Thursday, October 18, 2007

BARUA YA BUTIKU KWA MKAPA, ENZI MKAPA AKIWA MWENYEKITI WA CCM.

CCM imepoteza dira

MHESHIMIWA Mwenyekiti,
Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa nakuomba uvumilie na uisome barua hii tangu mwanzo hadi mwisho.

Ni barua yangu kwako kama Mwenyekiti wa Chama chetu, nami naileta kwako ni Mwana-CCM mwaminifu wa Chama changu – CCM – na viongozi wake wote.

Lakini pia nimandika barua hii kwa kuzingatia haja ya kukidhi ahadi moja ya CCM isemayo – NITASEMA KWELI DAIMA, FITINA KWANGU MWIKO. Hii siyo barua ya tuhuma, wala dharau au kiburi. Nimeandika kwa IMANI kubwa niliyonayo kwako na kwa chama chetu na misingi yake iliyotudumishia Amani na Umoja. Nimeandika kwa sababu zifuatazo:

Kwanza: Mimi ni mwana CCM wa siku nyingi, nimeingia TANU mwaka 1958, nikiwa darasa la 12 Tabora Boys Sekondari, umri wangu wakati huo ukiwa miaka 20. Tabia yangu ya utu uzima, imejengwa kwa kiasi kikubwa sana na malezi niliyoyapata katika Chama cha TANU na CCM baadaye.

Pili: Mimi ni muumini kama wana-CCM wengine, katika misingi, imani, maadili na taratibu za uongozi na uendeshaji wa CCM. Nafadhaika ninapoona dalili za kupuuzwa au kusahaulika, kwa misingi hiyo na imani na maadili ya chama chetu.

Tatu: Nimekuwa miongoni mwa viongozi wa ngazi za taifa katika serikali na chama kwa miaka mingi. Imani yangu ni kwamba bado mimi ni kiongozi na msaidizi wako nikiwa sina wadhifa wowote serikalini na katika chama.

Mimi sasa ni mmoja wa raia watiifu lakini bado ni kiongozi. Mzee mstaafu ni kiongozi, siruhusiwi kama viongozi wenzako wenye NYADHIFA nilizoshiriki kuhakikisha baadhi yenu mnazipata, na kuwapa ujumbe na maoni yangu kwa nia njema kabisa.

Nne: Naamini, kama wewe unavyoamini, katika msingi wa UWAZI na UKWELI. Nimeishi hivyo miaka yote; ndivyo nilivyolelewa na chama, wazazi wangu na Baba wa Taifa, Mwalimu J.K. Nyerere, ambaye, kama alivyofanya kwa viongozi wengine wengi wa taifa letu, amekulea wewe kisiasa na kukusaidia kukufikisha katika nafasi uliyo nayo leo ya Urais na Uenyekiti. Siwezi kuvumilia ubaya wa dhahiri mbele ya macho yangu, hupenda kusema kwa wahusika ili tujadili na kuafikiana tufanye nini. Huu ni wajibu wangu nikiwa raia mwema na mtiifu.

Tano: Mimi naamini CCM sasa imeanza safari ya kuelekea kwenye kifo chake, imekumbatia jambo ovu – RUSHWA – ambayo imeua viongozi wazuri wengi, vyama vya siasa na serikali makini duniani.

CCM imeanza kushindwa kusema na kutetea HAKI na UKWELI; imeanza kuvumilia na kutetea UBAGUZI: Imeanza kuwa CCM ya viongozi wafanyabiashara wanaoonyesha nia ya kutaka kubinafsisha CCM, na wasioonyesha nia thabiti ya kujali MAADILI ya chama chetu na taifa letu, siyo viongozi wa watu wanyonge tena.

CCM inaanza kushindwa kutofautisha kati ya wema na uovu, kati ya mwenendo unaoweza kuvunja UTAIFA wetu, na ule unaoweza kudumisha amani na Umoja wa taifa na raia zake. Kati ya rafiki na adui na sasa imeanza kuachana na siri kuu ya uhai wake KUHESHIMU WATU na mazungumzo ya wazi wazi ndani na nje ya vikao, juu ya jinsi ya kuendesha na kusimamia mambo ya WATANZANIA.

Badala ya uongozi wa CCM kuheshimu wanyonge na kutetea haki za wote pamoja na wanyonge, chama kimeanza kujenga tabaka la viongozi wenye mali au wanaowekwa katika nafasi za uongozi na wenye mali au kwa kutumia mali zao wao wenyewe, ili wapate nafasi za kufanya mambo yao.

Mali imeanza kuchukua nafasi ya uzalendo na kutumiwa na viongozi wengi wa CCM kama nyenzo ya uongozi bora wa kisasa. CCM imeanza hata kutoona haya, na viongozi wakuu, chini ya uongozi wako sasa wamenyamaza, wanaona haya kukemea uovu.

Sita: Taasisi ya Mwalimu Nyerere inafanya kazi unayoikubali: kutukumbusha wakati wote kuhusu misingi ya amani, umoja na maendeleo yenye tija kwa Watanzania wote.

Hoja za msingi

Nitaanza na tuhuma kwa chama, nikilenga vikao vya uongozi wa CCM kitaifa: Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM na uongozi wa vikao hivyo.

Vikao hivyo vimevunja miiko na maadili ya chama chet. Vimeruhusu rushwa, ubaguzi na vimeruhusu CCM ibinafsishwe kwa wenye fedha zao. Nitatoa mifano michache kama ushahidi: Mifano hii inahusiana zaidi na yaliyotokea wakati wa uchaguzi wa jumuia za CCM na wakati wa maandalizi ya uteuzi wa wagombea wa urais, ubunge na udiwani kupitia tiketi ya CCM (2005).

Mfano wa kwanza: Viongozi wakuu wa CCM, ambao pia ndio wajumbe wa vikao vya CCM kitaifa, hawakutani na kuzungumza nje ya vikao hivyo. Wanakwepana na kuogopana, au kuheshimiana kwa unafiki (isivyo kweli), na hivyo wanalalamikiana, wanasengenyana; wanakosa uongozi wa pamoja wa kushauriana, na kuelewana.

Tabia hii imekigawa chama, maana viongozi wamegawanyika. Kabla ya vikao vya uteuzi wa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya CCM, nilijitahidi, mwezi Mei, 2005, nikiwa kama mmoja wa wasaidizi wako na viongozi wengine, nikiwa pia mtendaji mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, inayojishughulisha na amani na umoja, kukutana na baadhi ya viongozi wangu wakuu wa CCM, kuzungumzia hali halisi ya amani na umoja katika Taifa letu. Wote walisema hawaridhiki na hali halisi ya taifa.

Walilalamika, baadhi yao wakikulaumu wewe Mwenyekiti wetu wa CCM, kwamba unakataa kukutana nao kila wakileta maombi yao. Baadhi ya viongozi wa CCM – Zanzibar walisema hivyo hivyo na baadhi ya wale wa CCM Bara nao walisema vivyo hivyo.

Lakini hata katika Mkutano Mkuu wa CCM wa uchaguzi (2002), nilishuhudia mwenyekiti wa wilaya moja, aliyesimama kutaka tu kujua sababu za msingi zilizoifanya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, ifute utaratibu wa mgombea wa kiti cha mwenyekiti taifa, naye kusimama mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na kuomba kura kama wengine.

Badala ya kumjibu vizuri mwenyekiti huyo, ambaye pia alikuwa mjumbe halali wa kikao hicho, alikemewa na kuzomewa. Miongoni mwa waliomkemea na kumdhalilisha ni wajumbe wa Kamati Kuu, ambao ni viongozi wakuu wa chama.

Mimi nilishangaa na kusikitika. Haki ya mjumbe ya kusema katika kikao chake inageuzwa kuwa kosa!

Kwa maoni yangu, kosa kubwa ni la Mwenyekiti wa taifa na viongozi wenzake wa Halmashauri Kuu ya Taifa. Naamini hawakutaka kuutolea maelezo utaratibu huu mgeni na mpya mbele ya Mkutano Mkuu wenye madaraka ya kuhoji kila uamuzi wa vikao vya chini yake.

Ikiwa mwenyekiti wa wilaya hakuwa na habari na huo utaratibu mpya, hata akataka uelezwe ili auelewe, na labda kuwasaidia wengine nao wauelewe, huu ni ushahidi wa kutosha kwamba CCM, chini ya viongozi wake wakuu, imeanza safari ya kukataa majadiliano miongoni mwa viongozi na wanachama pia.

Mazungumzo ya wazi wazi na nafasi ya kuzungumza ni moja ya nguzo muhimu ya chama chochote kizuri kinachojiheshimu. Nguzo hii ikipuuzwa au kuvunjwa, chama hakipo, hata kama viongozi wapo.

Ndugu Mwenyekiti, huenda unakumbuka pia kwamba katika mkutano huo, hapakuwa na nafasi ya majadiliano au kuuliza maswali yoyote kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Halmashauri Kuu au jambo lolote la sera za CCM na utekelezaji wake. Wageni waalikwa walipata nafasi katika siku mbili, kutoa salamu zao.

Lakini wajumbe zaidi ya 1,703 waliosafiri masafa marefu kuja Dodoma, hawakupata nafasi ya kujadili lolote la CCM isipokuwa kuchagua viongozi wao na kutawanyika.

Waliambiwa warudi wajadili taarifa ya NEC katika vikao vya mkoa. Hii ni kasoro kubwa ya uongozi na uendeshaji wa chama. Kusema kweli mkutano huo haukumwachia mwenyekiti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ‘mandate’ yoyote kuhusu sera za chama na utekelezaji wake.

Mfano wa Pili: Vikao vya uteuzi vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa Mei, 2005.

Mambo mengi yamesemwa kuhusu kasoro za vikao hivi. Sitaeleza mengi, nitataja tu yale machache niliyoyasikia, na baadaye nikafanya jitihada za kuyathibitisha kwa njia mbalimbali: Kasoro za msingi:

Kasoro za Uenyekiti wa CCM Taifa

Kwamba Mwenyekiti aliamua mapema kumuengua Makamu wa Mwenyekiti, Mzee J. S. Malecella, asigombee, inaelekea bila mashauri kati yake na makamu wake au Kamati Kuu.

Hatua hii ilileta aibu sana mbele ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa wakati Mwenyekiti na Makamu wake wanabishana na kubadilishana maneno yasiyofaa mbele ya viongozi wenzao.

Inashangaza kusikia eti kumbe Makamu Mwenyekiti alikata rufaa akaenda kulalamika mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa. Kule mzozo ukawa mkubwa zaidi, Mwenyekiti akijitetea kwa kusema Makamu wake hakumuuliza na wala hakutaka ushauri wake, wakati ameamua kugombea eti hii labda ni dalili ya dharau kwa mwenyekiti au kutojali umuhimu wa mashauriano.

Lakini naambiwa mwenyekiti naye hakujitahidi kumwita makamu wake amtake maelezo ya uamuzi wa kugombea bila kutaka kushauriana au hata kumnong’oneza maoni yake kuhusu uamuzi wa makamu kugombea.

“Viongozi wote wawili, Mwenyekiti na Makamu hawakuzungumza mapema. Kwa kweli Mwenyekiti, Makamu hawakuzungumza mapema. Kwa kweli Mwenyekiti aliwahi kumpiga kirungu makamu wake aliposema kwenye vyombo vya habari kulikuwa na “kigogo” mmoja wa chama anayemlaumu yeye (Mwenyekiti) kwa kukiuka au kukidhoofisha chama.

Upo ushahidi kwamba makamu anaamini mwenyekiti wake hakumpenda kutokana na uchonganishi wa fitina wa baadhi ya washauri wa karibu wa mwenyekiti.

Inawezekana haya yote ni mambo yasiyo na uzito au ukweli kamili. Lakini ikiwa kasoro hii ina kiasi fulani cha ukweli, ni kasoro inayohusu uongozi, si vizuri ikafumbiwa macho na CCM. Kundi la viongozi wa ngazi za juu wanaolalamika na kutororidhika na uhusiano uliopo miongoni mwao na kati yao na Mwenyekiti ni kubwa. Haifai kuinyamazia. Nani asiyejua kwambå leo hii mwenyekiti na makamu wake hawachangamkiani?

Kubadili kanuni ya uchaguzi

Mwenyekiti aliamua, yeye mwenyewe katikati ya kikao na bila ushauri wa kiongozi mwingine yeyote, kubadili kanuni ya uchaguzi wa mjumbe mmoja kura tatu.

Kanuni hii ilikuwa imejadiliwa awali, kabla ya kikao cha Halmashauri Kuu cha tarehe 4/8/2005. Halmashauri Kuu chini ya Mwenyekiti, ikaamua kanuni hiyo isibadilishwe.

Lakini baadaye kanuni hiyo, ndiyo iliyobadilishwa, bila sababu yoyote ya msingi, kwa usimamizi wa shinikizo la Mwenyekiti wakati wa kikao cha uteuzi wa wagombea.

Hili kweli lililotokea; sababu zake, zinasemekana ni kuzuia ‘mizengwe’ iliyokuwa imejitokeza, ambayo ingeweza kuwazuia wana – CCM bora wasiteuliwe, na badala yake kutoa nafasi ya kuwateua wana – CCM wabovu kwa maana nyingi.

Utaratibu huu wa kura tatu ndiyo uliotumika katika uchaguzi wa CCM (1995); ukatoa nafasi kwa Ndugu zetu Mkapa, Kikwete na Msuya kushindana. Kwenye Mkutano Mkuu Ndugu Mkapa na Kikwete waliweza kurudiana na kugawana kura zaidi ya 300 alizokuwa amepigiwa Ndugu Cleopa Msuya. Wajumbe wa Mkutano Mkuu walipata nafasi ya kuwapigia wagombea waliowataka saa ya mwisho.

Huu ni utaratibu wa kawaida kwa mujibu wa katiba ya CCM (ikiwa haijabadilishwa) wa kupiga kura ndani ya Chama kwa kura za makundi wakati anatakiwa apatikane mgombea zaidi ya mmoja. Upigaji kura kwa ajili ya wagombea wa CCM ilikuwa wapatikane watatu wa kupelekwa kwenye mkutano mkuu ili apatikane mmoja.

Wajibu wa kusimamia utekelezaji wa katiba na Kanuni za Chama ni kwa vikao vya chama lakini ieleweke hapa kuwa tatizo siyo la Ndugu Kikwete, au wagombea wengine, ni tatizo la mwenyekiti alipoamua kuikataa kanuni, au kuwashawishi wajumbe wa kikao, katikati ya shughuli za uchaguzi, kubadili kanuni ya msingi iliyokuwa imejadiliwa awali na viongozi hao hao, wakaamua isibadilishwe.

Hii ni kasoro kubwa ya kikatiba. Viongozi wenzako hawakuridhika na utaratibu huu, wamelalamika, bado wataendelea kutoridhika na kulalamika. Hili si jambo la kukubali au kukataa matokeo ya uchaguzi, ni jambo kubwa la kuvunja kanuni ya uchaguzi katikati ya uchaguzi, bila kufuata utaratibu wa kutumia madaraka ya Mwenyekiti.

Wajumbe kunyimwa au kufichwa ushahidi

Mwenyekiti hakuwa tayari kuwasaidia wajumbe wenzake kupewa ushahidi wa vitendo vya kukiuka au kuvunja maadili ya chama ingawa kamati ya maadili ya CCM, na vyombo vya dola, vilikuwa vimeandaa taarifa kamili.

Kwa hiyo, vikao vya chama havikufanya maamuzi yaliyozingatia ukweli wote uliojitokeza. Hata pale baadhi ya viongozi walipodai kupewa ushahidi, Mwenyekiti hakutaka kufanya hivyo, eti ushahidi ulikuwa ni aina ya majungu.

Hili linaweza kuwa kweli, lakini ushahidi uliokusanywa ungetolewa kwa wajumbe waujadili, sio kuwaficha kama kwamba wao ni watoto wadogo, au viongozi wasio na uwezo wa kutambua ukweli na majungu.

Ni kosa kubwa kwa vikao vikubwa, vya uchaguzi kufanya maamuzi bila kuwa na ushahidi na maelezo ya kutosha. Uamuzi huu umekifanya chama kishindwe angalau kukemea tabia ya rushwa iliyokithiri na kukemea ubaguzi wa kila aina uliojitokeza katika jamii yetu.

Hivi sasa kelele zilizojitokeza kuhusu rushwa kabla ya vikao vya tarehe 3-4 Mei, 2005 zimezidi kusikika katika jamii yetu kutokana na tabia sugu ya wagombea wengi wa CCM ya kutumia fedha nyingi kuwanunua wapiga kura na kura zao katika vikao vya uteuzi wa kura za maoni.

Hakuna sasa kiongozi yeyote wa CCM anayekemea tabia hii. Hili ni tatizo zaidi la mwenyekiti, maana yeye ndiye mwenye dhamana ya kutoa na kuruhusu matumizi ya ushahidi uliokusanywa na vyombo vya taifa vilivyoteuliwa kufanya kazi hiyo- Kamati ya maadili yaa CCM, na vyombo vyote vya ulinzi na usalama vya kitaifa ambavyo viko chini ya Mwenyekiti ambaye pia ni Rais wa Jamhuri na Jemadari Mkuu wa Majeshi yote ya Taifa la Watanzani.

Kazi hii ni ya Mwenyekiti, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kiapo chake cha utii. Katiba na kiapo cha Rais cha utii kwa Katiba huo ndio mwiko mkuu wa msingi wa utendaji wa Mwenyekiti/Rais na viongozi wake wakuu wanaomsaidia.

Hata wale wasiokula viapo wanalazimika kutambua kwamba mkubwa wao – Mwenyekiti wa Rais wa Jamhuri amekula kiapo cha utii, uaminifu, ujasiri, kutopendelea na kukataa woga. Mwiko huu ukivunjwa, taifa linakosa msingi imara na kulisimamisha na kulihimili.

Mwiko huu ukivunjwa unaondoa uhalali wa maamuzi. Vyombo vyote vinaweza kubabaika, visiweze kuelewe kama viapo vyao vina maana yoyote, na labda wakadhani kazi yao moja ni kutetea ubaya, maana wakifanya kazi nzuri, matokeo yake yakakataliwa au kupuuzwa wanaweza wasielewe.

Maana ikiwa kweli kazi ya vyombo hivyo vya maadili inaweza wasielewe. Maana ikiwa kweli kazi ya vyombo hivyo vya maadili inaweza ikaonekana haifai, haitoshelezi au haisaidii lolote, huku vyombo vyenyewe vinaamini vimefanya kazi nzuri, iliyostahili kuwasilishwa kwa kiongozi wao mkuu wa nchi, lipo tatizo la msingi sana la imani.

Maadili ya taifa yakianza kuvunjwa, huku taifa lina vyombo vya kusaidia Mwenyekiti/Rais, na viongozi wenzake, kulinda maadili hayo yasivunjwe, raia wana haki ya kuwa na wasiwasi na kutaka vyombo hivyo vijieleze na viwajibike kwa wananchi, maana vyombo hivyo ni vyao.

Taifa zima linapiga kelele rushwa, rushwa, rushwa na labda siyo rushwa tu ni kuuza nchi kwa fedha zinazoonekana ni nyingi sana lakini zisizojulikana zinatoka wapi.

Wanayo pia haki ya kutaka maelezo ya Mwenyekiti/Rais wao kuhusu vyanzo vya fedha hizi zinazotumiwa kuvuruga Chama na taifa. CCM itake isitake inayo kasoro katika eneo hili. Na viongozi wa CCM hawana budi kukubali kuwajibika kwa wananchi kwa madhara yoyote yanayoweza kusababishwa na hali hii ya rushwa Sugu.

Mwenyekiti wa CCM ni rubani mkuu

Taifa likianza kupiga kelele kwa sababu rubani mkuu wa ndege yao (Tanzania) na wasaidizi wake (wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu), hawaonekani kutambua au kujali wasiwasi wa raia wao, (abiria katika ndege Tanzania), na hasa wanachama wao, matatizo yakitokea yakasababisha madhara kwa sababu tu ya wasiwasi wa raia, ulipuuzwa au haukushughulikiwa ipasavyo, viongozi wakuu hawawezi kukwepa lawama.

Hivi sasa wana CCM wengi, na raia wa kawaida wa Tanzania wengi wana wasiwasi. Hata wewe Mheshimiwa Mwenyekiti uliwahi kukiri ukweli huu. Nchi inanunuliwa kwa fedha kupitia viongozi wa CCM?

Maana upo ushahidi kuwa fedha nyingi zinatumiwa katika uchaguzi huu: zinatoka wapi na ni za nani? Hao wanaozitoa wanayo malengo gani kwa Tanzania na Watanzania?

Kwanini watu hao wanaojulikana wameamua kuwafundisha raia wa taifa letu tabia mbaya ya kuuza nchi yao na haki yao ya msingi ya kumchagua kiongozi wanayomtaka kwa hiari? Fedha zimetumiwa kuvunja kanuni kuu ya msingi – hali. Maskini, au hata wasio maskini wanaozipokea fedha na kuuza kura zao, wanashawishiwa kwa hizo fedha.

Kwa taifa letu sasa watu wanaotoa fedha zinazonunua kura za wana CCM wapiga kura, na labda kuiuza Tanzania kwa jumla ni watendaji na ni kosa la jinai. CCM itavunjika, kusambaratika na kuliletea taifa letu madhara makubwa sana.

Ni kasoro kwa uongozi wa CCM kulifumbia macho jambo hili au kukataa kukubali kwamba tunalo tatizo na kuogopa au kupuuza kulizungumza hivi sasa. Hili si tatizo la Mwenyekiti wa CCM au mtu yeyote peke yake. Ni tatizo la Taifa, kama ilivyo kwa tatizo la UKIMWI. Rushwa ni UKIMWI wa maadili ya taifa letu.

Rushwa ni rushwa: ni mbaya. Rushwa inayoendeshwa sasa na wagombea wetu wa uongozi katika Taifa letu, ni balaa kwa CCM na wana-CCM mimi ninao ushahidi wa Jimbo langu la Musoma Vijijii.

Rushwa ya aina hii haiwezi kubadilika ikawa kitu kizuri kwa sababu inaitwa takrima, ubaya wake uko katika lengo na matumizi halisi, si jina.

CCM ambayo inaibatiza rushwa kuwa ni takrima kinyume cha ahadi na maadili yake yenyewe ambayo yanasema “RUSHWA NI ADUI WA HAKI SITATOA WALA KUPOKEA RUSHWA” haiwezi leo kusema utoaji na upokeaji rushwa ni takrima.

CCM haitaweza kuepuka kuvunjika kutokana na dhambi ya kukiuka maadili, ahadi na kiapo chake yenyewe. CCM ambayo Bunge lake hutunga sheria na kiapo chake yenyewe.

CCM ambayo inaliachia Bunge lake kutunga sheria ya kuhalalisha rushwa kwa kuiita takrima na kuwaruhusu wana CCM viongozi kutumia fedha nyingi sana, haiwezi kuepuka hukumu ya dhambi ya kuruhusu kupitishwa na kutumika sheria ambayo ina udhalimu ndani yake- (anti people).

Vitendo hivi vinaifanya CCM ijiangamize yenyewe na kujikaanga kwa mafuta yake yenyewe. Watanzania wengi niliokutana nao wanaamini TAKRIMA ni RUSHWA, hawaitaki, ingawa wanaipokea na kuitumia kwa sababu sheria inaihalalisha.

Tabia ya kutoa na kupokea rushwa itafanya uchaguzi na uwakilishi wa wananchi katika vyama (na hasa CCM na Bunge) viamuliwe sio na wanachama wengi wa CCM walio wanyonge au raia wengi walio wanyonge, bali ufanywe na watu wachache wenye fedha nyingi wanaonunua kura za wanyonge na maskini, na kuwanyang’anya uhuru wao, kwa maslahi yao. Tukifika hapo CCM itakoma kuwa chama cha watu, chama cha wanyonge, chama cha ukombozi wa wengi wanyonge na maskini na chama cha HAKI na USAWA. CCM ya wanyonge ni lazima ifanye jitihada ya kweli na inayoonekana kupiga vita rushwa, CCM lazima ikatae kuonekana kama dalali mkuu wa kujibinafsisha na kusimamia biashara ya kuuza na kununua kura na kuhatarisha uhuru, amani na umoja wa taifa letu.

Katika mazingira haya ya CCM kushindwa kukemea vitendo vya rushwa vya viongozi kwenye ngazi ya taifa ya wagombea urais, CCM imejiweka mahali pabaya.

Itawezaje kupata nguvu na ujasiri (moral courage) wa kimaadili kukemea rushwa kwa wagombea ngazi za chini za ubunge, uwakilishi na udiwani bila kuonekana kuwa kuna unafiki katika chama chenyewe?

Lililofumbiwa macho wakati wa mchakato wa kugombea kuteuliwa kuwa mgombea urais na hapo awali wakati wa uchaguzi wa viongozi wa jumuiya za chama, haliwezi kukemewa wakati wa kugombea kuteuliwa ubunge, uwakilishi au udiwani.

Na kuacha, au kushindwa, kulikemea hilo katika ngazi hizi ambazo zimesambaa nchi nzima, ni sawa na kuacha “saratani ya rushwa” (cancer ya rushwa), izagae katika miili ya Watanzania wote.

Inawezekana tu kukemea maovu haya sasa na baadaye kama kabla ya kufanya hivyo chama kitajikosoa wazi wazi kwenye vikao vyake vya uongozi, vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kwa kufanya hivyo chama kitaheshimika. Madhara kwa nchi yetu hayatakuwa makubwa sana hili likifanyika.

Hili la rushwa lilianza mbali. Lilianza na uchaguzi wa Jumuiya za Chama, Vijana, Wanawake na Wazazi. Yaliyotokea wote tunayojua lakini tukayafumbia macho.

Dhambi ile ya kufumbia macho rushwa wakati huo imeendelea ikafikia kwenye nafasi ya kugombea urais. Haikukemewa. Sasa inaendelea kwenye ugombea ubunge, uwakilishi na udiwani.

Tusipowahi kujikosoa katika ngazi hii ambayo uongozi wake unakwenda mpaka kwenye wilaya na kata, matawi na vijiji, basi tutakuwa tumeachia “mdudu rushwa” atafune sio mti na matawi tu bali pamoja na mizizi yake. Likitokea hilo chama kitakuwa salama namna gani na viongozi wakuu wa Chama chetu watatuambia nini sisi wanachama?

Matumizi mabaya ya historia

Kuitumia vibaya historia na kurejesha ubaguzi Tanzania ni kasoro kubwa ya nne. Hoja zilizotumiwa kumjadili Ndugu Salim. A. Salim hazikuwa mbaya, ni hoja kama hoja zingine. Lakini zilistahili zitolewe na kujadiliwa kwa kuzingatia kwa makini sana kanuni za vikao vikuu vya CCM.

Maana hoja hizo si kwamba tu zilitolewa na viongozi wakubwa na wa siku nyingi wa CCM, lakini pia ni hoja nzito sana, zinazoweza kumfukuzisha au kumshtaki mwana- CCM mtuhumiwa katika chama, kusababisha anayezitoa afukuzwe katika chama na kushtakiwa asipoweza kuzitetea na kuzithibitisha.

Zinaweza pia kukisambaratisha chama maana hoja hizo zinatia doa uaminifu wa viongozi, zikiwa ni ushahidi kuwa viongozi hawaamini. Hoja nzito za namna hii zisipojadiliwa kwa makini zinaweza kuwaweka wananchi katika makundi mawili wana- CCM na daraja la kwanza kwenye haki zote, na wana- CCM wa daraja la pili wasio na haki au wenye sehemu tu ya haki.

Histori ya CCM inajulikana, kama vile historia ya vyama vyetu vya awali vya ASP na TANU inavyojulikana. Historia ya vyama vya upinzani wakati na baada ya Uhuru Tanzania Bara na Tanzania Visiwani inajulikana.

Dhuluma, viwango vya dhuluma na matokeo yote mabaya kwa raia wetu ya dhuluma zilizosimamiwa na kutendwa na wakoloni wa Kigeni (Waingereza, Waarabu n.k. nazo zinajulikana. Mapinduzi ya Januari 1964 kule Zanzibar na sababu zake na vyote vinajulikana. Wenzetu wa Zanzibar wamepata madhara makubwa sana kabla na baada ya mapinduzi hayo. Wamepoteza maisha ya wenzetu wengi. Hayo yote tunayajua.

Lakini baadhi yetu tunaamini mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa na lengo kuu la kuondoa (kufuta kabisa) dhuluma katika visiwa hivyo na kuleta haki na usawa kwa Wazanzibari wote kujali rangi zao, asili zao dini zao n.k.

Hayakuwa mapinduzi ya kuondoa tabaka moja la watu wadhalimu na kuweka tabaka jingine lenye lengo na tabia ya kudumisha dhuluma. Kwa imani hiyo CCM ilizaliwa (1977) ili kuendeleza jitihada za kuondoa dhuluma Tanzania Bara na visiwani.

Lengo la kuunganisha ASP na TANU, siyo kuwagawa watanzania, bali kutusaidia Watanzanai kuchanganyika, kujifunza kuishi pamoja kama ndugu na kusamehe mabaya yote ya nyuma tuliyotendeana hata kama hayawezi kusahaulika.

Jitihada zetu zitakuwa katika kuwarithisha watoto wetu na vizazi vijavyo kupitia kwao, mazuri yote tunayokubaliana kuyatenda. Baada ya mapinduzi na baada ya kuunda CCM viongozi wakuu au wakongwe wa CCM, na wanachama wa CCM, hawawezi kutaka kuendeleza dhuluma za wakoloni na tabia zao za ubaguzi. Kufanya hivyo ni kukiuka imani ya chama chetu, misingi yake, na ahadi zetu: “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja, nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko.”

Katika kikao cha uteuzi wa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, inajulikana sasa kwamba baadhi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu kutoka Zanzibar walitoa hoja kumhusu Ndugu Salim A. Salim, wakitaka zizingatiwe kwa makini kabla na wakati wa kupiga kura.

Hoja hizo zilimtuhumu Ndugu Salim A. Salim kwa mambo matatu: Aliwahi kuwa mwanachama wa Hizbu, yeye ni Mwarabu na alishiriki mauji ya Rais Abeid Aman Karume.

Narudia kusema kuwa waliozitoa hoja hizi hawajakosea lolote. Walitumia uhuru wao na haki yao ipasavyo. Wao walisema kweli yao ili wasiwe watu wa fitina kama CCM inavyotaka.

Waliwaeleza viongozi wenzao mbele ya Mwenyekiti wa CCM (Taifa), ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, sababu zao za kumkataa Ndugu yao Dk. Salim A. Salim, asifikiriwe, wala kuteuliwa kuwa mgombea wa urais.

Kwao urais ni nafasi nyeti na takatifu, isiyoweza kukabidhiwa kwa Mtanzania na mwana-CCM mwenye kasoro kama zile walizozitaja kuhusu Dk. Salim A. Salim. Walifanya hivyo waziwazi, hawakujificha au kumwendea Mwenyekiti wa Taifa kwa siri na mizengwe kumtaka asaidie kumuengua Dk. Salim. Naamini wajumbe hao walitaka ajenda hiyo ijadiliwe kwa makini.

Inavyojulina kwa baadhi ya viongozi wa watu waliofuatilia hoja hii ni kwamba hoja hiyo nzito haikujadiliwa, ilitolewa na kuungwa mkono na wajumbe wawili (ikiwa ni sahihi) wachache walioisemea ni wale waliosema tu kuwa haikuwasilishwa kwa mujibu wa kanuni na taratibu za vikao vya CCM.

Ikiwa kweli hoja hiyo nzito haikujadiliwa, sababu zake zipi? Hisia ya baadhi ya wajumbe zimejengeka kuwa labda Mwenyekiti alitaka Dk. Salim A. Salim asemwe vile alivyosemwa ili apunguziwe sifa na baadaye asiteuliwe kabisa.

Kwa sababu jina lake limechafuliwa. Lakini hoja ilitolewa wakati muafaka ikiwa ni ushahidi wa dhahiri kwamba bado wapo wana CCM wenzetu wenye mashaka na wenzao wenye maradhi ya kutowaamini wenzao kwa sababu tu ya historia, au asili na rangi yao.

Yalitakiwa majadilino na majibu yenye msimamo thabiti, wala si ya ugomvi, kutoka kwa mwenyekiti na wajumbe. Lakini sivyo ilivyotokea. Sasa tunajua kuwa karibu wajumbe wote waliduwaa na kunyamaza. Baadaye baadhi wameanza kulalamika nje ya kikao. Madhara ya jambo hili kwa CCM ni mabaya na makubwa kama si leo, basi kesho yanaweza kuwa mabaya zaidi hasa kwa vizazi vijavyo vya watoto wetu.

CCM ambayo imejenga tabia ya uwazi na ukweli, na kutobagua wanachama wake katika makundi ya rangi, ukabila, dini jinsia n.k. inawezaje leo kushindwa au kukataa kujadili agenda ya ubaguzi?

Kama agenda hii itaachwa bila kujadiliwa na kukemea pale ambapo inastahili, CCM itabakije kuwa chama cha wanachama wa rangi zote, dini zote, jinsia zote, na kuwa tunapofika kwenye suala la uongozi hakuna ubaguzi na matabaka katika Chama?

CCM itaepukaje dhana kuwa ina wenyewe ambao ni wanachama weusi na wanachama wa kuja ambao si weusi? Au CCM itaepukaje hisia ya kuwa ukijiunga na CCM kutokea vyama vingine basi unakuwa mwanachama wa daraja la pili na wale wanaotokana na TANU au ASP ndio wa daraja la kwanza ambao wanaostahili kuongoza na wengine ni kuongozwa tu? Nini muda au kipimo cha kuchunguzwa (probation) ya hawa wanaoingia CCM kutoka vyama vingine kabla hawajakubaliwa kuwa wa daraja la kwanza, miaka 10, 20, 50?

Ingekuwa vizuri kama hoja hii ingepewa nafasi stahili ikazungumzwa kwenye kikao na Dk. Salim A. Salim akarejeshwa ndani ya kikao kujitetea kama kanuni na taratibu za vikao vya CCM vya uteuzi zinavyoelekeza.

Tuhuma zake ni nzito mno, bado anastahili kuwa Mwana CCM bila kushitakiwa na kuhukumiwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM au ya nchi!! Hii ni kasoro kubwa ya kikao cha chama chetu.

Ni kasoro ya uongozi wa chama chetu, siyo ya mwenyekiti tu, bali wajumbe wote wa Halmashauri Kuu, akiwemo na Dk. Salim. Maana hadi sasa hawasilisha malalamiko au rufaa yake mbele ya CCM.

Lakini sina hakika kama halalamiki pembeni. Kama mwenyekiti aliona haifai hoja nzito kama hiyo ijadiliwe, wajumbe wengine wangedai ijadiliwe. Dk Salim yeye angedai zaidi, na hata kupeleka rufaa yake kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kupitia Mwenyekiti wa CCM Taifa au Katibu Mkuu.

Yote hayakufanyika, na huenda wapo wanaoomba Mungu apishie mbali yasitokee. Lakini chini chini yanajadiliwa yanazidi kujenga chuki; kuwagawa viongozi na kufifiza au kudhoofisha mshikamano na uongozi wa pamoja uenyekiti (the Institution of Chairmanship) unapungukiwa heshima yake na madaraka yake yanayotokana na uongozi badala ya utawala nayo yanadhoofishwa.

Nafasi ya viongozi wakuu wa CCM kukaa pamoja na kujadiliana kila jambo nyeti inatoweka au kutotumiwa kabisa. Viongozi wa siasa wanakwepana, kuoneana aibu na nguvu ya uongozi leo wa pamoja inapungua.

Na mwisho uwezo wa viongozi na wanachama wa CCM kuishi kwa amani umoja umoja na mshikamano unapungua polepole, hali hii inatoa nafasi kwa chama kudhoofika na siku moja kusambaratika kabisa.

CCM inaanza kuwa chama cha viongozi wasioaminiana na kuheshimiana bali wanaoogopana, kutishana kulalamikiana na kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa pamoja kwa kuzingatia katiba yao na katiba ya nchi yetu.

Hii ni kasoro kubwa, haiwezi kuachwa isizungumzwe na kutafutiwa ufumbuzi wa haraka, kabla ya ya uchaguzi wa Oktoba, 2005.

Watanzania siyo vipofu wala siyo viziwi, wanaona na kusikia jinsi CCM inavyovurugika na jinsi Viongozi wakuu wa CCM wasivyoaminiana. Bila kufanya hivyo ukweli na uwazi uko wapi, na bila kufanya hivyo, uhalali wa uongozi uko wapi?

Ujasiri wa uongozi uko wapi! Nani ataweza kusimamia marekebisho ya kasoro hizi nzito, kama siyo vikao vya chama chetu cha CCM, chini ya uenyekiti wako na kabla hujastaafu! "LEGACY" ya chama chetu na uongozi wake katika awamu ya tatu wakatawanyika huku wamenuniana na kutuhumiana na nini itakuwa legacy ya mwenyekiti wetu?

Yule aliyemaliza awamu yake akiwa amekiandaa chama chetu kusambaratika kwa kukosa uongozi wa pamoja unaozingatia katiba, kanuni na taratibu zote za chama.

Maana ndivyo ilivyo na ndivyo itakavyokuwa. Wana-CCM wakitaka kujua sababu za hali hii , watapewa majibu gani na nani atawajibu!

Siyo, haki kumwachia ndugu yetu Jakaya Kiwete chama cha aina hiyo na uongozi wa aina hiyo. Bora kasoro hizo nilizozitaja na zingine ambazo wengine wamekueleza zijadiliwe sasa na kufikia uamuzi wa jinsi ya kuziondosha mara moja, au baada ya uchaguzi mkuu.

Dhana ya uongozi na kuwajibika kwa pamoja

Chama Cha Mapinduzi kina mila na utaratibu wa kuheshimu uongozi wa pamoja. Na uongozi wa pamoja ni uongozi wa vikao amabavyo vinatoa nafasi sawa, kwa wajumbe wote, bila ubaguzi, kujadili kwa kina masuala yote ya Chama wakiongozwa na mwenyekiti. Katika vikao wajumbe wote wana haki sawa ya kuheshimiwa, kuaminiana na kutoa mawazo yao.

Mwenyekiti ni mjumbe kama wajumbe wengine, lakini ni mwenye dhamana ya nyongeza ya kuongoza vikao. Akipenda aogopwe na wale wanaomuonea haya katika vikao. Uhusiano wake na viongozi wenzake katika vikao hauwezi kufananishwa na ule wa vibarua na waajiri au mabwana na watumwa.

Ni vikao vya wajumbe walio sawa, tofauti yao ni katika mgawano wa madaraka na majukumu yanayotokana na madaraka yao.

Lakini ushahidi unaoanza kujitokeza sasa ni ule wa wajumbe kumuogopa na kumuonea haya Mwenyekiti wao kwa visingizio mbalimbali vikiwemo ukali wa mweneyekiti, au hulka yake ya kujitenga na kutotaka kusikiliza wengine.

Kikao cha kamati kuu ya halmashauri kuu ya taifa ni kikao caha uongozi na viongozi, hakiwezi kuwa gulio la viongozi wanaolalamika tu, kutokana na kuogopa au kumuonea mwenyekiti haya. Dhana ya uongozi wa pamoja haitoi nafasi ya Halamashari Kuu ya CCM.

Wajibu wao ni kudai na kutetea haki yao ya mbele yao. Maana dhana ya uwajibikaji inawahusu wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, kumtupia lawama Mwenyekiti peke yake ni dalili ya uongozi dhaifu, unaokosa upendo, ukweli na ujasiri. CCM inayo kasoro hii, hivi sasa katika vikao vyake vya uongozi.

Ndugu mwenyekiti, unisamehe kwa barua hii. Nimekuandikia yote yaliyomo katika moyo wangu kuhusu uongozi wa Chama chetu CCM, hatima yake na hatima ya taifa letu. Nia yangu ya kufanya hivyo ni njema kabisa.

Namna yangu ya kusema mambo ni ileile haijabadilika, natumia lugha yangu, na kusema yote yaliyomo moyoni mwangu kwa sababu nakuamini, naamini chama changu cha CCM kuwa ni chama cha haki, uwazi na ukweli, ambacho pia kinafuata katiba yake, kanuni na taratibu zote za uongozi na utendaji.

Umri wangu sasa miaka 67 na miezi 4. Mimi, kama wewe ni wazee sasa. Wajibu wetu si kulalamika au kufichana ukweli. Wala hatuna wajibu wa kufuga urafiki wa woga baina yetu. Nimekuwa mtendaji, na kiongozi wa ngazi nyingi za juu katika Serikali (nimestaafu baada ya kufanya kazi kama KATIBU MKUU na Katibu wa Rais;) Mkuu wa Mkoa, Mbunge (ex-official) mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa na Katibu wa CCM wa Mkoa.

Nimefanya kazi hizo zote chini ya Baba wa Taifa, Rais Mwinyi na wewe pia.

Sina tabia ya kulalamika, maana mimi bado ni kiongozi, ingawa nimestaafu. Nasema nilichonacho moyoni, maana ndiyo malezi yangu kutoka wa wazazi wangu, na chama chetu cha CCM.

Narudia tena kutoa maoni yangu kuwa tusijidanganye kuwa CCM ni chama salama kama tunaendelea kuliacha swala la RUSHWA kuwa ni agenda ya CCM.

Kama CCM haitafanya agenda ya kudumu vyama vingine vitadandia agenda hiyo na dunia itaendelea kutuyumbisha kuwa ni sehemu ya agenda ya utawala bora.

Tusijidanganye pia kuwa CCM itabaki chama salama ya agenda ya utawala bora. Tusijidanganye pia CCM itabaki chama salama kama kitaanza kuwa chama cha uabaguzi.

Tusijidanganye kuwa CCM itaendelea kuwa chama cha wanyonge na chama ambacho kinaungwa mkono na wengi.

Kama wanyonge wengi hawana kauli ya walau kuchagua viongozi wao katika chama wala katika vyombo vya uwakilishi serikalini, bila matumizi ya fedha, fedha nyingi na ushawishi wa wenye fedha, kitakuwa si chama chao, ni cha wenye fedha.

Pendekezo

Msimamo wako ni wa uwazi na ukweli, CCM inayo maadili na utamaduni wa kujikosoa. Kabla ya vikao vua uteuzi vya CCM wewe mwenyewe na katibu mkuu wa CCM, nimesema kwa msisitizo mkubwa kuhusu umuhimu wa kuzingatia katiba ya CCM, kanuni na taratibu za CCM, katika kujiandaa kwa uchaguzi wa Oktoba. Umewahi kuwatuhumu viongozi wa CCM kwa kukosa ujasiri wa kujadili maovu ya CCM na viongozi wake, katika ngazi zao za uongozi. Ukiwauliza ujasiri wao uko wapi!

Nakuomba sasa utumie hizo sifa zako zote, uitishe kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya Taifa ili kujadili hali hii mbaya ya ccm kubinafsishwa na wagombea wanaotumia fedha nyingi zisizojulikana zinatoka wapi kuwanunua wapiga kura na kura zao.

Unaweza pia kuwakaribisha baadhi ya wana CCM, na watu wengine wa busara, kuhudhuria kikao hicho na kutoa mchango wao wa mawazo. Wote wajilipie maana wengi wanazo fedha.

Lengo liwe kutathmini hali halisi ya CCM na viongozi wake, kwa kuzingatia maadili ya Chama chao na taifa na kujikosoa ikibidi. Heshima ya CCM itarejea nawe utamaliza kipindi chako cha urais bila kucha fua jina lako na sifa zako nzuri na nyingi na kufifiza matokeo ya kazi nzuri uliyoifanya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wako.

Hiki hakitakuwa kikao cha kutafuta wachawi ,kutafutana au kutuhumiana. Ni kikao cha viongozi na uongozi, wenye nia njema, wenye ujasiri wa kutosha kukubali kuwa yapo matatizo na kukubali kutathmini hali halisi ya CCM iliyotufikisha hapa tulipo leo.

Mheshimiwa Rais narudia kuomba radhi kwa lugha siyo yale niliyoyasema kwako. Hayana siri, hivyo nimeyagawa kwa wajumbe wengine wa Kamati Kuu ya CCM na wenyeviti wa CCM Mkoa kwa sababu karibu wote niliopata nafasi ya kusema nao wanayafahamu na labda wanaona haya kuyasema kwako au kuyaanzisha ili yazungumzwe.

Nakuomba sana usaidiane nao kuirudishia CCM heshima yake, nguvu zake na utukufu wake.

Taifa letu bado ni changa sana, Watanzania bado ni maskini mno, hawajaweza kujenga misingi imara ya utawala bora na kujenga vyombo imara vya utawala wao ( Institutional Capacity): Wanaitegemea sana CCM wanawategemea sana viongozi wakuu wa CCM. Jitahidini kwa pamoja, msiwaangushe Watanzania wenzenu.

Nduguyo mtiifu na Mwana – CCM mwenzako,

Toka Tanzania Daima.

1 comment:

Anonymous said...

MZEEE KASEMA UKWELI HAKUNA FITINA LAKINI MAGAMBA YANAELEWA HAYA????