Monday, August 27, 2007

Ray C ataka sheria ziimarishwe kuwalinda wasanii


SERIKALI imeombwa kutunga sheria zitakazolinda kazi za wasanii nchini, ili kuwanufaisha wahusika kimapato, badala ya kuendelea na hali iliyopo hivi sasa ya kuwanufaisha walanguzi wa kazi za wasanii.

Wito huo umetolewa na msanii maarufu wa kike, wa muziki wa kizazi kipya, ‘Bongo fleva’, Rehema Chalamila ‘Ray C’ katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mwenge, mjini hapa.

Ray C alisema pamoja na COSOTA kuwa na jukumu la kuwasaidia wasanii, lakini hata hivyo bado kazi za wasanii wengi zinaendelea kuibiwa na watu mbalimbali.

Msanii huyo alisisitiza kuwa cha kushangaza ni kwamba unapokwenda Nairobi, Kenya, Bujumbura, Burundi na miji mingineyo, unaweza kukuta kazi za msanii zimefika huko, lakini aliyezifikisha hajulikani.

Ray C alisema endapo ingekuwapo sheria inayowalinda wasanii hao ingewasaidia, kwa madai kwamba kwa sasa wasanii nchini hawawezi kujilinda au hata kujitetea kutokana na rushwa kuwa imekithiri kwenye vyombo vya sheria.

Kutokana na hali hiyo, msanii huyo aliweka bayana kwamba wamekuwa hawapati faida kutokana na kazi zao zaidi ya kutegemea shoo wanazofanya, hali inayosababisha wasanii wengi wenye uwezo mdogo kushindwa kuendelea.
na Jumbe Ismailly

No comments: