Saturday, November 24, 2007


‘Asilimia 40 ya vifaa vya umeme vya nje ni bandia’

Nashon Kennedy, Mwanza
HabariLeo; Saturday,November 24, 2007 @00:03

ASILIMIA 40 ya vifaa vyote vya umeme vinavyoingizwa nchini ni bandia na hutumiwa na watumiaji bila ya wao kuzitambua bidhaa hizo.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Bidhaa Bandia kutoka Tume ya Ushindani nchini, John Mponela, alipowasilisha mada juu ya utaratibu wa kisheria wa mapambano dhidi ya bidhaa bandia zinazoingizwa nchini katika semina ya siku moja iliyowashirikisha washiriki kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, watu binafsi na wadau mbalimbali.

Mponela alisema bidhaa hizo bandia zimeshamiri zaidi kwenye vifaa vya ujenzi, umeme, vifaa vya elektroniki, dawa, viberiti, dawa za viatu na zile za meno.

Alisema sababu kubwa ya uingizaji wa bidhaa hizo ni pamoja na ulegezaji wa masharti ya biashara ulioanza miaka ya 1980 na kuwapo kwa suala zima la utandawazi.

Utafiti uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Marekani (ICR) unakisia kuwa kwa Tanzania pekee, Kampuni ya Sigara (TCC) inapoteza karibu asilimia 40 ya mapato yake kutokana na bidhaa bandia za sigara.

“ICR vile vile inakadiria kuwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki zinapoteza karibu dola za Marekani milioni 20 kila mwaka kama mapato ya kodi kwa bidhaa bandia,” alisema Mponela.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Godfrey Mkocha, aliwaomba watumiaji wa bidhaa zinazoingia nchini wahakikishe ni zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria na kwamba kila mwananchi anayo haki ya kuisaidia tume hiyo kulinda mazingira ya uchumi kupunguza gharama na kuongeza ubora wa huduma nchini.

Aliwatahadharisha wananchi kutonunua bidhaa bandia kwenye maeneo yao akisema kuwa zina athari kwa afya zao na zitawaathiri katika uchumi.


No comments: