Mgaya Kingoba, Dodoma, HabariLeo; Alhamisi, August 16, 2007 @00:02
WABUNGE jana walianza kujadili rasimu ya Kanuni mpya za Bunge, ambazo kama zikipitishwa itakuwa marufuku kwao kuchanganya Kiingereza na Kiswahili wakati wakichangia bungeni na hawataruhusiwa kutumia muda mwingi kupongezana na kupeana pole.
Rasimu hiyo inatokana na kazi iliyofanywa na Kamati Maalumu iliyoundwa na Spika Samuel Sitta ikiongozwa na Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai (CCM) kupitia kanuni na kuzirekebisha kwa nia ya kuleta ufanisi.
Wabunge walianza kujadili rasimu hiyo jana kwa faragha baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Kuhusu lugha, rasimu ya kanuni hizo ambayo HabariLeo imeipata inapendekeza kuwa: "Kwa kadri itakavyowezekana, Mbunge hataruhusiwa kuchanganya lugha zote mbili (Kiswahili na Kiingereza) wakati anazungumza bungeni ila tu anaponukuu".
Katika kudhibiti utoaji 'holela' wa pongezi na pole, rasimu hiyo inapendekeza kudhibiti hali hiyo.
Rasimu inapendekeza kuwa endapo litatokea jambo lolote ambalo mhusika wake au muathirika wa jambo hilo anastahili kupewa pongezi au pole na wabunge, basi Spika atatoa pongezi au pole kwa mhusika au muathirika wa jambo hilo kwa niaba ya wabunge wote.
"Baada ya Spika kutoa pongezi au pole kwa mhusika au muathirika wa jambo lolote kwa ajili ya kuokoa muda wa majadiliano, Mbunge ye yote hataruhusiwa kutoa pongezi au pole kwa mhusika au muathirika wa jambo hilo wakati wowote wa majadiliano bungeni," inaeleza rasimu.
Baadhi ya mabadiliko yaliyokuwa yakijadiliwa na wabunge ni Spika kuapishwa na Rais, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Serikali za Mitaa kutoka Upinzani, Waziri Mkuu kuhojiwa na Bunge kila Alhamisi na kuwapo kwa Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria.
Pia kanuni hizo mpya zinapendekeza kupigwa Wimbo wa Taifa kila mkutano wa Bunge unapomaliza vikao vyake.
Pia kanuni hizo mpya zinapendekeza kupigwa Wimbo wa Taifa kila mkutano wa Bunge unapomaliza vikao vyake.
Katika suala la Kamati za Bunge, kunapendekezwa shughuli za kawaida za Kamati kuendeshwa kwa uwazi tofauti na sasa ambako vikao vingi vya Kamati za Bunge huwa ni vya faragha.
"Shughuli za kawaida za Kamati zitaendeshwa kwa uwazi ambako Kamati itaalika wadau kupata maoni na ushauri wao kwa ajili ya kuboresha muswada au jambo ambalo litakuwa linashughulikiwa na Kamati hiyo," inaeleza rasimu hiyo.
Pia inaeleza kuwa wenyeviti wa Kamati za Hesabu za Serikali na Serikali za Mitaa watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Kamati hiyo ambao wanatoka katika Kambi ya Upinzani.
Kwa sasa, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge toleo la 204, Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), ndiye atoke upinzani. John Cheyo wa Bariadi Mashariki (UDP), ndiye Mwenyekiti wa sasa wa kamati hiyo.
Rasimu inaeleza wazi kuwa Mbunge yeyote ambaye ni Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya hatachaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali au Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa.
Inapendekeza kuwapo na Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria ambaye atakuwa Msaidizi Mkuu wa Katibu wa Bunge kwa masuala yote yanayohusu sheria.
Kazi zake zinatajwa kuwa ni kuchunguza na kuhakikisha kuwa sheria zote zinazotungwa hazipingani na Katiba ya Nchi, kuchambua miswada ya kupitishwa bungeni na kuwasaidia wabunge waielewe vizuri ili kuboresha michango yao bungeni na kuchambua Kanuni za Bunge na kutoa ushauri kwa Bunge kuhusu marekebisho yoyote kuzifanya Kanuni ziendane na wakati.
Nyingine ni kupitia mikataba yote iliyosainiwa na Serikali ili kulishauri Bunge na Kamati zake kuiridhia mikataba hiyo au la, kusaidia Kamati au wabunge kutayarisha miswada ya kamati au binafsi na kila atakapohitajika kufanya hivyo.
Kuliwakilisha Bunge mahakamani endapo Bunge litashtakiwa au kushtaki, kuhakikisha miswada yote iliyopitishwa inachapishwa kama ilivyopitishwa na Bunge na kushughulikia masuala yote kisheria yatakayopelekwa kwake na uongozi wa Bunge.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo, Mshauri Mkuu wa Bunge wa Mambo ya Sheria atateuliwa na Tume ya Huduma za Bunge kutoka miongoni mwa wanasheria waandamizi.
Kuhusu Wimbo wa Taifa, rasimu hiyo inaeleza: "Mara tu baada ya Bunge kupitisha hoja ya kuahirisha Mkutano wa Bunge, wimbo wa taifa utapigwa kufuatana na utaratibu uliowekwa na Bunge.
Endapo Mbunge atafariki dunia wakati Bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya maombolezo, jambo ambalo halikuwapo katika kanuni.
Kwa mujibu wa maelezo ya Naibu Spika bungeni jana, michango ya wabunge katika semina ya jana na leo ndiyo itatumika kuboresha rasimu hiyo kabla ya kukubaliwa kuwa Kanuni za Bunge.
No comments:
Post a Comment