Sunday, February 18, 2007
JK in London: "Vyama Vingi Si Uadui"
Watanzania wengi walifika London, Uingereza kuonana na Rais Jakaya Kikwete. Courtsey: http://mjengwa.blogspot.com
Na Saidi Yakubu, London
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwepo kwa vyama vingi Tanzania haimainiishi uadui kwa wafuasi wa vyama husika. Rais aliyasema hayo katika mkutano wake na Watanzania waishio Uingereza hapo jana.
Akizungumza na watanzania hao takriban mia saba ambao walijaza ukumbi wa Galeon Suite katika hoteli ya Royal National jijini hapa, Rais Kikwete alisema haamini kwamba kuwepo kwa vyama vingi hususan visiwani Zanzibar maana yake ni uadui kwa wafuasi husika.
‘’Tangu nikiwa waziri huwa nakutana na wapinzani tena nawaalika tunakula na kuchanganyika pamoja, sidhani kama ni sawa katika mfumo wa kidemokrasia kutomuuzia jirani yako kibiriti kwa vile tu ni wa chama kingine’’ alisema.
Rais Kikwete alikuwa akijibu swali la mtanzania Ali Omar alietaka kujua muelekeo wa mazungumzo baina ya CCM na CUF kuhusu hali ya kisiasa visiwani Zanzibar baada ya uchaguzi mkuu.
Mtanzania huyo, alimuuliza Rais iwapo mazungumzo hayo [kufuatia kauli yake bungeni baada ya kuingia madarakani mwaka 2005] ya kujadili kile anachokiita mpasuko wa wapemba na waunguja yamechukua mwaka mmoja kuanza, vipi mambo yatakuwa katika utekelezaji wa makubaliano hayo.
Mkutano watanzania na Rais Kikwete safari hii ulionekana kuwaridhisha wengi hususan baada ya Ubalozi wa Tanzania kuamua kukodisha ukumbi mkubwa zaidi kufuatia manung’uniko ya watanzania wengi ambao hawakupata nafasi ya kuingia ukumbini kumsikiliza Rais wao katika mkutano wa awali mwezi uliopita.
Akijibu swali la mwandishi wa habari hizi ambae alimuuliza Rais JK iwapo ataweza kuwasaidia watanzania waishio nchini hapa hususan kutoka visiwani ambao waliomba hifadhi ya kisiasa wakidai kukimbia vurugu za kisiasa Zanzibar ambapo baada ya miaka kadhaa kupita, Serikali ya Uingereza ikaamua kuwapa haki ya kuishi nchini hapa nje ya taratibu za Uhamiaji baada ya awali kuwanyima hifadhi ya kisiasa, tatizo kubwa ni kuwa wamekuwa wakikwama kupata pasi zao za kusafiria za Tanzania kwa vile ubalozi na idara ya uhamiaji wanashindwa kujua hadhi yao ya ukaazi nchini hapa.
Akijibu swali hilo Rais JK alisema anapata shida kuelewa kiini hasa cha tatizo ni kipi kwani midhali watanzania hao kutoka visiwani bado wana pasi zao za zamani basi wana haki ya kupewa pasi mpya, ‘’Sioni tatizo hapa au labda sijapewa maelezo yote manake kama hawa ni watanzania na waliingia na pasi zao basi haihitaji tamko langu kwamba wapewe pasi au niingilie kati, wanachotakiwa ni kwenda ubalozini na hati zao za zamani wapatiwe pasi mpya’’ alisema Rais Kikwete.
Akijibu swali kuhusu vitambulisho vya Taifa kufuatia swali la mtanzania alietajitambulisha kwa jina moja, Kathryn alietaka kujua ni kwanini serikali inatumia dola milioni sabini (70) kuendesha zoezi la utoaji wa vitambulisho vya taifa wakati bado maeneo kadhaa hakuna maji, walimu wana mishahara midogo na bado serikali imeelemewa na mizigo kadhaa muhimu zaidi, Rais Kikwete alisema zoezi la vitambulisho vya taifa ni muhimu kwa kila nchi, ‘Kwanza niseme tumechelewa manake uamuzi ulitolewa mwaka 1964 na zoezi hili utekelezwaji wake umekuwa ukisogezwa mbele mwaka hadi mwaka kutokana na ukosefu wa fedha na kila tunavyoahirisha ndivyo gharama zinavyozidi kuongezeka, sasa hivi tumeamua kutenga fedha hizi na kuanza kutekeleza mradi huu kwa vile umuhimu wake umeongezeka zaidi, lakini pia sio sawa kusema eti tusitoe vitambulisho hivi kwa vile kuna walimu shule zipo duni au kwa sababu nyingine manake kwa kila tunachofanya basi kipo tutakachokosa, wachumi wanaita Opportunity Cost sasa wakati matatizo hayo bado yakiwapo lakini na vitambulisho vya taifa ni muhimu vile vile’’ alisema Rais Kikwete.
Msafara wa Rais Kikwete ambao pia unawaumuisha Waziri wa Mambo ya Nje, Benard Membe, Waziri wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Waziri wa Elimu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haroun Suleyman na wabunge, Bi Grace Kihwelu wa CHADEMA na Bwana Mwambalaswa wa CCM unatarajiwa kuondoka leo kuelekea nchi za Scandinavia, na baadae Makao makuu ya Jumuiya ya Ulaya nchini Ubelgiji. Rais na msafara waka wanatarajiwa kurejea nyumbani mapema mwezi Machi. Maoni: http://mjengwa.blogspot.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment