Msekwa Makamu Mwenyekiti CCM.
*Arithi mikoba ya Malecela ambaye amestaafu
*Apewa ujumbe wa kudumu katika CCM na NEC
*CCM kuandaa tafrija kubwa ya kumpongeza
*Apewa ujumbe wa kudumu katika CCM na NEC
*CCM kuandaa tafrija kubwa ya kumpongeza
Na John Daniel, Dodoma
HALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), imepitisha jina la aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Bw. Pius Msekwa, kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, kumrithi Bw. John Malecela, aliyekalia nafasi hiyo kwa miaka 15.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Bw. Pius Msekwa,
akizungumza na waandishi wa habari jana,
muda mfupi baada ya kupata wadhifa huo
Dodoma jana. (Picha na Richard Mwaikenda)
akizungumza na waandishi wa habari jana,
muda mfupi baada ya kupata wadhifa huo
Dodoma jana. (Picha na Richard Mwaikenda)
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, jina la anayefaa kushika nafasi hiyo hupendekezwa na Mwenyekiti wa chama na kisha kuwasilishwa kwenye Kamati Kuu na ikisharidhia, linawasilishwa NEC nayo ikiafiki huwasilishwa rasmi katika Mkutano Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Yusufu Makamba, alisema Kamati Kuu na NEC ziliridhia uteuzi huo na kwamba Bw. Malecela ameamua kustaafu.
"Kama mnavyojua, kuwa Mheshimiwa Malecela amekuwa Makamu Mwenyekiti kwa miaka 15 sasa, hivyo ameamua kujiuzulu nafasi hiyo, NEC imeamua kuwa Bw. Malecela atakuwa mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa kutambua na kuenzi mchango wake katika chama,"alisema Bw. Makamba.
Alisema CCM itaandaa tafrija maalumu ya kumpongeza kiongozi huyo ambaye bado anaonekana kuwa na nguvu za kutosha za ushawishi ndani ya CCM.
Pia alisema NEC imemteua Bibi Hadija Faraja, kuwa Katibu wa CCM Unguja Kaskazini.
Baadhi ya wajumbe wa NEC waliozungumza na Majira jana huku wakikataa majina yao kutajwa, walidai kuwa kuteuliwa kwa Bw. Msekwa kushika nafasi hiyo ni mojawapo ya njia ya kumaliza makundi ndani ya CCM.
"Unajua huyu mzee ana uzoefu mkubwa wa kuwaunganisha watu, hivyo kuwa Makamu wetu kutatusaidia sana kwani hata matabaka yaliyokuwa yanaanza kuonekana anaweza kuyamaliza kabisa tofauti na wengine ...wengine walikuwa na upande, lakini huyu anaonekana kuwa katikati, hapa Mwenyekiti amepatia," alisema moja wa wajumbe wa NEC ambaye pia ni mgombea.
Bw. Msekwa licha ya kuwa kiongozi wa muda mrefu ndani ya TANU na hatimaye CCM, alishirikiana na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya ASP, marehemu Thabit Kombo wa Zanzibar kuandaa Katiba ya CCM ambayo ilizaliwa mwaka 1977 baada ya TANU na ASP kuungana.
Pia alikuwa ndiye Katibu Mtendaji wa Kwanza na CCM na kisha kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi mwaka 2005, mbali na kuwa Mbunge wa Ukerewe.
No comments:
Post a Comment