LEO tunasherehekea miaka 43 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Pamoja na kula na kunywa, maadhimisho hayo yanatoa fursa nyingine kuthibitisha kuwa itakuwa vigumu sana kwa watu wenye nia ya kuuvunja Muungano huo kufanikisha azma yao.
Tumetoka mbali, tumevuka milima na mabonde. Yapo mabonde yaliyokuwa na nzige na asali, lakini kuna sehemu tumepita katika mabonde yenye miiba na mbung’o. Tumeshavuka huko, tupo hapa tulipo na la muhimu sana ni kutazama kule tuendako.
Tutalazimika pia kutazama tutokako kwa nia ya kuangalia tulipojikwaa, kwamba tulifanikishaje kuondokana na kikwazo kilichotukwaza.
Wakati tunasherehekea miongo minne hii na ushehe, ni vema kujiuliza kama si Watanzania wenyewe, Muungano utaimarishwa na nani? Kwa hakika, kila mmoja anafahamu kuwa hakuna mwenye jukumu hilo zaidi ya Watanzania.
Lakini wakati tunasherehekea miaka 43 ya Muungano, ni vema tukajiuliza nafasi ambayo Watanzania (hawa wa kawaida) wamepewa katika kuusuka Muungano huo. Na tunapoliangalia suala hilo, ni vema kuanzia mwanzo wa Muungano.
Lakini ni vema kuweka wazi kuwa, kufanikisha kuunganisha Tanganyika na Zanzibar wakati ule, tena katika mazingira ambayo wananchi wa kawaida hawakushirikishwa kikamilifu, ulikuwa ni uthibitisho tosha kuwa watu wa nchi hizo mbili walikuwa na udugu wa karibu mno. Ingekuwa ni ndoto kuweza kuwaunganisha watu ambao mahusiano yao si ya karibu.
Ukaribu huo bado ungalipo, na ndio silaha kubwa ambayo inaweza kutumika kuimarisha Muungano. Hofu isiwekwe juu ya kauli zinazotolewa na kuziona kana kwamba zinatishia au zinaashiria kutaka kuuvunja Muungano.
Kwa miaka hii yote, imejidhihirisha kuwa hakuna mwenye nia ya kuuvunja Muungano. Kama angelikuwepo, tayari angekuwa ameshajitokeza, au yale anayoyakusudia yangekuwa yameshaonekana waziwazi. Hata kama mtu kama huyo atajitokeza leo hii, tunajivuna kuwa tuna kila silaha ya kumdhibiti. Iwapo vyombo vinavyohusika vitashindwa kufanya hivyo, wananchi wa kawaida watamdhibiti, kwa sababu wanafahamu umuhimu wa Muungano huo.
Pamoja na matatizo yake, Muungano umedumu kwa zaidi ya miongo minne, na hakuna dalili kwamba utavunjika. Hivyo, ni upuuzi kudai leo kuwa, kuujadili Muungano ni kuleta chokochoko zenye lengo la kutaka kuuua.
Au kudai kwamba lipo kundi la watu ambao wana nia ya kuua Muungano. Kama kundi hilo lingekuwepo, lilikuwa na nafasi ya kufanya hivyo na kufanikiwa kirahisi katika miaka ya mwanzo ya Muungano, ambako ulikuwa haujapata mizizi ya kutosha na si leo ambako upeo wa uelewa wa Watanzania umepanuka sana.
Wakati leo tunatafakari na kujadili kile kinachoitwa kero za Muungano, tunapaswa pia kuangalia ushiriki wa Watanzania wa kawaida katika kuimarisha Muungano. Hili ni muhimu kwa sababu ili Muungano uwe imara na wa maana zaidi, unapaswa kuwa wa watu, hawa wa kawaida. Muungano unapaswa kuwanufaisha watu hao la sivyo, hautaonekana kuwa na maana yoyote na hakika hautadumu.
Ndio, watu ndio kiini cha Muungano huu. Tusipowaangalia vizuri, hawa ndio wanaoweza kuuvunja Muungano kwa sababu ni wao. Tusiwaangalie wanasiasa wala wapambe wao, tuwaangalie Watanzania wa kawaida na kuona ni jinsi gani Muungano umefanikisha kuboresha maisha yao, kwani hilo ndilo wanalolihitaji.
Tuangalie jinsi Muungano ulivyomnufaisha mwananchi wa kawaida kwa nia ya kufanya marekebisho katika sehemu ambazo zinaonekana kuwa ushiriki wa mtu wa kawaida haujawa mzuri.
Ni hatari sana kuwa na Muungano ambao hauna mashiko miongoni mwa watu ambao umekusudiwa kuwaunganisha. Tutakuwa na Muunganoi legelege ambao utadumishwa kwa nguvu za viongozi na si matakwa ya wananchi.
Na tunapofanya zoezi hilo, tujitahidi kuhakikisha kuwa mwananchi huyo anahusishwa ipasavyo. Tusirudie makosa yaliyopita ya viongozi kukaa na kuamua wamfanyie nini mwananchi huyo. Kufanya hivyo kunaweza kuwa kulifanikiwa mwaka 1964 kutokana na sababu zilizokuwepo wakati huo.
Kwanza inawezekana kuwa hatukuwa na rasilimali za kutosha kuwauliza Watanzania kuhusu aina ya Muungano wanaoupendelea. Pia inawezekana kuwa, upeo na uelewa wa Watanzania wakati huo, usingewawezesha kufanya kile Wazungu wanachokiita ‘informed decision’.
Hali ni tofauti leo hii. Kama tunaweza kuvumilia matumizi ya ziada yanayofikia sh bilioni 900, sidhani kama tunaweza kuumia iwapo tutaamua kwa makusudi kutumia bilioni chache kuwauliza Watanzania nini wanakitaka katika Muungano wao.
Leo hii uelewa wa Watanzania ni mzuri sana, hivyo wapo katika nafasi nzuri ya kufanya ‘informed decision’ kuliko ambavyo ilikuwa mwaka 1964.
Tusiogope kwamba watatoa mawazo ambayo utekelezaji wake utageuza aina ya Muungano tulionao, ambao baadhi ya watawala wanadhani kuwa ni aina fulani ya msahafu. Tuwape nafasi Watanzania hawa waeleze aina ya Muungano wanaoutaka na iwapo matakwa yao yatatimizwa, tutaibuka na Muungano imara ambao watawala hawatakuwa na kazi kubwa kuutetea kwa wananchi kama ilivyo sasa.
Kwa hakika, maoni ya Watanzania ndiyo yatakayotuwezesha kuboresha Muungano. Iwapo watawala watayaogopa maoni yao, watakuwa wanawalazimisha kufuata vile ambavyo watawala hao wanataka. Sidhani kama tutakuwa tunajenga Muungano wenye nguvu na mashiko.
Zipo hoja mbalimbali zimetolewa kuhusu Muungano. Nyingi kati ya hoja hizo, zimekuwa zikigusia matatizo yaliyopo katika Muungano huo. Yapo matatizo yanayotokana na hulka binafsi za viongozi, lakini kubwa ambalo linapaswa kupewa kipaumbele katika harakati za ujenzi wa Muungano imara, ni muundo na mfumo wa Muungano.
Muundo na mfumo ndio unaotoa dira ya namna Muungano utakavyofaa kuwa chombo cha kuwasaidia wananchi ambao wameamua kuungana. Kukwepa kulizungumzia hili, au kuwatisha wale ambao wanaliibua suala hili, ni sawa na kufagia uchafu ndani na badala ya kuuzoa na kwenda kuutupa jalalani, unauficha chini ya kapeti!
Hakuna hatari wala dhambi kujadili iwapo unaotufaa ni Muungano wa serikali mbili kama tulionao, au tuwe na serikali tatu, au tuwe na serikali moja. Tena mjadala kuhusu suala hilo unapaswa kuwa mpana sana.
Kama ilivyodokezwa awali, upeo wa uelewa wa Watanzania hivi sasa utatuwezesha kupata mawazo murua ambayop iwapo yatafanyiwa kazi bila kuangalia nani katoa wazo, tutafanikiwa kujenga Muungano ambao utakuwa bora kuliko huu tulionao.
Si kwamba Muungano tulionao si bora, lakini matatizo yaliyojitokeza, ambayo wengine wameyabatiza jina la ‘Kero za Muungano’, yanaonyesha wazi kuwa bado Muungano wetu haujakaa katika mstari ulionyooka.
Tutakuwa tunafanya dhambi kubwa sana iwapo tutaendeleza hali iliyoanza kujitokeza ya makundi mbalimbali, wanasiasa wakiongoza, kuanza kuutumia Muungano kama kete ya kushinikiza hoja zao.
Pamoja na siasa, Muungano utakuwa na maana sana iwapo utawasaidia Watanzania kujiinua kiuchumi na kijamii. Maendeleo katika nyanja hizo yatasaidia kuimarisha siasa na demokrasia kama tunavyolenga.
Ni vema kuonya kuwa mjadala huo hautamaanisha kuwa tunaachana na mfumo wa Muungano wa serikali mbili uliopo. Mjadala utatusaidia, iwapo tutaamua kuendelea na serikali mbili, kuibua mambo ambayo yanaufanya mfumo huo uzae matatizo ambayo yapo sasa.
Mjadala ulenge katika kuibua matatizo yaliyopo na mbinu madhubuti ya kukabiliana na kuyatatua matatizo hayo. Kuendelea kung’ang’ania kuwa mfumo wa serikali mbili ndio muafaka, bila kuangalia matatizo yaliyopo yanasababishwa na nini na tutawezaje kuyatatua, ni kuendelea kukalia bomu ambalo utambi wake unaendelea kuungua taratibu.
Kuna uwezekano mkubwa kuwa sababu zilizowafanya waasisi wa Muungano kuona umuhimu wa kuweka serikali mbili, hazipo tena leo hii, kwamba umuhimu wa serikali mbili katika Muungano umepitwa na wakati. Kuna dhambi gani kulijadili hili na kuliweka katika muktadha unaofaa?
Kama ilivyopatwa kuelezwa, asilimia kubwa ya Watanzania walio hai leo, wamezaliwa baada ya Muungano. Wamezaliwa wakiikuta Tanzania na si Tanganyika na Zanzibar kama ilivyokuwa kabla ya Muungano.
Lakini wameenda shule na huko wamefundishwa kuwa kabla ya kuwa Tanzania, kulikuwa na nchi mbili na viongozi wake wakakubaliana kuziunganisha ili kupata nchi moja. Kulikuwa na misingi ya makubaliano hayo na pia misingi ya Muungano huo. Wengi wanajua tu kwamba Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Karume walikubaliana kuunganisha nchi zao, lakini wachache sana wanajua misingi hasa ya makubaliano baina na Nyerere na Karume.
Watu wachache pia wanafahamu misingi ya Muungano na ndio maana leo hii, upotoshaji umekuwa mwingi kuliko ukweli halisi kuhusu Muungano.
Mjadala uliopanuliwa kuhusu Muungano, utasaidia kutoa fursa kwa ukweli kuhusu Muungano kuhubiriwa na kueleweka miongoni mwa Watanzania wengi ambao Muungano wamekuwa wanausoma tu kwenye vitabu na kuusikia katika masimulizi ya watu wachache ambao waliushuhudia.
Katika moja ya hotuba zake maarufu, Mwalimu Nyerere aliwahi kubainisha kuhusu hatari ya Muungano kuvunjika kutokana na uchoyo tu wa baadhi ya viongozi. Hali ya mambo inaonyesha kuwa, kauli ya Nyerere kuwa Wazanzibari wanaweza kujitenga tu kwa kuvutwa na Uzanzibari wao, bado haijafanyiwa kazi ipasavyo.
Lakini hali ya mambo inatulazimisha twende mbali zaidi ya hapo. Katika hotuba hiyo, Nyerere alisema kuwa watakapofanikiwa kujitenga kutokana na msukumo wa Uzanzibari wao, watakuja kubaini kuwa kumbe wao si wamoja kama walivyodhani na kwamba kilichokuwa kinawafanya wajione wamoja ni Muungano.
Tetesi za mipango ya kuundwa kwa Jamhuri ya Watu wa Pemba, inaweza kuwa ndio mwanzo wa utimilifu wa unabii wa Mwalimu Nyerere. Tunafanya nini kukabili hilo? Kuendelea kukaa na kusubiri matatizo yajisuluhishe yenyewe, au kutanguliza siasa wakati tunatafuta mbinu za kuyatatua, ni kujichimbia kaburi polepole.
Tunapouangalia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa mwaka 1964, ni wakati muafaka kuangalia jinsi nchi inavyotishiwa na mmomonyoko kutokana na tofauti za kikabila, kidini na kadhalika. Hata kama tutaendelea kukataa, hayo yapo. Watanzania wa leo si wamoja kama walivyokuwa miaka michache iliyopita.
Ushahidi mojawapo ni kupanuka kwa pengo kati ya matajiri na masikini. Huu ni ufa ambao Mwalimu Nyerere aliwahi kuugusia pia, lakini tunajifanya vipofu na kushindwa kuuona kuwa ni moja ya matatizo yanayoukabili Muungano wetu.
Huu ushujaa wa kuyafumbia macho matatizo haya, ambayo yapo bayana, utakuja kutufikisha pabaya.
Makala ya Peter Nyanje wa gazeti la Tanzania Daima.
1 comment:
You have done really very good site. Great work, Thank you!
Post a Comment