni, 2013 mjini Entebbe, Uganda; tarehe 28 Agosti, 2013 mjini Mombasa,
Kenya; na tarehe 28 Oktoba, 2013 mjini Kigali, Rwanda.
Mheshimiwa Spika;
Naomba kwanza
niweke wazi jambo moja, kwamba nchi mbili wanachama au zaidi hazikatazwi kuwa
na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo mbalimbali. Hata sisi
Tanzania tunao ushirikiano wa namna hiyo na nchi zote wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Lakini, nchi wanachama zinatakiwa kufanya hivyo kwa
yale mambo ambayo hayako kwenye shughuli za Jumuiya kwa maana kwamba hayamo
katika Mkataba au Itifaki au hakuna uamuzi wa msingi uliofanywa na vikao au
taasisi za Jumuiya kuyashughulikia. Pia, tunaweza kufanya hivyo kwa mambo
ambayo yalishaamuliwa na Jumuiya yatekelezwe na ruhusa imetolewa kwa nchi yo
yote iliyokuwa tayari kutekeleza ama peke yake au kwa kushirikiana na nchi
nyingine.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa
matamko ya pamoja (Communique) yaliyotolewa baada ya mikutano hiyo, kuna mambo
yapatayo manane ya msingi yaliyoamuliwa kufanywa na nchi hizo kwa
lengo la kuendeleza utengamano wa nchi hizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki. Mambo hayo ni haya yafuatayo:
- Kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa hadi Kampala, Kigali na Bujumbura.
- Ujenzi wa Bomba la Mafuta la kutoka Kenya hadi Uganda na Sudani ya Kusini.
- Kujenga Kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda.
- Kuanzisha Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutekelez vipengele vyote;
- Kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki na kwamba itaundwa Kamati ya kuanda rasimu ya Katiba ya Shirikisho.
- Kuharakisha uanzishwaji wa Visa ya pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (Single East African Community Tourist Visa);
- Kuandaa utaratibu wa kutumia vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao; na
- Kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika;
Ni dhahiri
kwamba orodha hiyo imechanganya mambo yale ambayo ni ya Jumuiya na yale yasiyo
ya Jumuiya. Kwa mfano, mambo manne kati ya hayo manane hayamo
kwenye masharti ya kutokufanyika bila ya kuihusisha au kupata ridhaa ya Jumuiya
ya Afrika Mashariki. Jambo la kwanza ni uzalishaji na usambazaji wa
umeme. Ni kweli kwamba tunao mkakati wa kuwa na akiba ya pamoja ya nguvu
ya umeme (East African Power Pool). Hata hivyo, bado jukumu la kuzalisha
na kusambaza umeme huo limeachiwa nchi wanachama zenyewe kuamua. Lakini,
hivi ndugu zetu hawa wanao muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao
kimsingi umebuniwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni
wanachama?
Jambo la pili, ni ujenzi wa kiwanda cha kusafisha
mafuta nchini Uganda. Hili si suala la Jumuiya bali la nchi ya Uganda
kuamua yenyewe peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine. Rais
Yoweri Museveni alituarifu mpango huo na sote tuliupokea kwa furaha kwamba sasa
tutapata mafuta karibu na nyumbani. Alitualika kushiriki katika
ujenzi wake sijui sasa amebadili mawazo kwamba Tanzania siyo muhimu.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la tatu ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka
Kenya hadi Sudani ya Kusini na Uganda. Hili si jambo linalobanwa na
masharti ya Jumuiya. Ni juu ya nchi hizi tatu kuamua kufanya ili kuwezesha
mafuta yao kufika kwenye masoko. Hata hivyo, nimeambiwa kuwa Jumuiya
imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa
nalo lifike Tanzania kupitia upande wa Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika ujenzi wa
bomba hilo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la nne ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka
Mombasa – Kampala – Kigali – Bujumbura. Hili nalo hatuna tatizo
nalo. Si mradi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ni jambo lililo chini ya
mamlaka ya nchi wanachama husika. Hata hivyo, ni vyema kutambua ujenzi wa
miundombinu ya reli, barabara na usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za
Afrika Mashariki ni miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa
na Jumuiya yetu. Jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana
tuna East African Railway Masterplan, tuna East African Road Network, na tuna
Lake Victoria Development Programme kwa ziwa Victoria.
Kwa ajili hiyo, nilitegemea kuwa reli ya kutoka
Mombasa hadi Kigali na Juba ingekuwa na tawi linalounganisha reli hiyo na reli
ya Tanzania kama ilivyo reli ya Moshi – Voi – Taveta aliyotuachia mkoloni.
Tulitegemea hivyo kwa minajili ya kuunganisha soko la Afrika Mashariki ambapo
naamini Tanzania ni mdau muhimu. Lakini inaelekea kwa maoni ya wenzetu
hivyo sivyo.
Mheshimiwa Spika;
Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila
sababu ya kuuliza kwa nini wenzetu wameamua kufanya hivi. Kumetokea nini
toka tukutane pale Arusha Aprili 28, 2013 na Juni 24, 2013 walipokutana kuamua
kufanya mambo ya kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa
kubaguana, Haijawahi kuwa hivi kabla.
Mheshimiwa Spika;
Katika mambo manne yaliyosalia ambayo yaliamuliwa na kuwekewa utaratibu wake wa
utekelezaji na Jumuiya ya Afrika Mashariki mawili hatuna maneno nayo.
Mambo hayo ni matumizi ya vitambulisho vya taifa kama hati ya kusafiria na Visa
ya Pamoja ya Utalii kwani tuliamua kwa pamoja kuwa nchi wanachama zilizokuwa
tayari waanze. Lakini, kwa upande wa kuanzishwa kwa Himaya Moja ya Ushuru
wa Forodha (Single Customs Territory) na Shirikisho la Afrika Mashariki
tunadhani wenzetu wamekiuka uamuzi wetu wa pamoja.
Mheshimiwa Spika;
Katika Mkutano Maalum wa 11 wa Wakuu wa Nchi wanachama uliofanyika tarehe 28
Aprili, 2012 Jijini Arusha, tulipokea na kuridhia mapendekezo ya kuanzisha
Himaya Moja ya Ushuru wa Forodha (Single Customs Territory). Kwa mujibu wa
mapendekezo hayo kila nchi mwanachama itasimamia shughuli zake za kiforodha na
kukusanya mapato yake kama ilivyo sasa. Hata hivyo, kwa bidhaa
zinazopitia nchi moja kwenda nchi nyingine mwanachama, ukaguzi na ukusanyaji wa
mapato utafanyika katika kituo cha kwanza bidhaa hizo zinapoingilia.
Mapato hayo yatawasilishwa kwa nchi husika baada ya kuthibitisha kuwa bidhaa
zilivuka mpaka.
Mheshimiwa Spika;
Kutokana na uamuzi huo, Wakuu wa Nchi waliagiza
Baraza la Mawaziri kuunda Kikosi Kazi cha kujadiliana na kuandaa utaratibu wa
utekelezaji wa mfumo huo. Taarifa ya kikosi kazi inatakiwa kutolewa
katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi utakaofanyika Kampala, Uganda tarehe 30
Novemba, 2013. Iweje leo nchi tatu wanachama ziamue peke yao kuanza kutekeleza?
Wanatekeleza nini na kwa nini wafanye hivyo?
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki hadithi yake inafanana na hii
ya Himaya ya Forodha. Katika Mkutano wa 14 wa Wakuu wa Nchi
wanachama uliofanyika tarehe 30 Novemba, 2012, Nairobi, tulipokea taarifa ya
hatua iliyofikiwa kuhusu mchakato wa kutaka kuanzishwa kwa Shirikisho. Mkutano
huo uliagiza nchi wanachama kujadiliana zaidi kuhusu mpango kazi wa kufikia
Shirikisho la Kisiasa na mpango wa kutekeleza mapendekezo mengine yaliyotolewa
na Timu ya Wataalamu. Inategemewa kuwa Baraza la Mawaziri litawasilisha
mapendekezo ya majadiliano hayo katika Mkutano wa 15 wa Wakuu wa Nchi mwezi
Novemba, 2013. Iweje leo wenzetu hawa waamue kuanzisha mchakato wao wa
kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Kwa kweli huwa najiuliza
maswali mengi na kukosa majibu kuhusu nini kinachoendelea kufanywa na viongozi
wenzangu watatu na kwa nini! Nakosa majibu ya uhakika. Je wenzetu
wamekosa imani na Jumuiya ya Afrika Mashariki na je wanataka kuunda yao?
Je wanaichukia nchi yetu na hivyo wameamua kutufanyia vitimbi tutoke! Au
sijui wanachuki na mimi! Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa
hatuna mpango wa kutoka (kama vijana wasemavyo hatoki mtu hapa).
Tupo na tutaendelea kuwepo!
Mheshimiwa Spika;
Tanzania haijafanya jambo lo lote baya dhidi ya Jumuiya au nchi yo yote
mwanachama. Na ukweli ni kwamba ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na
mwaminifu kwa Jumuiya. Tunatimiza ipasavyo wajibu wetu kwa Jumuiya na
kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Sabahu ya wenzetu watatu kuamua kufanya mambo yahusuyo
Jumuiya yetu peke yao kwa kweli haieleweki.
Mheshimiwa Spika;
Tunasikia eti kuwa baadhi yao walipoulizwa kwa
nini wengine hatupo wakasema kuwa wao wametangulia na sisi tutakapokuwa tayari
tutajiunga. Yaani wana Umoja wa Waliokuwa Tayari (Coalition of the
Willing). Hivi ni nani hayuko tayari (who is not willing?)
Haiwezekani watu waitane wenyewe bila ya kutualika halafu wadai kuwa wao ndiyo
wako tayari na kujenga dhana kuwa sisi wasiotualika ndiyo ambao hatuko
tayari. Madai hayo hayana ukweli. Ni vyema waseme ukweli.
Kama walitualika tukakataa ndiyo wanaweza kusema hayo.
Mheshimiwa Spika;
Kumekuwepo na madai kutoka kwa baadhi ya wenzetu,
eti kwamba Tanzania haina moyo wala dhamira ya dhati ya kuendeleza
utengamano wa Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo inasemekana eti
nchi yetu imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kwamba Tanzania tunawachelewesha wengine kupiga hatua za haraka. Wanadai
kama siyo hivyo Jumuiya ya Afrika Mashariki ingekuwa mbali kwa maendeleo.
Maneno hayo yamekuwa yanarudiwa au kujirudia mara nyingi kiasi cha kuwafanya
baadhi ya watu wa Afrika Mashariki na hata kwingineko duniani waamini
hivyo.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kusema kwa dhati ya moyo wangu kwamba
madai hayo hayana ukweli wo wote. Isitoshe hata sababu zinazotolewa
kuthibitisha ukweli wake hazina mashiko. Hazifanani na ukweli kuhusu
Tanzania na Watanzania walivyo. Tanzania ni muumini wa dhati wa umoja na
utengamano wa nchi za Afrika Mashariki na Afrika. Tumethibitisha hivyo
kwa vitendo kwa kuunganisha nchi zetu mbili huru yaani Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika na kuwa taifa moja liitwalo Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Muungano wa nchi zetu mbili ndio pekee uliodumu kwa
muda mrefu kuliko yote Afrika.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni mwanachama mwaminifu wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki kwa maana ya kutekeleza Mkataba ulioanzisha Jumuiya hiyo, kwa
Itifaki zake na maamuzi halali ya vikao na taasisi za Jumuiya. Kama lipo
jambo ambalo hatujalifanya ilivyotakiwa itakuwa ni kwa sababu za msingi na siyo
kwa sababu ya kupuuza Jumuiya. Tunaithamini sana Jumuiya na tumeipa kipaumbele
cha juu. Hatuwezi kuhangaika kwa gharama kubwa ya muda wetu, fedha zetu
na kutoa mchango wa hali na mali kuianzisha, kujenga na kuifikisha Jumuiya hapa
ilipo halafu tuwe ni watu tunaoongoza kutokuipenda na kudhoofisha maendeleo na
ustawi wake. Ni maneno ya kushangaza na wala hayaingii akilini. Ama kweli
akutukanae hakuchagulii tusi.
Mheshimiwa Spika;
Nionavyo mimi msimamo wetu kuhusu kuharakisha Shirikisho na masuala ya ardhi,
ajira, uhamiaji, pengine ndiyo yanayotuletea hisia zisizokuwa sahihi juu
yetu. Mimi siamini kama kuna mengine. Hata hivyo, napata taabu
kuamini kwamba kutofautiana kwa mawazo katika mambo hayo kutapelekea baadhi ya
wenzetu wasipende hata kushirikiana nasi kwa mambo ambayo hayana matatizo na
tumekuwa tunashirikiana vizuri.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania imekuwa inawasihi wanachama wenzetu kuwa
tujenge Jumuiya yetu hatua moja baada ya nyingine kama ilivyo kwenye Mkataba
ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hatuna tatizo la kuongeza kasi
ya ujenzi wa Jumuiya lakini tusivuke hatua yo yote. Tusiende kasi ya
kupindukia. Mkataba unaelekeza tunaanza na Umoja wa Forodha, inafuatia Soko la
Pamoja kisha Umoja wa Kifedha na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Mheshimiwa Spika;
Ni kweli kabisa hatukuunga
mkono kuharakisha Shirikisho la Kisasa kabla ya kukamilisha baadhi ya
hatua. Na, tulifanya hivyo kwa nia njema ya kutaka Shirikisho lijengwe
juu ya msingi imara. Na, msingi huo si mwingine bali utengamano wa
kiuchumi kwa maana ya Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja na Umoja wa Kifedha
zilizojengeka vizuri na kufanya kazi ipasavyo na kunufaisha wanachama wote
sawia.
Mheshimiwa Spika;
1.
Lazima tutambue ukweli kuwa kunufaika kiuchumi ndicho kichocheo kikubwa cha
nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa Jumuiya yetu. Kama mambo ya
kiuchumi yakipangika vizuri na kila nchi ikanufaika sawia, unajenga msingi
imara kwa Shirikisho la Kisiasa kustawi na kudumu. Kama ngazi hizi tatu
za awali hazitashughulikiwa vizuri na nchi wanachama zikahisi hazinufaiki
ipasavyo, Shirikisho litayumba au kuyumbishwa hivyo kudumu kwake kutakuwa kwa
mashaka.
Mheshimiwa Spika;
Tanzania ni kati ya zile nchi zinazotaka ngazi zote za mchakato wa utengamano
zitekelezwe moja baada ya nyingine bila kuruka hata moja. Kwa msimamo na
mtazamo wetu, Shirikisho iwe ndiyo hatua ya mwisho. Na huo siyo
msimamo wangu au wa Serikali peke yake, ndiyo msimamo wa Watanzania walio
wengi.
Bila ya shaka sote tutakumbuka kuwa mwaka 2006 Wakuu wa Nchi Wanachama wa
Jumuiya waliunda Kamati Maalum katika kila nchi kukusanya maoni ya wananchi
kuhusu kuharakisha Shirikisho la Afrika Mashariki. Kwa hapa nchini Kamati
hiyo iliongozwa na Profesa Samwel Wangwe na katika taarifa yake, Kamati
ilieleza kuwaasilimia 74.4 ya Watanzania wanaunga mkono kuwepo kwa
Shirikisho lakini ni asilimia 25.4 tu ndiyo
waliunga mkono kuharakishwa kwake.
Mheshimiwa Spika;
Takwimu hizi zinaelezea ukweli kuhusu hisia za Watanzania, kuhusu kuwepo kwa
Shirikisho na kasi ya utekelezaji wake. Watanzania wengi sana wanaunga
mkono kuwepo kwa Shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka jambo hilo
lisifanywe haraka haraka. Wanataka lifanywe kwa umakini mkubwa na tuende
hatua kwa hatua kama ilivyoainishwa katika Mkataba uliounda Jumuiya ya Afrika
Mashariki.
Mheshimiwa Spika;
Sera na msimamo wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakwenda
sambamba na ile ya wananchi wa Tanzania. Ndiyo maana tumeafiki
mapendekezo ya Kamati ile ya mwaka 2004iliyoongozwa na Mheshimiwa
Amos Wako wakati ule akiwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya. Kamati hiyo
iliundwa kupendekeza namna ya kuharakisha utekelezaji wa mchakato wa utengamano
wa Afrika Mashariki.
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umetamka muda wa kutekeleza ngazi ya
Umoja wa Forodha lakini uko kimya kuhusu ngazi zilizofuata. Ili kuondoa
kasoro hiyo na kwa nia ya kuharakisha Shirikisho Kamati ilipewa jukumu la kutoa
maoni na mapendekezo juu ya namna ya kufanya hivyo. Kamati ilifanya kazi
nzuri ya kupata maoni na hisia za watu wa makundi mbalimbali katika nchi
wanachama kuhusu ujenzi wa Jumuiya na utengamano.
Mheshimiwa Spika;
Kwa upande wa Tanzania kwa mfano, Kamati ya Mheshimiwa Amos Wako ilitambua
hisia za Watanzania kuhusu ardhi na ajira na kupendekezwa kuwa masuala hayo
yabaki kwenye mamlaka ya nchi wanachama kuamua. Kuhusu mchakato wa
utengamano Kamati ilipendekeza kwanza kwamba mchakato wa ujenzi wa Umoja wa
Forodha uachwe mpaka ufike ukomo wake wa miaka mitano. Baada ya hapo muda
wa kutekelezwa ngazi zinazofuata unaweza kupunguzwa. Kwa mfano
walipendekeza kuwa matayarisho ya kuunda Soko la Pamoja yaanze hata kabla ya
mchakato wa Umoja wa Forodha kufika mwisho ili mara wakati huo ukifikiwa Soko
la Pamoja linaanze. Hivyo hivyo mara baada ya ngazi hiyo kuanza
matayarisho ya kuanza ngazi ya Umoja wa Kifedha yanaanza. Ngazi hiyo nayo
ikianza matayarisho ya kuunda Shirikisho yanaanza. Kamati pia imetoa
mapendekezo ya namna ya kufikia uamuzi kuhusu Shirikisho kwamba wananchi wa
nchi wanachama wataamua kwa kura. Tukifuata mapendekezo ya Kamati ya
Mheshimiwa Amos Wako na wenzake kama tufanyavyo sasa Tanzania haina matatizo
nayo.
Mheshimiwa Spika;
Baada ya kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na wana-Afrika Mashariki kuhusu ujenzi
wa Jumuiya yao inasikitisha kuona vinafanyika vitendo vinavyoanzisha mivutano
kuhusu mambo yaliyokwisha fanyiwa kazi na kuamuliwa. Tunapata taabu zaidi
pale watu wanapobagua wenzao na wanapofanya mambo yanayopingana na Mkataba wa
Jumuiya na Itifaki zake. Kwa kweli kama mwenendo huu hautabadilika sijui
mambo yatakuwaje mbele ya safari.
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu inapenda kuona kuwa tunakuwa na Jumuiya
ya Afrika Mashariki iliyo imara na iliyo endelevu. Jumuiya ambayo
inaendeshwa vizuri, mambo yake ni mazuri na nchi zote wanachama na watu wake
wananufaika nayo, na hivyo wanaifurahia. Tanzania haina tatizo na kuharakisha
mchakato wa utengamano, lakini tunapata taabu kuruka baadhi ya hatua kabla
hazijakamilika. Tunawaomba wenzetu kuwa makini katika kila hatua
tunayochukua. Bila ya kufanya hivyo, Jumuiya yetu itakuwa
imejengeka katika msingi dhaifu hivyo ustawi na uhai wake utakuwa na changamoto
nyingi. Hatupendi ya mwaka 1977 yatokee tena.
Mheshimiwa Spika;
Napenda kuwahakikishia kuwa
Tanzania itaendelea kushiriki katika shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake. Tutafanya kila tuwezalo
kuhakikisha kuwa Jumuiya haidhoofiki wala kufa. Na iwapo itadhoofika au
kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe kidole kuwa chanzo wala kichocheo
chake. Ndiyo maana, hatutachoka kuzungumza na wenzetu kuhakikisha kuwa
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki inaendelea kustawi.
Tutaendelea kukumbushana umuhimu wa kufanya mambo
yanayojenga na kuepuka yale yanayoweza kubomoa. Tutakumbushana umuhimu wa
kuheshimu matakwa na masharti ya Mkataba ulioanzisha Jumuiya, Itifaki zake na
maamuzi halali ya vikao rasmi na asasi za Jumuiya. Tukifanya hivyo
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki itadumu, itazidi kustawi na kunufaisha nchi
wanachama na watu wake kama yalivyo malengo na madhumuni ya kuundwa
kwake.
Mungu Ibariki Afrika
Mungu Ibariki Tanzania
Idumu Jumuiya ya Afrika Mashariki
Mheshimiwa Spika na
Waheshimiwa Wabunge;
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment