Ndg. Albin Tenga, alikuwa msimamizi mkuu wa mkutano, Jumatano, 28. Februari 2007
Ndg. Maftah Himid, katibu mwenezi akisoma risala. Jumatano, 28. Februari 2007.
Katibu mwenezi akimkabidhi risala Rais Kikwete, makamu mwenyekiti ndg. Hassan Ng´anzo akisubiri kumpa Rais, zawadi kutoka kwa Watanzania waishio Norway.
Risala ya Watanzania waishio Norway kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jumatano, 28. Februari 2007. Grand Hotel, Oslo.
Mheshimiwa Rais, Asalaam Aleykum na karibu Oslo!
Wahenga walinena ”milima haikutani lakini binadamu hukutana” hawakukosea. Tulikukaribisha mara ya mwisho ulipokuja Oslo ukiwa Waziri wa mambo ya nchi za nje, leo hii tunakukaribisha tena katika mazingira tofauti. Rais wetu aliyepata ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika 2005, tunakupongeza, hongera sana na karibu Oslo!
Tungependa kwanza kutoa historia fupi ya Chama Cha Watanzania Oslo. Chama kilianzishwa 1984 hapa Oslo kwa madhumuni ya kuwaunganisha Watanzania waishio Oslo na vitongoji vyake, kwa ajili ya mambo mbalimbali ya kijamii na ya kitaifa yanayotuhusu Watanzania. Chama Cha Watanzania kimekuwa kinajishughulisha na mambo yafuatayo;
Kuadhimisha:
* Sherehe za Uhuru na Jamhuri - Tisa Desemba
* Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar - tarehe 12 Januari
* Sherehe za siku ya Taifa (yaani Muungano) – tarehe 26 Aprili
* Kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere – tarehe 14 Oktoba.
Pamoja na shughuli hizi za kitaifa, Chama vilevile kinafanya shughuli za kuwashirikisha watoto, ndugu, jamaa na marafiki zetu wa Kinorwegiani ili kuendeleza mshikamano wa Watanzania huku ugenini. Kwa kifupi Mheshimiwa Rais, chama chetu kinashirikiana vyema na vyama vya watu kutoka mataifa mengine na vitengo mbalimbali vya serikali ya hapa.
Mheshimiwa Rais,
Ujio wako ni wakati muafaka wa kutoa dukuduku zetu. Tungependa kutumia nafasi hii kupata ufafanuzi na maelezo kuhusu masuala yafuatayo:
Mheshimiwa Rais,
Toka mwaka 1964 baada tu ya Muungano, serikali iliazimia kuwapa raia wote wa nchi vitambulisho vya uraia; lakini mpaka leo hii, azma hiyo haijatekelezwa. Mheshimiwa Rais, azma hii ya vitambulisho imefikia wapi? Tunadhani kuwa serikali inaona na inajua umuhimu wa raia wake kuwa na vitambulisho. Nyumbani wageni wengi wanaishi kiholela, na madhara yake yanajulikana hakuna haja ya kuyarudia. Suala la kuwapa wananchi vitambulisho vya uraia ni la muhimu na tunadhani imefikia wakati muafaka.
Mheshimiwa Rais,
Suala la kuwa na uraia wa nchi mbili tunadhani umeshalisikia . Je, endapo kama suala hili likikubaliwa kuna uwezekano wa Watanzania waliochukua uraia wa nchi zingine kwa sababu moja au nyingine, kurudishiwa uraia wa Tanzania kama wakiomba kufanya hivyo?
Mheshimiwa Rais,
Umoja na mshikamano wa Watanzania usingewezekana kama nchi isingekuwa na lugha ya Taifa ya kizalendo, yaani Kiswahili. Nchi yetu imebahatika sana kwenye suala hili la lugha ya asili kama lugha ya Taifa. Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema ”… kama Kiingereza ni lugha ya dunia, basi Kiswahili ni Kiingereza cha Afrika”. Ndugu zetu wengine barani Afrika wameuelewa msemo huu. Rais Mstaafu Joakim Chissano wa Msumbiji aliwahi kutumia Kiswahili kwenye hotuba yake moja kwenye mkutano wa Umoja wa Afrika. Huo ni mfano mmoja tu kuonyesha jinsi Kiswahili kinavyoheshimika duniani.
Lakini inasikitisha kuona jinsi Kiswahili hadi sasa hakijawekewa mkakati endelevu wa kukiwezesha kitumike kama lugha ya kufundishia kuanzia ngazi ya chekechea hadi Chuo Kikuu. Nafasi ya Kiswahili ya kukua inakuwa finyu kila kukicha kwa sababu hakitumiki ipasavyo. Lugha yoyote haiwezi kuendelea kama haitumiki kwenye elimu ya juu ya nchi. Kuna msemo siku hizi kuwa kwa sababu za utandawazi, basi lazima tujifunze Kiingereza. Msemo huo ni wa kweli, lakini si kizuizi kwa nchi kuwa na lugha yake ya Taifa kwa faida ya wananchi wake.
Hoja nyingine ya wanaokidhalilisha Kiswahili ni kuwa eti hakina misamiati ya kutosha kwa dunia ya leo ya utandawazi na teknolojia ya habari na mawasiliano. Mheshimiwa Rais, wenzetu hawa Wanorwejiani wanaheshimu sana lugha yao. Lugha yao nayo ina mapungufu makubwa tu. Kwa mfano, bado wanatumia baadhi ya misamiati ya lugha za kigeni, hususani Kiingereza na hasa kwenye fani za sayansi na teknolojia, lakini hawakwami au kushindwa kutumia lugha yao kwenye elimu toka chekechea hadi vyuo vikuu. Kila siku BAKITA yao inajitahidi kuunda visawe vipya na kwenda sambamba na wakati. Tunadhani huu ni mfano mzuri wa kuigwa. Hivi Mheshimiwa Rais, ni wangapi kati yetu hapa tukiota usiku tunaota kwa Kiingereza? Kama si kwa lugha za makabila basi ni kwa Kiswahili.
Mheshimiwa Rais,
Tunakupongeza kwa uamuzi wako wa busara kuamua kulipeleka suala la Shirikisho la Afrika Mashariki kwa wananchi waliamue wenyewe. Pamoja na hayo tunapendekeza wananchi waelimishwe kwa kina kuhusu suala zima la Shirikisho la Afrika Mashariki ili watoe maoni yenye uhakika kwa suala muhimu kama hili.
Mheshimiwa Rais,
Tunakupongeza kwa hatua ulizozichukua mara tu ulipoingia madarakani, kuamua kulishughulikia ipasavyo suala la mpasuko wa kisiasa visiwani, yaani mgongano baina ya CCM na CUF. Mazungumzo yanayoendelea kati ya viongozi wa juu wa vyama hivyo viwili tunayatakia mafanikio mema. Mheshimiwa Rais, mpaka sasa Watanzania wengi hatuelewi nini kinachoendelea kwenye mazungumzo hayo. Je, unaweza kutudokeza kidogo?
Mheshimiwa Rais,
Tunakupongeza kwa jitihada zako za kuendeleza ujenzi wa barabara kuunganisha mkoa mmoja na mwingine na hatimaye nchi nzima. Tunakumbuka kwamba juhudi hizi zilianzishwa wakati wa serikali ya awamu ya tatu. Tunakumbuka pia kauli ya kufurahisha ya Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwamba “kufikia mwaka 2007 watu wataendesha taxi kutoka Mtwara mpaka Mwanza”. Tunasikitika kwamba mpaka sasa ahadi hii haijakamilika na badala yake kuna malumbano makali baina ya Serikali na wakandarasi kiasi hata baadhi kufikia hatua ya kunyang’anywa kandarasi walizopewa. Tuna wasiwasi kuwa malumbano haya yatakwamisha zaidi jitihada hizi. Mheshimiwa Rais, tutashukuru kupata maoni yako kuhusu suala hili.
Sambamba na hilo, tunasikitika kwamba safari za treni ya abiria kwa reli ya kati sasa zinaanzia Dodoma. Wananchi wanaingia gharama ya kusafiri kwa basi toka Dar es salaam, Morogoro nk na wengi wao hulazimika kuingia gharama za malazi wakiwa Dodoma. Wote tunafahamu kwamba miundo mbinu ndio kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi. Je, suala hili unalipa uzito kwa kiasi gani ili kauli ya maisha bora kwa mtanzania iwe ya vitendo.
Mheshimiwa Rais,
RUSHWA! Rushwa imekithiri kwenye nchi yetu. Tunasikia kuna msemo siku hizi kuwa ”Rushwa ni zao la biashara”. Jamani hivi rushwa imekuwa ni zao la biashara? Hali hii inasikitisha sana! Mheshimiwa Rais, umewahi kunukuliwa na vyombo vya habari kuwa unayo majina toka TUKURU yaani PCB ya vigogo wa serikali na wafanya biashara wakubwa wanaojishuhulisha na rushwa. Kilio cha wananchi lini majina hayo yatajulikana na wahusika kufikishwa kwenye mkondo wa sheria?
Mheshimiwa Rais,
Umeshinda kwa vishindo, umekuja na “ari mpya, nguvu mpya na kasi mpya” na umeshawahi kusema kuwa ari, nguvu na kasi zako hazitakuwa nguvu ya soda. Tunakushukuru kwa kusema hivyo, na tunakuomba usipunguze ari, nguvu na kasi kwenye vita kubwa inayowakera Watanzania na wapenda haki duniani kote, RUSHWA!
Mheshimiwa Rais,
Watanzania wote tuna matumaini makubwa kwa kuchaguliwa kwako. Ni matumaini yetu kuwa utafuatilia kwa makini kero za Watanzania. Tunakuomba usikate tamaa. Ni mategemeo yetu kuwa uongozi wako wa awamu ya nne utaendelea kwa ARI MPYA, NGUVU MPYA NA KASI MPYA kama uliyoanza.
Kwa kumalizia, Mheshimiwa Rais, tunaomba tukukabidhi zawadi ya jumla kutoka kwa Wanachama wetu waishio hapa Norway ili utukumbuke japo ni ndogo; kwani wahenga walisema ”kutoa ni moyo, si utajiri”.
Asanteni sana!
Dr. Sendeu Titus M. Tenga
Mwenyekiti,
Chama Cha Watanzania, Oslo Norway.
http://watanzaniaoslo.blogspot.com
1 comment:
Watanzania wa Oslo. Hongereni kwa maandalizi na kufanikisha siku ya mkutano na Rais Kikwete.
Post a Comment