Monday, September 17, 2007

Kikwete umewagundua wanaokumaliza kisiasa-(Gumzo)

Picha kutoka: jakayakiwete.com

Na Ramadhan Semtawa

SIKU zote katika maisha, huwa naamini katika ukweli ambao ni dira muhimu ya maisha yangu. Inawezekana hatua yangu ya kuwa mkweli ikawa haiwapendezi wengi wanaonizunguuka au hata baadhi ya watawala, lakini Mungu muumba wa mbingu na ardhi, anapenda ukweli.

Kwa kujua kwamba, napata nguvu kubwa na ulinzi kutoka kwa mwenyezi Mungu, ndiyo maana sipendi kuita rangi nyeusi kuwa nyeupe, au bluu kuwa zambarau, kwa maana nyingine rangi nyeupe nitaita nyeupe tu na si nyeusi, kwani huo ndiyo ukweli! Katika kuzingatia hilo, katika safu moja ndani ya gazeti hili la mwezi Julai, niliandika haja ya Rais Jakaya Kikwete, kucheza karata mpya kutokana na umaarufu wake kuonekana unaporomoka kwa kasi.

Ndani ya hoja yangu ya msingi, nililalamikia sana baadhi ya watendaji wanaomzunguuka Rais Kikwete na hata washauri, kwani wanashindwa kumweleza ukweli mkuu huyu wa dola, kuhusu mwenekano halisi wa taswira yake kwa wananchi.

Kwa kuwa nampenda Rais wangu, nikamweleza ukweli kwamba Rais umaarufu wako ndiyo huo unapotea, cheza karata nyingine, sasa sijui ndiyo hii kageukia michezo, mimi sijui. Lakini kama amefanya hivyo, nampongeza ni hatua moja mbele ya kurudisha umaarufu, lakini hii ya michezo si hoja yangu ya msingi.

Hoja ya msingi, ni kuangalia hatua ya Rais kutaka watendaji wanaompangia ziara zake za Mikoani, wasimpeleke katika barabara nzuri au maeneo yenye mafanikio tu bali maeneo yenye matatizo.

Nilivyomuona na kumsikia Rais, akitoa kauli hiyo ambayo ni nzito na yenye mantiki pana, katika luninga wiki iliyopita wakati anafanya majumuisho ya ziara yake ya mkoa wa Dodoma, nilikaa vizuri kuona nini anasema mkuu huyu wa dola.

Rais Kikwete, anasema kuna watendaji hawampeleki katika maeneo yenye matatizo ikiwemo barabara kwa visingizio lukuki, wengine wakisema usalama ni mdogo na sababu nyingine nyepesi mithili ya mdudu chungu, lakini yeye akasisitiza anataka apelekwe huko.

Lakini kikubwa, ambacho kimenisukuma kuileta hoja hii hapa ni kufurahishwa na hatua hii ya Rais kubaini kwamba, kumbe kuna baadhi ya watendaji wake hawamsaidii kumjengea taswira nzuri kwa wananchi bali wana mmaliza.

Hawa ni wale ambao rangi nyeupe wanaiita nyeusi, na hata Rais akilalamikiwa wao wanamwambia hapa unapendwa kweli wala usiwe na wasi wasi mheshimiwa. Hii ni dhambi ya unafiki, dhambi inayowafanya watendaji wa namna hii wamjengee chuki Rais kwa wananchi ambao wamemchagua kwa matumiani makubwa ya kuleta mapinduzi katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Unafiki huu unatokana na nidhamu ya woga, watu wanafikiri Rais ni kama Mungu, wakisahau huyu amechaguliwa kuwatumikia wananchi. Ni hawa wanaompangia Rais ziara katika barabara za lami tu, wakisahau Kikwete ni mkuu wa dola ya Tanzania na wala hatoki Marekani, hivyo anapaswa kujua matatizo ya nchi na wananchi wake.

Rais huyu hata kama angetoka katika familia ya kitajiri, bado angepaswa kufikishwa kule ambako watu wanakula ugali wa mhogo na mlenda au ugali na kachumbari!
Sasa hatua ya kutaka kumpeleka Rais Kikwete katika barabara za lami ni unafiki mkubwa na wala si kumsaidia, ndiyo maana nampongeza kwa kubaini hili.

Lakini Rais anapaswa kufahamu, hatua hii ya kupinga unafiki wa viongozi hawa ni ya kwanza, ya pili angepaswa pia kutumia e mamlaka yake kuwaondoa madarakani, kwa maana wanaweza hata wakawa wamemdanganya Rais katika taarifa zao za mipango ya maendeleo. Kwa maana kama wanaweza kuficha matatizo ya wananchi ili wapendezeshe, watashindwaje kumpa takwimu na mipango ya maendeleo ya uongo?

Hii ndiyo aina ya viongozi tuliyonayo, viongozi wanaokosa utashi binafsi, viongozi wanaongozwa na unafiki na nidhamu ya woga, hawawezi kuipaisha ndege ya uchumi wala kufanikisha azma ya kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Falsafa ya maisha bora haiwezi kutimia kwa kuwa na viongozi wanafiki, nchi hii ni masikini kwani nani hajui, hivi kuna haja ya kumficha Rais kweli kuhusu matatizo yetu?

Rais hakuomba kura mijini kwenye lami, huyu alifika hadi vijijini ambako anapaswa kufika kuona ile falsafa yake ya maisha bora imeanza kuwafikia hawa wanaokula ugali wa mhogo na mlenda? Nampongeza William Lukuvi, mkuu wa mkoa wa Dodoma kwa kuamua kumpeleka Rais hadi katika maeneo magumu, hawa ndiyo aina ya watendaji tunaowataka katika nchi.
Hatutaki viongozi ambao wanaonyesha udhaifu na kutojua majukumu yao, hawa Rais hawakufai wala hawalifai taifa, si wenzako hata kama walikuficha matatizo kwa misingi ya kufikiri wanakupenda.

Binafsi, naomba niseme kwa mujibu wa sheria, nitamweleza Rais na serikali kwa ujumla, ukweli kupitia kalamu kwa yale ambayo nasikia yanazungumzwa kutofurahisha wananchi au ninayobaini kama udhaifu. Kwa maana nitakuwa simtendei haki Rais na serikali yake, kama nitaamua kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa na kumfanya yeye ni Masiha wakati kuna udhaifu au mabaya yanatendeka katika serikali, hii ni dhambi ya unafiki!

Dhambi hii haitaishia kumtafuna Rais Kikwete na serikali yake tu, lakini unafiki huu kesho utanitafuna mimi, na vizazi vya sasa na vijavyo ndani ya taifa hili. Nitakuwa sitendei haki nafsi yangu wala kuijenga nchi yangu , nitakuwa nimefanya usaliti mkubwa, hivyo Rais anapaswa kuelezwa ukweli kuhusu matatizo ya nchi hii.

Ndiyo maana nakerwa na kuchukizwa kuona viongozi hawa wanaoficha matatizo ya wananchi kwa Rais, ndiyo hawa humwambia kwamba wananchi hapa wanakupenda sana mheshimiwa wakati wananchi wana mlalamikia. Huu ni wendawazimu, lakini ninachopenda kumshauri Rais ni kwamba, yeye ndiye ameomba kura kwa wananchi kuwa mkuu wa dola hii ya jamhuri ya muungano, kesho akirudi tena ataulizwa yeye na si wakuu wa mikoa au mawaziri.

Kwa mantiki hiyo, Rais anapaswa kuwa makini na watendaji hawa wabovu wasio na sifa za kuwa viongozi, kwa maana watakuja kumfanya apate maswali magumu katika uchaguzi wa 2010.
Napata wasi wasi mkubwa kuona kama Rais atashindwa kutimiza falsafa hii ya maisha bora, atakuja na falsafa gani 2010 ili aweze kuteka tena akili za Watanzania?

Kwa kifupi ni kwamba, miaka hii iliyobaki kabla ya 2010 ni ya Rais Kikwete kucheza karata zake kwa umakini mkubwa, vinginevyo atapaswa kufanya kampeni ngumu katika uchaguzi ujao.
Hapa niwe wazi, Rais Kikwete kama binadamu ana udhaifu wake, lakini kikubwa kinachomuangusha ni wasaidizi wake katika ngazi mbalimbali.

Rais anaonekana kuwa na utashi binafsi wa dhati wa kuleta maendeleo katika nchi, lakini kuna wasaidizi ambao ni wabovu aliwapa nafasi hizi kimakosa ingawa ana mamlaka ya kufaanya hivyo, ndiyo maana wanamsifia tu. Hivyo, Rais umewagundua hawa wanaokufanya wewe ni 'Masiha', naomba upige hatua ya pili mbele wafukuze, hawakusaidii bali wana kuharibia kwa wananchi na kukumaliza kisiasa.

Ramadhan Semtawa: semtawa@yahoo.co.uk,
http://semtawa.blogspot.com, 0732-107 188

No comments: