Mchezo unaanza saa 2 kamili kwa saa za Afrika Mashariki. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mh. Amani Abeid Karume.
Rais Jakaya Kikwete, ambaye asubuhi hii ameelekea Arusha kwenye kikao cha viongozi wa Maziwa Makuu, huenda akajiunga na Watanzania wengine kuishangilia Taifa Stars endapo kama atawahi.
Jana Rais Kikwete, - ambaye amewezesha kuufufua uzalendo uliowashinda Watanzania karibu wote katika medani ya michezo, hususan kandanda, kwa kuendelea kuwa 'kichwa cha mwendawazimu' - jana alitembelea kambi ya Taifa Stars hoteli ye Golden Tulip moja kwa moja akitokea wilayani Kondoa, Dodoma.
Kutokana na uzalendo uliotukuka hivi karibuni, kuna uwezekano wa watu kujisahau na kufikiri kwamba ili mradi tutaifunga Msumbiji, basi Ghana tutakwenda. Ukweli wa mambo na uhalisi wa mchezo wa soka unaweka mashakani matumaini haya.
Ila ukweli ni kwamba kuna jumla ya makundi 12 ambapo kila moja linatoa timu moja na zinaungana na mwenyeji Ghana, jumla inakuwa 13.
Makundi yenye washindi wa uhakika:
Kundi 1: Cote d’Ivoire imeshamaliza kazi kwani ni timu moja inatakiwa kwenda kwa kuwa ziko tatu. Gabon na Malagasi ziko nje zinasubiri mwaka 2010 vinginevyo Gabon iifunge Cote D’Ivoire 22-0, hakuna kitu kama hiki.
Kundi 2: Misri itakwenda kutokana na hali ilivyo kwani Burundi na Botswana haziko katika mkao mzuri wa kuipita ama kuzidi pointi 10 na kuwahi nafasi mbili za kapuni. Mauritania ni kibonde wao. Hakuna mshindi wa pili kwenda Ghana.
Kundi 4: Natamani Tanzania ingekuwa humu kwani kuna timu mbili kali na mbili dhaifu kufa. Tunisia itakwaa nafasi ya kwanza na Sudan ya pili. Shelisheli na Morisi nje.
Kundi 5: Kameruni ilishamaliza kibarua chake na waliobaki hawawezi kufikisha pointi 11 ambazo ndizo mpaka wa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha nafasi za kudoea.
Kundi 10: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakuwa mwenyeji wa Libya na tayari inaongoza kwa kuwa na pointi 11 na walitoka 1-1 mjini Tripoli. Kwa kuwa Libya, Namibia na Ethiopia hawawezi kufikisha pointi 11, ni heri kuipa bashasha Kongo kwamba itatoka hata sare tu na kwenda Ghana. Hakuna nafasi ya udowezi hapa.
Kundi 12: Moroko wameshamaliza mambo kwa kuwa kundi hili lina timu tatu tu, hivyo ni mshindi mmoja tu anayeenda. Malawi na Zimbabwe ziko taabani bin hoi.
Makundi yenye kimunyemunye cha safari ya Ghana:
Kundi 3: Hili kundi Nigeria itakuwa mshindi wa kwanza kwa sababu imeipita Uganda ambayo ni ya pili kwa pointi 5. Kazi iko kwa Uganda ambayo ina uwezo wa kufikisha pointi 11 na kama si kulazimishwa sare na Lesotho ingeshamaliza matatizo saa hizi.
Kundi 6: Ili kurahisisha mambo ni bora kukubali kwamba Angola itatoka salama kwani Kenya na Swaziland hazina pointi za kutosha na Eritrea ilishakubali magoli matatu zaidi ya iliyofunga, hailekei kuwa itaifunga Swaziland kapu kubwa kilaini. Angola hata ikifungwa Nairobi haina tatizo. Ingawa Eritrea inaweza kufikisha pointi 11 lakini suala la magoli litakuwa kizingiti.
Kundi 7: Senegal inaongoza kwa tofauti ya magoli dhidi ya Tanzania huku zote zikiwa na pointi 8, hivyo zote kuwa na nafasi ya kwenda Ghana. Shida moja ni kwamba Senegal inacheza nyumbani na timu isiyo na nafasi yoyote na ikishinda itakuwa mshindi wa kwanza labda tu ushindi uwe wa 1-0 na Tanzania iifunge Msumbiji 9-0, hapo mambo yatakuwa poa. Je, hii inawezekana....? Jibu unalo.
Kundi 8: Kundi lenye upinzani kama wa lile la kwetu kwani Algeria inayokwenda Gambia kucheza ina pointi 8 na Guinea inayoikaribisha timu nyonge ya Cape Verde nayo pointi 8. Kila yenye pointi 8 ikishinda itabidi kusubiri hesabu ya magoli kutoka makundi mengine ingawa Guinea ina nafasi nzuri zaidi.
Kundi 9: Kundi lenye timu zenye nafasi za kusonga mbele. Mali na Togo zina pointi 9 kila moja lakini Mali ina magoli 8 na imefungwa 1 wakati Togo ina 7 na imechapwa 7. Zinacheza mechi ya mwisho huko Togo. Atakayefungwa ametoka moja kwa moja. Zikitoka sare yoyote, basi Togo ni nje. Tatizo ni kwamba kuna Benin yenye pointi 8, hivyo kuwa kwenye nafasi ya kupata 11, inacheza ugenini na Sierra Leone wiki moja baadaye. Nyumbani ilishinda 2-0 na ikishinda mara hii, itabaki hesabu ya magoli tu. Kimsingi kundi hili lina uwezo mkubwa wa kutoa timu mbili.
Kundi 11: Afrika Kusini yenye pointi 11 itaikaribisha Zambia yenye pointi 8. Zilipocheza Lusaka Zambia ililala kwa 1-0. Kwa kuwa timu yoyote yenye pointi 11 inaweza kwenda Ghana kutegemeana na magoli ya kufunga na kufungwa, Afrika Kusini haitapenda kuingia kwenye wasiwasi kwa kukubali kufungwa na Zambia. Hata hivyo ina magoli 9 dhidi 1 ililofungwa, iko salama. Zambia ikishinda itaingia kwenye kusubiri hadithi ya magoli. Hapa pagumu.
UTABIRI WA NANI ANAKWENDA GHANA?
Mwenyeji: Ghana (hii ya uhakika)
Kundi 1: Cote d’Ivoire
Kundi 2: Misri
Kundi 3: Nigeria
Kundi 4: Tunisia
Kundi 5: Kameruni
Kundi 6: Angola
Kundi 7: Senegal
Kundi 8: Guinea
Kundi 9: Mali
Kundi 10: Kongo ya Kabila
Kundi 11: Afrika Kusini
Kundi 12 Moroko.
Mshindi wa Pili Bora mwenye uhakika:
Sudan: Kundi la 4.
Nafasi Mbili Zilizobaki:
Eritrea: Kundi la 6 - itaifunga Swaziland kwao angalau 4-0 au zaidi na dua zake zisikilizwe dhidi ya timu nyingine kwenye kibano hiki.
Tanzania: Kundi la 7 – iwapo itaifunga Msumbiji na kuombea wengine wote wenye nafasi ya kufikisha pointi 11 wafungwe ama watoke sare.
Algeria: Kundi la 8 – iwapo itashinda walau 1-0 na kuombea mabaya kwa wenzake wote.
Benin: Kundi la 9 – iwapo itashinda walau 1-0. Ina magoli 8 na imefungwa 4, iko safi labda tu kama ushindi wa timu nyingine utakuwa wa magoli kibao.
Zambia: Kundi la 11 – iwapo itaifunga Afrika Kusini walau 1-0 tu na kuombea wenzake wafunge magoli kiduchu.
NAFASI YA TANZANIA NIAJE?
Katika kundi hili wanaopigania nafasi za pili, Eritrea na Tanzania ndizo zina rekodi mbaya zaidi kwa zimefungwa magoli mengi kuliko zilizofunga (Eritrea inazidiwa kwa 3 na Tanzania kwa 2). Zambia na Benin zina magoli 4 zaidi ya yake ya kufungwa. Uganda ina faida ya magoli 3 na Algeria 1 tu. Ili Tanzania iende Ghana inabidi Uganda, Eritrea, Algeria, Benin na Zambia zifungwe ama zitoke sare, hapo ndipo kaushindi hata ka goli 1-0 katatupeleka Ghana. Vinginevyo basi mmoja wao tu afanikiwe na wengine wapoteze nafasi. Lakini nafasi ya uhakika zaidi ni pale Senegal itakapofungwa na sisi kushinda au Senegal ishinde 1-0 na sisi tuichape Msumbiji 9-0.
Kutoka kwa: http://issamichuzi.blogspot.com/
No comments:
Post a Comment