Friday, August 31, 2007

Uganda hatimaye yakikubali Kiswahili kuwa lugha ya taifa


Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Uganda imepitisha Kiswahili kuwa lugha ya taifa ambapo kuanzia sasa itafundishwa kwa lazima kuanzia shule za msingi na sekondari.

Kiingereza ambayo ndiyo ilikuwa rasmi ya nchi hiyo, sasa imefanywa kuwa lugha ya pili na itakuwa ikitumika maofisini kwa sababu maalum.

Uganda imefikia hatua hiyo baada ya Kiswahili kutumika kama lugha kuu ya mawasiliano katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na maeneo ya kusini ya nchi ya Sudani ambazo ndiyo wadau wakubwa wa maendeleo ya nchi hiyo, wakati Tanzania ni lugha ya taifa.

Kutumika kwa Kiswahili katika nchi hiyo kutaboresha mahusiano baina ya nchi hiyo na nyingine za Afrika Mashariki na Kati zinzotumia lugha hiyo na kuchochea maendeleo ya uchumi hasa katika kipindi hiki cha kuanzishwa kwa Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pamoja na uamuzi huo Uganda inahitaji kuweka mikakati kuikuza lugha hiyo kwa kuongeza idadi ya walimu watakaoifundisha shuleni kwani idadi iliyopo haikidhi mahitaji.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchi hiyo ambayo kwa miaka kadhaa imekuwa ikitumia Kiingereza katika mawasiliano, inahitaji zaidi ya miaka 100 kuwaandaa wataalam wa Kiswahili wa kufundisha kwenye shule 13,000 za msingi katika nchi hiyo.

Mikakati mingine inayofanywa na nchi hiyo kupata watalaam wa lugha hiyo wa kutosha, ni kulifanya somo la Kiswahili kuwa la lazima katika shule za msingi na sekondari na kuliingiza katika mafunzo ya elimu ya watu wazima.

No comments: