JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA
HABARI
UAMUZI WA SERIKALI YA
KENYA KUZUIA MAGARI YA KITALII YALIYOSAJILIWA TANZANIA KUINGIA UWANJA WA NDEGE
WA KIMATAIFA WA JOMO KENYATTA KWA AJILI YA KUCHUKUA NA KUSHUSHA WATALII
Tarehe 22 Desemba,
2014, Serikali ya Jamhuri ya Kenya ilitoa amri ya kuzuia magari ya kitalii
yenye usajili wa Tanzania kwenda kuchukua na kushusha watalii wanaotumia uwanja
wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta wakiwa njiani kuja kutembelea vivutio
vya utalii katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Baada ya uamuzi
huu wa Serikali ya Kenya, Waziri wa Maliasii na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu
alifanya majadiliano na Waziri wa masuala ya utalii wa Serikali ya Kenya siku
ya tarehe 16, Januari, 2015 ili kutafuta ufumbuzi wa kadhia hii. Matokeo ya
mkutano wa Mawaziri hawa yalikuwa ni kusitishwa kwa muda katazo lililotolewa na
Serikali ya Kenya kwa makubaliano kuwa yafanyike mazungumzo baina ya pande hizi
mbili ndani ya kipindi cha wiki tatu kuanzia tarehe 16 Januari, 2015 ili
kurekebisha Mkataba wa Ushirikiano katika sekta ya utalii wa mwaka 1985 kati ya
nchi zetu mbili.
Kufuatia makubaliano hayo Wizara ya Maliasili
na Utalii iliiomba Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iandae kikao
hicho cha pamoja katika muda uliopangwa. Kwa kuzingatia historia na uzito wa
suala lenyewe, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki iliona umuhimu wa
kuhusisha Wizara zingine husika za Uchukuzi, Mambo ya Nje, Viwanda na Biashara,
Fedha, Ulinzi, Mambo ya Ndani, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira na Viongozi wa Sekta Binafsi ili kupata msimamo wa nchi wa pamoja
kabla ya mkutano na Kenya.
Hivyo, vikao vya wataalam vimefanyika Dar es
Salaam na Arusha hadi wiki ya kwanza ya mwezi huu wa pili kwa maandalizi ya
kikao cha mwisho cha Mawaziri upande wa Tanzania kabla ya kukutana na wenzetu
wa Kenya. Pamoja na kushauriana na Waziri mhusika wa Kenya (Masuala ya Afrika
Mashariki, Biashara na Utalii, Bi. Phyllis Kandie) kusogeza mbele tarehe ya
mkutano wa pamoja ili kuruhusu muda wa kutosha kwa majadiliano ya ndani na
wadau, Bi. Kandie alimwandikia Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki,
Dkt. Richard Sezibera na kumnakili Waziri Nyalandu, kurejesha amri yake ya
awali ambayo alisema inaendana na Sheria ya utalii na kanuni za uchukuzi za
Kenya.
Serikali ya Tanzania kimsingi imesikitishwa na
uamuzi huo wa Serikali ya Kenya kwani haujengi wala hauendani na dhamira njema
ya Mkataba wa Kuanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuenzi njia ya
mazungumzo, maelewano na maridhiano katika kufikia maamuzi. Suala la
kurekebisha mkataba ulioingiwa na nchi hizi mbili kwa hiari miaka 30 iliyopita,
si jepesi la kujadiliwa na Mawaziri wawili tu na kuwekeana ukomo wa muda katika
kulipitia. Serikali ya Tanzania itaendelea na mchakato iliouanzisha wa
kuhusisha wadau wote na kufikia uamuzi ambao itauwasilisha kwa Serikali ya
Kenya kupitia vikao rasmi vya Jumuiya.
Pamoja na kwamba amri hii ya Serikali ya Kenya
inaenda nje ya mkataba wa 1985 kwa kuvihusisha hata viwanja vya ndege kuwa
sehemu ya vivutio vya utalii, Serikali ya Tanzania itaheshimu na kuzingatia
amri hiyo ili kulinda undugu na urafiki uliopo kati ya nchi zetu huku
tukitafakari hatua za kuchukua ili kuondoa bughudha kubwa itakayotokea kwa
watalii na wasafiri wetu wanaopitia uwanja huo wa Jomo Kenyatta. Aidha Tanzania
itachukua hatua ya kuwafahamisha watalii na wageni wote wenye nia ya kutembelea
vivutio vya kitalii vya Tanzania kutumia viwanja vingine vya ndege ili kuepuka
kadhia na gharama zisizo za lazima.
Kwa upande wa Tanzania, viwanja vya ndege hasa
vile vya Kimataifa vitaendelea kuwa sehemu ya malango ya kuingilia na kutokea
kwenda kokote iwe ndani ya Jumuiya au nje ya Jumuiya na havitavichukuliwa kama
vivutio vya utalii. Tanzania haitazuia magari ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki au nchi nyingine yoyote kuingia katika viwanja vyake vya ndege
kuleta au kuchukua watalii wanaopitia katika viwanja hivyo na kwenda katika
nchi zao.
Mkataba wa mwaka 1985 kati ya Tanzania na
Kenya ulilenga kutoa mwongozo wa ushirikiano katika Sekta ya Utalii kati ya
nchi zetu mbili. Aidha, makubaliano hayo yalielekeza maeneo muafaka kwa ajili
ya kubadilishana watalii huku ikizingatiwa kuondoa bugudha kwa watalii. Maeneo
hayo ni pamoja na miji ya mipakani pamoja na miji rasmi iliyopendekezwa na
kukubalika na pande zote mbili ikiwemo Nairobi ambako kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Jomo Kenyatta kipo.
Mwisho, Tanzania itaendelea kuenzi undugu na
urafiki uliojengeka kwa zaidi ya miaka 50 tokea uhuru kati ya nchi zetu mbili
na suala dogo kama hili halitaweza kuteteresha uhusiano wetu mzuri.
WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
No comments:
Post a Comment