Tuesday, September 04, 2007

UGONJWA MPYA : Uumbuajiasis Viongozitanzanialitis Hadharanum

Ugonjwa uliomuua Amina!

Ugonjwa huu mpya ambao aliugua Bi. Chifupa na uliosababisha mauti
yake kwa jina la kitaalamu hujulikana kama Uumbuajiasis Viongozitanzanialitis Hadharanum.Ugonjwa huu unatokana na kufuatilia mambo ya serikali na viongozi kwa karibu kiasi cha kutaka kuweka ubovu wao hadharani.

Dalili kubwa za ugonjwa huu ni hizi:
a. Kupenda nchi zaidi kuliko chama

b. Kuwa tayari kutetea mali ya Taifa na kuilinda mali hiyo

c. Kutoogopa yatakayokukuta
karibu
d. Kuanza kuweka hadharani ubovu na siri za viongozi hasa kwa jamaa yako wa karibu
e. Kutosikiliza ushauri wa kutakiwa kukaa kimya na wakubwa wako
f. Kuwa kimbelembele kuzungumza na kukemea maovu kila upatapo nafasi

g. Kuwa mtetezi wa Katiba na mkosoaji wa jamii
h. Kutolegeza msimamo hadi kifo.

Maambukizi:
Ugonjwa huu unaambukiza watu wachache kwani watu wengi wameshapatiwa kinga yake. Kwa wale wanaombukizwa wanafanya hivyo zaidi kwa kusoma habari za ufisadi, rushwa, na ubadhirifu katika serikali yao. Kwa
kupitia
mitandao, vitabu, na vyombo vya habari virusi vya ugonjwa huu vinajipenyeza katika akili za watu na kusababisha kusisimka kwa ubongo. Wale waliombukizwa ugonjwa huu hujikuta wakitafuta habari za kila namna na kushiriki mijadala yenye kutafakari mustakabali wa Taifa lao.

Kinga:
Ugonjwa huu kinga yake kubwa hujulikana kwa kitaalamu kama Mrungura. Kinga hii hutolewa kwa wale wote wenye kuanza kuonesha dalili za kukumbwa na ugonjwa huu. Kinga hii huwekwa kwenye mabenki na maofisi mbalimbali ili kuzuia viongozi wakubwa wasipatwe na virusi vya ugonjwa huu. Kinga hii pia hufanya kazi kwa wale walioanza kuonesha dalili kama kina Phillip Marmo, Chrisant Mzindakaya n.k Pindi mtu akishapatiwa kinga hii HAWEZI kuipinga serikali!

Tiba:
Hadi hivi sasa ugonjwa huu hauna tiba ya uhakika kwani wale ambao wameshaugua kwa muda mrefu hawako tayari kutibiwa kwani wanaona wanaishi vizuri tu na ugonjwa huu.

Karantini:
Pindi baadhi ya wakubwa wakiona kuna mtu ambaye amefikia hatua ya juu kabisa ya ugonjwa huu basi kwa mbinu wanazozijua wenyewewanamkarantini, na wakati mwingine anakuwa katika hali hiyo ya kutengwa hadi kifo ili asiendelee kuwaambukiza watu wengine. Jihadhari: Kwa vile ugonjwa huu ni wa hatari, watu wabadhirifu, wezi wa mali ya umma, walaghai, na mafisadi hawawezi kuustahimili. Ugonjwa huu ni kinyume kabisa na watu hawa hivyo kama hutaki kuambuzizwa hakikisha unaendelea kujikita katika katika vitendo viovu vya kuharibu mali za umma na kuivunja vunja nchi huku ukishiriki katika kumegeana hadhina ya Taifa. Kwa vile ugonjwa huu unaendelea kuambukiza taratibu, kuna kila dalili hapo
ulipo UNAISHI NA MWATHIRIKA.

Kutoka (Jumanne 04.09.2007):
darcity@yahoogroups.com


No comments: