Askofu Dkt. Benson
Bagonza
ASKOFU wa Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk. Benson Bagonza
amesema rushwa imelifikisha taifa mahala pabaya.
Kutokana na hali
hiyo, amewataka viongozi wa dini kukemea hilo kwa nguvu zote.
Askofu Bagonza
alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na gazeti hili kuhusu sakata la
kunyimwa dhamana kwa Mchungaji Jakson Kanyiginya katika mazingira yenye harufu
ya rushwa.
Mchungaji huyo
ambaye juzi alipandishwa kizimbani akituhumiwa kumpiga mfanyabiashara Joseph
Gareba, alinyimwa dhamana baada ya mwendesha mashitaka Meja Juma Litafa
kuzikataa barua za wadhamini hadi azifanyie uhakiki na kuamuru mchungaji huyo
awekwe rumande hadi Februari 26.
Hata hivyo,
mchungaji huyo aliachiwa kwa dhamana juzi baada ya maaskofu, wachungaji na
viongozi wengine wa kanisa hilo waliokuwa kwenye mafungo kukatisha mafungo yao
na kuandamana hadi katika Kituo cha Polisi cha Karagwe kushinikiza apate
dhamana kabla ya Februari 26.
Mbali na Bagonza,
maaskofu wengine walioshiriki kwenye maandamano hayo ni Paulo Mkuta na
Nelson Kazoba ambao waliandaa tamko na kulikabidhi kwa Kamanda wa Polisi Mkoa.
Askofu Bagonza
alivilaumu vyombo vya dola na mahakama kwamba vimejaa rushwa, hasa baadhi ya
vijana waliopata ajira hivi karibuni ambao alisema wanataka mafanikio ya haraka
kupitia rushwa.
“Rushwa
imetufikisha mahala pabaya sana. Wapo vijana walioajiriwa kwenye mahakama zetu
wanasema wanapokea rushwa kwa sababu wanataka kurejesha mikopo waliyopewa na
serikali wakati wakisoma. Leo kanisa limeandamana kwa sababu mtu wetu kaguswa,
jiulize wapo wangapi wanaonewa?” alisema Askofu Bagonza.
Akizungumzia
chanzo cha mzozo huo, Askofu Bagonza alisema mfanyabiashara Gareba alikuwa na
kesi ya ardhi na kanisa tangu miaka 80 na mahakama iliagiza ardhi hiyo isiguswe
hadi kesi itakapomalizika.
Alisema mwaka jana,
mfanyabiashara huyo aliingia kwenye eneo hilo na kuanza kukata miti, lakini
waumini walipoona hali hiyo walimjulisha Mchungaji Jakson ambaye aliwachukua
polisi na kumkamata Gareba na kumuweka ndani.
Kwa mujibu wa
Askofu Bagonza, baada ya tukio hilo, mfanyabiashara huyo alienda kufungua kesi
ya kupigwa kwa siri bila kanisa kujua hadi juzi Mchungaji Jakson alipoitwa
polisi na kufikishwa mahakamani.
Kutoka Tanzania Daima.
No comments:
Post a Comment