Friday, September 28, 2007

Ustadhi afunga ndoa na mke wa mgoni wake!


Akisimulia mkasa huo, Kidevu alisema kuwa yeye ni mpangaji katika nyumba ya familia ya Lunyungu, ingawa mwenye nyumba huyo alikuwa akiishi Mabibo lakini mara kwa mara alikuwa akifika nyumbani kwake (Kidevu) kumtembelea.

Kidevu alisema, siku moja kabla ya tukio, Lunyungu alifika nyumbani kwake ambapo kuna grosari na kuagiza kinywaji kisha baada ya muda yeye na mkewe wakatoweka.

"Kitendo cha kutoweka kwa mke wangu katika mazingira ya kutatanisha kukanifanya niingiwe na wasiwasi, hata hivyo, nikavuta subira nikiamini kuwa angerudi lakini hadi usiku hakurejea. Nikachukua jukumu la kwenda kwa dada yake anayeitwa Jaka anayeishi Kigogo kumtaarifu juu ya suala hilo," alieleza Kidevu

Aliongeza kuwa siku hiyo mkewe hakurudi kabisa nyumbani hadi kesho yake alipopewa taarifa na mke wa Lunyungu aitwaye Pili Said kuwa alimuona Leila akiwa na Lunyungu katika Baa ya Mississippi wakiponda raha na kumuomba waende kuwafumania.

"Taarifa hiyo ilinishtua, hivyo tulifuatana pamoja na wapambe hadi kwenye baa hiyo na kufanikiwa kuwafumania wagoni hao wakiwa katika mahaba mazito, lakini walipotuona walikimbia," alisema Kidevu.

Aliongeza kuwa baada ya wagoni wao kukimbia, yeye na Pili waliumia sana moyoni hivyo, waliamua kurudi nyumbani ili kuwasubiri lakini kilichowashangaza ni kuwa watu hao hawakurudi.

Aidha, Kidevu alisema baada ya kuona wawili hao hawatokei walikubaliana kuwa nao wafunge ndoa kwa vile mkewe na Lunyungu walikuwa wamesaliti ndoa zao.

"Tulifikia uamuzi wa kuoana, baada ya kuona Lunyungu amekimbia na mke wangu nami ikabidi nimchukue mkewe, nikaandika talaka siku hiyo hiyo, saa kumi nikapeleka posa ya kumuoa mke wa Lunyungu na ikakubaliwa, hivyo tangu siku hiyo tunaishi pamoja," alisema Kidevu.


Naye aliyekuwa mke wa Lunyungu, Pili Said alimwambia mwandishi kuwa amefurahishwa na uamuzi waliouchukua kwani alikuwa akifikiria ataishi vipi baada ya kukimbiwa na mumewe.
"Leila amekimbia na mume wangu nami inabidi niishi na mume wake, nilikuwa nikifikiria wapi nitaenda lakini nimefurahishwa na uamuzi tuliouchukua, nina imani tutapendana na kuishi kwa amani katika ndoa yetu," alisema Pili.

Hata hivyo, habari zaidi zinasema kufuatia fumanizi hilo aliyekuwa mke wa Kidevu (Leila) amekuwa akimpigia simu mumewe na kuomba radhi ili warudiane lakini mumewe amekuwa akikataa.

No comments: