Monday, September 17, 2007

Mauaji ya Wakenya 14 yagubikwa na utata


MAUAJI ya watu 14 wanaodaiwa kuwa ni majambazi raia wa Kenya, waliouawa na polisi mkoani Kilimanjaro kwa kile kinachodaiwa ni mapambano ya kurushiana risasi, yamegubikwa na utata na usiri wa aina yake.

Utata huo unatokana na kuwepo na usiri mkubwa wa uhalisia wa tukio lenyewe na taarifa zilizotolewa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro.

Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima tangu kutokea kwa tukio hilo, umebaini kuwa lilipangwa na kilichofanyika eneo la tukio huko Weruweru Maili sita, ni sawa na mchezo wa kuigiza.

Inadaiwa mipango yote ya kutekeleza mauaji hayo iliendeshwa na makachero wa polisi wa Tanzania waliojipenyeza nchini Kenya kama washirika wa matukio ya uhalifu na kufanikiwa kuteka mawazo ya watu hao.

Baada ya kufanikiwa kwa hilo, ‘majambazi’ hao waliweza kupata ramani ya benki ya Exim tawi la Moshi na kuandaa mipango ya kuvamia kwa lengo la kuwaua Wakenya hao.

Mtoa habari aliyezungumza kwa sharti la kutotaka jina lake litajwe, ameliambia gazeti hili kuwa, baada ya kufanikiwa kuwaingiza nchini raia hao wa Kenya, kilichofanyika ni utekelezaji wa hatua ya mwisho.

“Kama unavyoona hapa (eneo la tukio) ni sehemu yenye uwazi mkubwa, sasa kama lingekuwa tukio la kurushiana risasi, kwa nini polisi wasidhurike?” alihoji mtoa habari huyo.

Inadaiwa watu hao walikusanywa kama panya ndani ya mtego na kuwekwa kwenye magari ya polisi yenye nambari za kiraia na kupelekwa eneo ambako polisi wanadai ni maficho ya majambazi hao.

Huko ndiko kunakodaiwa mpango huo wa kuwaua ulianza kutekelezwa kwa kuuawa mmoja baada ya mwingine, huku polisi wakiyachakaza kwa risasi magari mawili likiwamo la kwao kama njia ya kuficha ukweli.

Katika kuonyesha kuwa tukio hilo lilikuwa sawa na mchezo wa kuigiza, gari la polisi T 168 AEA Hiace GLX, lilipigwa risasi zikatokea kwa juu huku kioo cha mbele kikiwa hakijapata madhara yoyote.

“Angalia kwa makini hilo gari lao (la polisi), utaona risasi zimepenya juu ya gari bila vioo vya mbele kuathirika… sasa kama lilikuwa ni tukio la kurushiana risasi, kwa nini vioo vya mbele visichakazwe na majambazi hao?” alihoji mtoa habari wetu.

Inadaiwa hata kitendo cha Wakenya hao kwenda ndani ya benki hiyo kwa lengo la kubadili fedha za kigeni, ni mpango ambao ulikuwa umeandaliwa na makachero hao kama njia mojawapo ya kukusanya ushahidi wa mazingira.

Mbinu nyingine iliyotumiwa katika mpango huo, ni kuwatawanya Wakenya hao kwenye nyumba mbalimbali za kulala wageni na kuweka kisingizio kuwa walikuwa wakitafuta vyumba vya kulala.

Baadhi ya nyumba hizo ni pamoja na baa maarufu mjini hapa ya Flamingo na Mkulima ambako watu waliokuwepo katika baa ya Flamingo walithibitisha kuwaona Wakenya hao wakitafuta vyumba vya kulala.

Kwa upande wa wananchi wa kawaida waliozungumza na Tazania Daima, wakiwamo wanaoishi karibu na kulikotokea tukio hilo, wamedai bado polisi wanahitajika kutoa taarifa za kweli juu ya kilichotokea.

Wanadai taarifa ya Jeshi la Polisi haiweki wazi ni katika mazingira gani watu hao 14 walipatwa na risasi na kufa wote pasipo hata mmoja kujeruhiwa huku polisi wakitoka salama.

“Kama ni suala la uzalendo sawa, lakini tukiamua kusaka ukweli wa tukio hili, bado kuna maswali mengi… haiwezekani brother (mwandishi), upande mmoja ukaathirika kwa asilimia 100 katika tukio la kurushiana risasi na upande wa pili usiathirike hata kidogo, hapa kuna kitu,”alisema mwananchi mmoja.

Wafanyakazi wa shamba la kahawa la Two Bridges ambako mauaji hayo yanadaiwa kutekelezwa na polisi, wameliambia Tanzania Daima kuwa, hawaelewi kilichotokea zaidi ya kusikia milio ya risasi na hivyo kuzima jenereta waliyokuwa wakiitumia shamabani hapo na kujikusanya sehemu moja.

Wafanyakazi hao wamedai tangu mchana kabla ya tukio hilo, waliwaona askari waliokuwa wakirandaranda maeneo ya tukio pasipo wao kuelewa kinachoendelea.

Utata mwingine unaozidi kuligubika tukio hilo, ni maelezo ya polisi kuwa, waliweka gari lao kama kizuizi wakati eneo hilo la tukio upo uwazi mkubwa ambao hauzuii gari jingine kupita.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanaunga mkono mauaji hayo bila kufafanua zaidi kwa madai kuwa, matukio ya ujambazi, hasa wa kutumia silaha nzito zikiwamo za kivita huku yakiwahusisha raia wa nchi jirani, yameonekana kuota mizizi nchini.

Septemba 5, mwaka huu, saa 1.30 katika eneo la Weruweru ndani ya eneo la mashamba ya kahawa ya Two Bridges, polisi waliwaua watu 14 wakidai kuwa ni majambazi waliokuwa na mpango wa kuvamia benki ya Exim, iliyopo barabara ya Boma mjini Moshi.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, polisi walidai kupata taarifa za kuwepo kwa watu hao na kwamba mtego wa kuwanasa uliandaliwa na wakafanikiwa kuwaona wakielekea mafichoni kabla ya uvamizi huo.

Waliouawa katika tukio hilo ni Simon Maina Ndabuki, Moses Kuria Kamau, David Njuguna Mbugua, Peter Maina Waweru, William Muiruri Kamau na Phillipo Irungu Wanjiru.

Wengine ni Rudovick Giceru Kariuki, John Gikonyo Buku, Zacharia Mwangi Kamathiro na Jeremiah Macharia, wote wakazi wa jijini Nairobi.

No comments: