Friday, September 14, 2007

Mwamunyange awa Mkuu mpya wa Majeshi

RAIS Jakaya Kikwete amempandisha cheo Luteni Jenerali Davis Adolf Mwamunyange, kuwa Jenerali na kumteua kuwa Mkuu wa Majeshi.

Jenerali Mwamunyange anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali George Waitara, ambaye amestaafu rasmi jana.

Kabla ya uteuzi huo, Mwamunyange alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana usiku na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, ilieleza kuwa wakati huo huo, Rais Kikwete amempandisha cheo Meja Jenerali Abdulrahman Amir Shimbo, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kuwa Luteni Jenerali, na kumteua kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ.

Luteni Jenerali Shimbo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Mwamunyange.

Aidha, Rais Kikwete amempandisha cheo Brigedia Jenerali Martin Madatta, kuwa Meja Jenerali, na kumtea kuwa Mkuu wa JKT, nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Jenerali Shimbo.

Kabla ya uteuzi huo, Meja Jenerali Madatta, alikuwa Mkuu wa Uzalishaji Makao Makuu ya JKT.

Uteuzi wa viongozi hao umeanza jana.

Mkuu mpya wa Majeshi, Jenerali Mwamunyange, na Mnadhimu Mkuu wa Majeshi, Shimbo, wataapishwa Jumamosi ijayo, saa 2 asubuhi, Ikulu, Dar es Salaam.

Naye Safina Tibanyendera, anaripoti kuwa aliyekuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama anayemaliza muda wake, Jenerali George Waitara, amepiga marufuku imani ya dini ya kilokole ndani ya jeshi hilo, kwa madai kuwa ulokole unaweza kumtoa mtu katika taratibu za kijeshi.

Waitara alisema hayo jana wakati wa sherehe za kumuaga zilizofanyika makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam na kuwataka maofisa wa jeshi hilo wanaojiona wameokoka kwenda makanisani kuliko kuendelea kuwa wanajeshi.

“Tusiingize ulokole kwenye jeshi…imani ni imani, kiongozi akiwa mlokole na wafuasi walokole itakuwaje? Tukianza kusema huyu hastahili kufanya kazi hii kwa sababu ni mlokole, hapo tutakuwa tunaleta migawanyiko, na mtu wa namna hiyo anayeleta ulokole kwenye jeshi, kazi itamshinda,” alisisitiza Waitara.

Aidha, aliwataka maofisa wengine kumpa ushirikiano wa kutosha mtu atakayechaguliwa kushika nafasi yake, ambaye anatarajiwa kutangazwa na kuapishwa wakati wowote kuanzia sasa.

“Mafanikio mliyoyaona kipindi chote cha uongozi wangu, ni kwa sababu ninyi mlionyesha ushirikiano pamoja na mimi ndiyo maana tumepiga hatua katika mambo mengi, hivyo nahimiza mshikamano…muwe kitu kimoja, kwa sababu jeshi ni moja, msigawanyike,” alisema.

Waitara, aliwaasa viongozi wote wa vikosi vya jeshi kuacha ubaguzi, kwani unaweza kusababisha mgawanyiko na makundi ndani ya jeshi hilo, jambo ambalo linaweza kushusha tija katika ufanisi jeshini hapo.

Aidha, aliwakemea wanajeshi wanaoharibu sifa ya jeshi kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, na kudai kuwa watu hao hawatakiwi ndani ya jeshi, kwa hiyo viongozi wa vikosi wawe macho kuhakikisha wanawatambua wanajeshi wanaowasimamia tabia zao ili mkorofi aweze kufukuzwa mara moja.

“Hata tuhuma peke yeke haifai kwa mwanajeshi, viapo vyenu vya kuwalinda raia vinakuwa tofauti, mimi nahisi watu hao waliingia jeshini kwa ajili ya kutafuta ajira, tusiwape nafasi tuwaondoe mara moja,” alisema.

Alisema, kipindi cha uongozi wake amejitahidi kupunguza matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wanajeshi kama chakula, mavazi na malipo yao ya likizo ambayo hivi sasa yanatolewa kwa wakati pamoja na fedha ya usafiri.

Akizungumzia bima ya afya, aliwataka maofisa wote wa jeshi kukata bima ya afya, na kwamba watakaoingia mwaka wa kwanza (wageni), itakuwa ni kama sheria kwao kuhakikisha kuwa ni lazima kukata bima ya afya kabla ya kujiunga na jeshi hilo.

Akisoma risala, Kamanda wa Kikosi cha Makao Makuu ya Jeshi, Kanali Salum Kijuu, amempongeza Jenerali Waitara kwa mambo mazuri ambayo ameyafanya na kumtaka aimarishe afya yake kwa kufanya mazoezi ili asizeeke haraka.

Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na kusimamia nidhamu ya jeshi, ujenzi wa ukuta wa jeshi, kukarabati majengo machakavu na vyoo, kujenga kisima cha maji, kuongeza mishahara, pensheni, marupurupu na kuboresha uwanja wa kuchezea gofu.

Jenerali Waitara amelitumikia jeshi hilo kwa kipindi cha miaka sita tangu alipochaguliwa Julai Mwaka 2001.


Chanzo cha habari: Tanzania Daima.

No comments: