Siku mbili
baada ya kuanza kwa Bunge hilo, baadhi ya wajumbe wametaka waongewe posho kwa
maelezo kuwa kiasi wanachopewa sasa cha Sh300,000 kwa siku hakiwatoshi kutokana
na kupanda kwa gharama za maisha Dodoma.
Wajumbe hao
walitoa kauli hiyo jana katika kikao cha kuwasilisha na kujadili rasimu ya
kanuni za Bunge hilo ambacho kilianza saa nne asubuhi.Kwa kiasi kikubwa, kikao
hicho ambacho awali waandishi wa habari walizuiwa kuingia, kilitawaliwa na hoja
ya kuongezwa kwa posho za wajumbe na kuungwa mkono na wajumbe wengi bila
kufuata utaratibu maalumu uliokuwa ukisisitizwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge
la Katiba, Pandu Ameir Kificho.
“Wajumbe wengi
walikuwa wakisimama na kutaka kuzungumza bila kufuata utaratibu maalumu. Jambo
hilo liligeuza ukumbi wa Bunge kuwa kama soko,” kilisema chanzo chetu. Baadhi
ya wajumbe waliopata nafasi ya kuzungumzia nyongeza ya posho hizo ni Mbunge wa
Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi na Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa.
Katika
ufafanuzi wake kwa waandishi wa habari, baada ya kikao hicho kuahirishwa kwa
muda, Ndassa alisema: “Bunge ndiyo linalotengeneza Katiba ya nchi. Nasikitika
kuwa kiwango cha fedha ambacho tunalipwa ni kidogo na hakitoshi kwa sababu
kuishi katika Mji wa Dodoma ni gharama kubwa.”
Ndassa alisema
kati ya Sh300,000 wanazolipwa wajumbe hao, posho ya kikao ni Sh220, 000 na
80,000 ya kujikimu na kwamba kiasi hicho hakitoshi.
“Mfano ni siku ya Jumamosi na
Jumapili. Katika siku hizo mbili wajumbe wote hawalipwi Sh220,000 za posho za
kikao na wakati huohuo wanatakiwa kuwalipa madereva wao, kununua mafuta ya
gari, chakula na malazi,” alisema.
Aidha, alisema
kitendo cha wajumbe kutakiwa kulipwa Sh220, 000 baada ya kusaini katika kitabu
cha mahudhurio mara mbili kwa siku ni sawa na udhalilishaji.
“Nilimweleza
mheshimiwa mwenyekiti kwamba wajumbe tupo 600 na kulingana na hali halisi wote
hatuwezi kuhudhuria kikao kila siku, zipo siku ambazo baadhi yetu wanakuwa na
shughuli nyingine na wapo watakaougua, sasa na hao wasilipwe Sh220,000 kweli?”
alihoji.
Alisema
Serikali inatakiwa kulitazama suala hilo kwa kina kwa maelezo kuwa linaweza
kuibua mvutano unaoweza kusababisha wajumbe hao kushindwa kuijadili Rasimu ya
Katiba kama inavyotarajiwa na wengi.
“Wajumbe wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba walikuwa wakilipwa Sh500,00 kwa siku, lakini
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanalipwa Sh220,000 tena mpaka wahudhurie
kikao. Hii siyo sawa kabisa,” alisema.
Alisema
madereva wa Tume hiyo ya Katiba walikuwa wakilipwa Sh220,000 kwa siku... “Posho
yangu ni sawa na aliyokuwa akilipwa dereva wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Sielewi kabisa
maana hata viwango vyetu vya posho ni tofauti na wajumbe wa Bunge la Katiba
kutoka Zanzibar, wao wameongezewa posho.”
Alisema jambo
hilo litaibua ubaguzi kwa sababu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na
kuongezewa posho lakini wajumbe 201 walioteuliwa na Rais hawana mahali pa
kulalamika ili kuongezewa posho.
Pamoja na
Ndassa kutotaka kuweka wazi, kumekuwa na madai kuwa wajumbe kutoka Zanzibar wameongezewa
Sh120,000 na Baraza la Wawakilishi, hivyo kuwafanya kupata Sh420,000 kwa siku.
Hata hivyo,
Katibu wa Baraza hilo, Yahya Khamis Hamad alikana madai hayo akisema hakuna
fedha za ziada walizolipwa.
Alisema malipo
waliyosaini wakiwa Dodoma yaliyotokana na kuhudhuria vikao vya Kamati za
Baraza, lakini si nyongeza ya posho.
Akizungumzia
suala hilo Nchambi alisema: “Sisi tumeshazoea maisha ya Dodoma na tunaishi
hivyohivyo tu licha ya kuwa fedha ni ndogo. Ila hawa wenzetu ambao ni wageni
hali zao ni mbaya.
“Wajumbe wapo
hapa kwa ajili ya kutengeneza moyo wa nchi yao na wakati tunakuja hapa Dodoma
tulielezwa wazi kuwa tusiende kuishi katika nyumba za wageni za vichochoroni.
Sasa kwa mantiki hiyo hiki kiwango cha fedha tunacholipwa kitatosha kweli?
“Hapa bungeni
wapo maprofesa walioacha kazi zao zinazowaingizia fedha nyingi na kuja kuandika
Katiba. Kitendo cha kuwalipa fedha kidogo
kinaweza kuwakatisha tamaa.”
Kificho
alihitimisha mjadala huo kwa kusema suala hilo la posho litawasilishwa
serikalini kuona namna ya kulifanyia kazi.
Baada ya
wabunge kutoka kwenye mjadala huo, Mjumbe, Kabwe Zitto alisema anasikitika
kwamba tangu siku ya kwanza, suala la posho linashika kasi... “Kiukweli inavunja moyo sana… Ni
dhahiri wajumbe lazima walipwe lakini malipo ya posho ndiyo kipaumbele kweli?”
Imeandikwa na
Mwinyi Sadallah, Raymond Kaminyoge Fidelis Butahe na Freddy Azzah.
No comments:
Post a Comment