Issa Shivji, Profesa Mstaafu wa Kigoda Cha Mwalimu Nyerere.
Aibu, aibu,
aibu. … aibu ya kitaifa! Utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili
uliosababisha mateso, ukatili, udhalilishwaji, upigaji na hatimaye vifo vya
wananchi ni aibu kubwa kwa taifa letu. Sio aibu tu bali ni janga la kitaifa
linalohitaji kufanyiwa tathmini na tafakuri na wananchi wote katika ujumla wao
na kujiuliza: tunaelekea wapi?
Nini
kimesababisha vyombo vya dola na mfumo wetu wa kisiasa kukosa kabisa
uwajibikaji kiasi kwamba vyombo vilivyopewa jukumu la kuyalinda maisha, utu na
heshima ya wananchi, vigeuke kuwa watesaji na wadhalilishaji wa wananchi hao
hao! Kwa nini hatujifunzi? Kwa nini hatujirekebishi?
Katika
historia yetu tumewahi kuwa na janga kama hili mnamo mwaka wa 1976 kutokana na
Operesheni Mauaji huko Shinyanga na Mwanza. Mwalimu Nyerere aliwalazimisha
viongozi wa kisiasa, akiwemo Mzee Mwinyi, kujiuzulu na watendaji wengine,
wakiwemo wakuu wa jeshi la polisi na usalama katika ngazi ya mkoa, kuchukuliwa
hatua za kisheria na kuadhibiwa ipasavyo. Tukio la operesheni Tokomeza
linafanana sana na tukio la Operesheni Mauaji, lina sura ileile ya utesaji,
udhalilishaji, ubakaji, na uporaji wa mali ya wananchi.
Matukio mengine ya aina hiyo, japokuwa hayakuwa
makubwa kiasi hicho, yamewahi kutokea huko nyuma. Katika awamu ya pili,
1. Kulikuwa na uaaji wa wafanyakazi wa Kiwanda cha
Sukari cha Kilombero mnamo mwaka 1986, na madhara na mateso waliyoyapata
wananchi wakati wa Mwembechai. Katika awamu ya tatu ilitokea kashfa ya
waandamaji huko Pemba kuuliwa na wengine kudhalilshwa kiasi kwamba tukio hili
lilileta aibu kubwa sana kwa taifa. Kwa jumla, matukio kama haya, yaani
utumiaji wa mabavu na vyombo vya mabavu – polisi, usalama, maaskari wengine
kama wanamgambo, askari wa wanyama pori n.k. – yameongezeka awamu hadi awamu
kiasi kwamba katika awamu ya nne tunashuhudia mauaji na mateso ya wanahabari na
wananchi yakiongezeka mara dufu. Hili la operesheni Tokomeza ni kilele.
Sasa tufanyeje?
Uwajibikaji
Mawaziri wanne wamelazimishwa kuachia ngazi kwa
kubeba dhamana ya kisiasa. Na wamepongezwa! Mengi mengine yanazungumziwa kwa
mtazamo wa kichama na kisiasa. Wengine wanaenda mbali kusema kwamba Waziri Mkuu
pia anatakiwa kujiuzulu. Haya yanaeleweka kwa sababu tukio lenyewe limeamsha
hisia za watu na watu wanataka kuona waziwazi kwamba hatua za maana
zinachukuliwa kuwatuliza.
Ni kweli kabisa kwamba tukio hili ni kashfa kubwa
sana ya kitaifa. Katika mfumo wa kibunge (parliamentary system), Serikali nzima
pamoja na mkuu wa serikali, yaani waziri mkuu, wangejiuzulu na labda uchaguzi
mkuu ungeitishwa. Lakini katika mfumo wetu wa kirais (presidential
system), mkuu wa serikali sio Waziri Mkuu. Ni
2.
Rais, na rais
pia ni mkuu wa nchi. Kwa hivyo, kujiuzulu kwa Waziri Mkuu hakuna uzito.
Kwa upande mwinigine, huwezi kutegemea rais mwenyewe na serikali yake kujiuzulu
kwa sababu, rais pia ni mkuu wa nchi. Na huwezi ukawa nchi bila kiongozi mkuu;
kutakuwa na ombwe la uongozi.
Kwa upande wangu, ili kuonyesha kwamba
tukio hili linachukuliwa kwa uzito wake, na hisia za wananchi zinajibiwa
zipasavyo, mambo mawili yafuatayo yanaweza kufanyika mara moja:
Moja, Rais kuvunja Baraza lake lote la
Mawaziri, kama alivyofanya Mzee Mwinyi miaka ya tisini. Hatua hii itakaribiana
na uvunjaji wa serikali. Hii itakuwa ni dalili ya uwajibikaji wa kisiasa.
Pili, watendaji, wakiwemo wale katika
ngazi za juu, wafikishwe mbele ya mahakama kwa mashtaka ya kijinai. Mwanasheria
Mkuu amependekeza uundaji wa Tume ya Kimahakama. Hii ni njia moja wapo lakini
mara nyingi njia hii hutumika kama mbinu za kufunika kombe ili mwanaharamu
apite. Nionavyo, labda safari hii, Rais Kikwete anaweza kutumia njia mbadala ya
kuteua Mchunguzi huru (independent investigator and prosecutor) ambaye
atakusanya ushahidi na kuandaa mashtaka ya kupeleka mbele ya Mahakama.
Na katika uchunguzi huu, watendaji
wote wanaohusika, pamoja na wa kijeshi, usalama, na wa kiraia, wachunguzwe na
kushtakiwa bila kujali nyadhifa zao.
3.
Tatu, jambo hili lizungumzwe na kujadiliwa na taifa
zima kwa upana na undani wake bila kuficha au kulionea haya. Hakuna shule
muhimu ya kujifunza kuliko shule ya umma. Shule ya Umma inafundisha na pia
inasaidia kujenga maadili na uwajibikaji. Katika mijadala idara zitatajwa, watu
waovu watasemwa kwa majina, maovu yanayofichwa uvunguni yatafichuliwa
hadharani.
Mwishowe, ningependa kuligusia jambo
moja muhimu ambalo linaonekana halijaguswa hata kidogo.
Dola na matumizi ya mabavu
Dola ni taasisi ya mabavu, popote pale
duniani. Jeshi, polisi, maaskari wengine kama wa wanyama pori, wa hifadhi na
kadhalika ni vyombo vya mabavu. Vyombo hivyo vya mabavu katika dola vinapata
uhalali wa kisiasa kutumia mabavu kwa sababu vinadhibitiwa na kusimamiwa na
vyombo na viongozi wa kisiasa ambao hupata uhalali wao kutokana na kuwa
wawakilishi wa wananchi. Kwa mfano, jeshi la ulinzi hutumia mabavu kuilinda
nchi dhidi ya maadui wa nje. Uwezo wa kutangaza vita na kuingiza jeshi vitani
ni wa rais kama Amiri Jeshi mkuu; na rais ni kiongozi wa kisiasa
aliyechaguliwa, sio mwanajeshi.
Katika mfumo wowote ule ambao ni wa
kiraia, kwa maana kuwa sio wa kijeshi (military) au wa kipolisi (police state),
vyombo vya kisiasa ndio hudhibiti na kusimamia vyombo vya mabavu. Jukumu la
jeshi la ulinzi ni kuilinda nchi. Jukumu la jeshi la polisi ni kulinda amani,
4.
Wananchi na mali zao. Majukumu haya mawili ni
tofauti na yanatenganishwa kikatiba. Hayaingiliani.
Ndio maana, jeshi la ulinzi halitumiki
kudhibiti ghasia nchini. Hii ni kazi ya polisi. Katika mazingira ya kipekee
ambayo kuna hatari ya serikali kupinduliwa kwa nguvu au kama kuna uasi ndio
Jeshi la Ulinzi huingizwa mitaani. Na jambo hili hufanyika baada ya Rais
kutangaza hali ya hatari kwa mujibu wa masharti ya katiba.
Kwa hivyo, ni kinyume na Katiba na
mazoea mabaya kuliingiza jeshi la ulinzi katika mambo ya kiraia, kama vile
uhalifu au ujangili. Kufanya hivyo ni kujenga mazoea mabaya na ya hatari sana.
Kinyume na msingi huu wa kikatiba,
Operesheni Tokomeza ilichukuliwa kama operesheni ya kijeshi. Katika washiriki
2,371, wanajeshi walikuwa 885 au asilimia 37, yaani zaidi ya theluthi moja.
Polisi walikuwa 480 au asilimia 20 tu. Wengine walikuwa kutoka majeshi
mbalimbali kama la wanyapori n.k.
Pili, operesheni hii ilisimamiwa na
Jeshi la Ulinzi. Na nikinukuu maneno ya Taarifa ya Kamati ya Bunge, “Taarifa za
mwenendo wa operesheni zilikuwa zinapelekwa moja kwa moja kwa Mkuu wa Majeshi
na kwamba, hazikumfikia Waziri wa Maliasili na Utalii.” Isitoshe, viongozi wa
kisiasa kama wakuu wa wilaya na mikoa na viongozi wa kuchaguliwa kama madiwani,
hawakushirikishwa wala hawakupewa taarifa zozote kuhusu operesheni hii. Mbaya
zaidi, baadhi yao waliteswa na kudhalilishwa na maaskari waliohusika na
5.
Operesheni kiasi kwamba Mkuu wa Wilaya ya Ulanga
alijificha katika hoteli.
Kwa kifupi basi, operesheni hii
haikudhibitiwa wala kusimamiwa wala kuendeshwa kama operesheni ya kiraia
(civilian operation), badala yake iliendeshwa kama operesheni ya kijeshi
(military operation). Hili ni jambo la hatari sana na ni mazoea mabaya,
hayakubaliki katika mfumo wa utawala wa kiraia (civilian government) .
Kuchanganya jeshi la ulinzi na mambo
ya kiraia ni dhambi kubwa katika mfumo wa kisiasa tunaoufuata nchini mwetu.
Jambo hili halikubaliki kabisa!.
Kwa hivyo, inashangaza kwamba hata Kamati
ya Bunge haikuona hili na badala yake ikapendekeza kwamba Serikali iandaae
“operesheni nyingine ambayo itapangwa na kutekelezwa na Jeshi la Wananchi wa
Tanzania na Idara ya Usalama wa Taifa. ” Na hoja hii inaonekana kuungwa mkono
bila kutiliwa shaka na wabunge wetu! Maana yake nini, wabunge hawajui na
hawatambui kwa kuruhusu hili wanajenga mazoea hatari? Kama ndivyo basi ipo haja
ya wanasiasa wetu pamoja na wabunge kujielimisha zaidi jinsi serikali za kiraia
zilizochaguliwa na wananchi zinavyoendeshwa.
Angalizo! Tujihadhari, tusizoee kabisa
kutumia Jeshi la Ulinzi katika mambo ya ndani kwa sababu kwa kufanya hivyo
tutakuwa tunajenga mazoea hatarishi sana kwa mfumo wa kidemokrasia.
No comments:
Post a Comment