Monday, September 24, 2007

Sungusungu wabakaji jihadharini!!!!



“Mchezo wao umeanza hivi karibuni, wanapovamia eneo huwa ni kasheshe, halafu wanajitambusha wao ni sungusungu, mwanzoni tuliamini,” alisema mmoja kati ya vyanzo vyetu. Iliongezwa na vyanzo hivyo kuwa haikuwachukua muda mrefu kubaini kwamba watu hao si askari kama wanavyodai.

“Sungusungu gani wakivamia eneo wao wanakamata wanawake peke yake? Ikabidi tuanze kufuatilia, ndipo tukagundua kumbe wakiwachukua huwa hawawapeleki polisi kama ambavyo huwa wanadai. “Wanaenda nao uchochoroni na kuwabaka, hili lilithibitika zaidi baada ya kumbaka mwanamke mmoja hivi karibuni hadi kufa, kwahiyo hao siyo sungusungu na wanatupa ‘presha’ kweli kweli,” alisema mtoa habari wetu mwingine.

Baada ya kupata habari hiyo kutoka kwenye vyanzo vyetu, Timu ya Ijumaa Wikienda, ilienda eneo husika ili kunasa ‘live’, mchezo mchafu wa sungusungu hao ‘feki’. Usiku wa manane wa kuamkia Alhamisi (Septemba 20, 2007), waandishi wetu walishuhudia kundi la vijana wapatao sita ambao walifika kwenye Baa ya Rambo na kujitambulisha kama sungusungu. Mara walipojitambulisha, sungusungu hao wwbandia walimkamata binti aliyefahamika kwa jina la Aisha Peter, waliyedai ni mfanyabiashara wa kuuza mwili (changudoa).

Walipomkamata Aisha, Sungusungu hao walidai wanampeleka Kituo cha Polisi Urafiki, Dar es Salaam. Baada ya kushuhudia picha hiyo, gazeti hili liliwasiliana na polisi wa Kituo Kidogo cha Manzese ambapo lilikabidhiwa askari mmoja na kuanza kuwafuatilia sungusungu hao na binti waliyemkamata. Hatua chache kutoka Kituo cha Polisi Manzese, polisi huyo na waandishi wetu, waliweza kuwashuhudia sungusungu hao wakiwa kwenye jaribio la kumbaka binti waliyemteka, katika moja ya vichochoro vya Manzese Tip Top.

Hata hivyo, wabakaji hao walitawanyika baada ya polisi kupuliza filimbi, ingawa jopo la waandishi wetu lilifanya ukomandoo kwa kumsaidia askari kumtia nguvuni mmoja wa watuhumiwa, kama picha zinavyoonekana ukurasa wa kwanza.

Mtuhumiwa huyo baada ya kukamatwa, aliweza kutambuliwa na Aisha kwa jina la Imma Santana, kutokana na jinsi alivyosikia akiitwa na wenzake. Akiwa karibu kufikishwa kituoni, Santana alimponyoka askari na kutoroka, ingawa baadaye shauri hilo lilifunguliwa jalada namba MZP/RB/2328/07 Ubakaji katika Kituo cha Manzese.

Akiongea na gazeti hili, Jumamosi iliyopita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow alisema, atafuatilia kwa ukaribu kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake. Gazeti hili, linamuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, kuingilia kati na kudhibiti ukatili wa aina hii.azeti hili, linamuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, kuingilia kati na kudhibiti ukatili wa aina hii.

Habari hizi toka: Global Publishers Tanzania.

No comments: