KIKWETE KUMRITHI NYERERE YANGA?
Na Mwandishi wetuWAKATI zoezi la utoaji kadi mpya za Klabu ya Yanga ya Dar es Salaam likiendelea shauku kubwa ya Wanayanga ni kutaka kuona kama Rais Jakaya Kikwete, atajitokeza kuchukua fomu hizo na baadaye Kadi ya uanachama.
Yanga ambayo ilianza kuzigawa fomu hizo za maombi ya uanachama zipatazo 30,000, Jumatatu Oktoba 22, ikianza na jiji la Dar es Salaam, imezuia fomu kuanzia namba moja hadi 100, ambazo zitauzwa kwa viongozi.....
Mamia ya wanachama wa Yanga, tangu kutangazwa kwa uamuzi wa kuziweka fomu namba moja hadi 100 kwa ajili ya viongozi, wamekuwa wakitaka kujua na kuona ni viongozi gani wakuu wa kiserikali watakaojitokeza kuchukua fomu hizo.
Wanachama hao wamekuwa wakitamba kuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere ndiye mwanachama wa Yanga aliyetunukiwa kadi namba 01 ya Klabu hiyo.
Kutokana na hilo, wanachama na wanazi wa klabu hiyo kongwe zaidi nchini, hususan katika medani ya soka, wanataka kuthibitisha iwapo tetesi zisemwazo kuwa Rais Kikwete naye ni memba wa Jangwani.
“Tunasikia kuwa Mzee Nyerere alikuwa mwanachama namba 01, sasa tunasubiri kuona kama mheshimiwa Rais, ambaye naye watu wanadai kuwa ni mwenzetu atajitokeza kuchukua Kadi, kwani tumesikia kuwa viongozi wanataka kumpa kadi hiyo namba moja.
“Kama kweli atajitokeza kuchukua kadi tutamsindikiza na matarumbeta kwani ni heshima kubwa kiongozi wa nchi kuwa mwanachama wa klabu yetu,” alisema mmoja wa wazee wa Yanga ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Wanachama hao wanasubiri pia kuona ni viongozi gani wenye nyadhifa za juu serikalini watakaojitokeza hadharani na kutangaza kuchukua fomu hizo, za kuomba uanachama wa Yanga.
Hilo linatokana na ukweli kwamba baada ya kuanzishwa kwa kampuni ya Yanga mwaka 2003, baadhi ya mawaziri akiwemo Naibu Waziri wa Elimu Utamaduni na Michezo enzi hizo, Mudhihir Mohammed Mudhihir, kujitokeza hadharani na kutamka yeye ni Yanga damu.
Katika kuthibitisha hilo Mudhihir aliwaongoza viongozi kadhaa kuchukua Kadi ya Useneta wa Yanga, ingawa wengi kati yao hawakutaka kujitangaza hadharani juu ya ukereketwa wake wao kwa Yanga.
Zoezi hilo la utoaji fomu za kuombea Kadi za uanachama kwa mkoa wa Dar es Salaam litakamilika kesho, na baada ya hapo litahamia katika mikoa mingine ya Tanzania bara na visiwani.
No comments:
Post a Comment