MREMBO wa Tanzania, Richa Adhia, amesema si jambo la busara kwa Watanzania kuanza kubaguana kwa misingi ya rangi, ukabila na udini.Richa alisema hayo jana alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Power Breakfast cha Radio Clouds FM ya jijini Dar es Salaam.
Mrembo huyo aliyetwaa taji hilo Jumamosi iliyopita, alikuwa akijibu swali juu ya malalamiko yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba hakustahili kuwa mshindi wa shindano hilo kwa sababu ni Muhindi.
“Nilishangaa niliposikia maneno haya, sikutegemea kabisa kwamba watu watasema hivi. Imeniuma sana kwa sababu nilianza kushiriki mashindano haya tangu ngazi ya vitongoji, lakini hawakusema kitu.
“Watanzania tumekuwa na utamaduni wa kuishi pamoja kwa miaka mingi bila ya kubaguana kwa misingi ya rangi, ukabila na udini. Wanaosema mimi ni Muhindi nawashangaa. Mimi nimezaliwa Tanzania, nimekulia hapa na wala sijawahi kufika India,” alisema.
Richa alisema suala la rangi halina nafasi katika dunia ya sasa na kwamba ushiriki wake katika shindano hilo ulilenga kuonyesha kuwa Tanzania ni taifa la watu wa rangi, dini, kabila na itikadi tofauti.
Mrembo huyo alisema wazazi wake wote wawili ni Watanzania, mama akiwa mzaliwa wa Pemba, wakati baba yake ni mzaliwa wa mkoa wa Morogoro.Alisema alizaliwa mkoani Dar es Salaam mwaka 1988, akiwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wane, na alilelewa katika mji wa Mwanza. Alisoma katika shule tofauti mkoani Mwanza na Dar es Salaam, na ana uwezo wa kuzungumza vizuri lugha ya Kisukuma.
Richa alisema aliwahi kuiwakilisha Tanzania katika shindano la dunia la ‘Miss Arts’ lililofanyika mwaka jana nchini Philippines na ana uzoefu na fani ya urembo.Alisema safari ya Philippines ilikuwa ya kwanza kwake kutoka nje ya Tanzania. Katika shindano hilo, Richa alisema aliingia hatua ya 15 bora.
“Nina uzoefu wa mashindano haya kutokana na kushiriki shindano la Miss Arts mwaka jana. Mungu ndiye anayejua kama nitaweza kufanya vizuri kwenye shindano la dunia. Nitashirikiana na kamati ya Miss Tanzania ili kuhakikisha nafanya vizuri,” alisema.
Akizungumzia ushiriki wake katika mashindano ya mwaka huu, Richa alisema mwanzoni, baba yake alikuwa na wasiwasi na hakuufurahia uamuzi wake, lakini baada ya kuhudhuria shindano la Miss Kinondoni, alimpa baraka zote.
Kwa upande wa mama yake, alisema alikuwa akimpa moyo wa kushiriki na kufanya vizuri tangu aliposhiriki shindano la Miss Dar City Center na amempatia ushirikiano mkubwa.
Richa, ambaye elimu yake ni ya kidato cha nne, kwa sasa ni Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi wa Kampuni ya Berger Paint Limited ya Dar es Salaam. Amewataka Watanzania kumpa ushirikiano ili aweze kupeperusha vyema bendera ya nchi katika shindano la dunia, linalotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu mjini Sanya, China.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lino Agency, inayoandaa mashindano hayo, Hashim Lundenga, alisema moja ya sifa za washiriki ni kwa mrembo kuwa raia wa Tanzania wa kuzaliwa ama kuandikishwa.
Alisema maswali yanayoulizwa kwa washiriki siku ya fainali si kigezo cha kumpata mshindi, kwa vile mchakato wa kutafuta mshindi haufanyiki siku ya mwisho tu.“Tusilaumu, tunapaswa kujua kanuni, sheria na taratibu za mashindano. Maswali yanayoulizwa siku ya fainali yanachukua asilimia 15 au 20 tu. Mchakato mzima wa kumpata mshindi unaanza tangu siku ya mwanzo warembo wanaporipoti kambini,” alisema.
Lundenga alisema uwezo wa kujieleza ni muhimu kwa vile lengo la kumpata mwakilishi katika shindano la dunia sio kumuwezesha ashinde, bali pia kuitangaza nchi kimataifa.
“Tunataka kuitangaza nchi, sio tu kumpata mrembo mwenye uwezo wa kutwaa taji la dunia. Vigezo ni muhimu na vipo vingi,” alisema.
Kutoka gazeti la Uhuru: Na Rashid Zahor, Jumatano, 5.9.2007
Mahojiano na Richa: http://bongocelebrity.com/2007/09/01/miss-tanzania-
2007-ni-richa-adhia/#comments
Mahojiano na Richa: http://bongocelebrity.com/2007/09/01/miss-tanzania-
2007-ni-richa-adhia/#comments
No comments:
Post a Comment