Friday, November 02, 2007
Na Emmanuel Lengwa, Dodoma.
Wavulana watakaotiwa hatiani na mahakama kwa kosa la kuwabaka watoto wenzao wataanza kupewa adhabu ya kucharazwa bakora.
Hayo yamesemwa Bungeni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Johnson Mwanyika, ameyasema hayo wakati akiwasilisha Muswada wa Sheria ya kufanya marekebisho mbalimbali.
Akasema Bw. Mwanyika kuwa muswada huo unatarajiwa kuifanyia marekebisho Sheria ya Makosa ya jinai, kanuni ya adhabu sura ya 16 ambayo awali ilikuwa ikitoa adhabu bila kuzingatia umri wa mkosaji.
Akasema katika Sheria ya Kujaamiiana, watu waliokuwa wakipatikana na hatia walikuwa wakiadhibiwa kifungo cha miaka 30 jela bila kujali umri wa mkosaji.
Akasema kuwa sheria hiyo ilikuwa ikiwanyima watoto haki zao nyingine za msingi, kama vile elimu, na kujiendeleza kimaisha.
Akasema Mwanasheria huyo kuwa muswada huo ukipitishwa kuwa sheria, watoto watakaokuwa wanatiwa hatiani wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko na kuachiwa huru ili wapate haki zao nyingine za msingi.
Akichangia muswada huo, Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni katika masuala ya Katiba na Sheria, Bi. Fatma Magimbi, akasema wakati sheria hiyo ikiwapunguzia adhabu watoto, iongezewe nguvu kwa watu wazima wanaotiwa hatiani kwa kuwabaka watoto.
Mheshimiwa Magimbi ambaye pia ni Mbunge wa Chake Chake, akapendekeza kuwa wanaume na wanawake watakaotiwa hatiani kwa kuwabaka watoto wahasiwe.
Hata hivyo Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Hurrison Mwakyembe akakosoa neno Ubakaji kutumika kwa watoto kwa vile litasababisha mkanganyiko kwenye sheria nyingine.
Dk. Mwakyembe akafafanua kuwa Ubakaji unakuja pale tu mtu anapolazimishwa kufanya tendo la ngono na kuwa ikiwa muhusika ameridhia tendo hilo hakuna ubakaji.
Akasema kuwapo kwa neno hilo kutapingana na sheria nyingine zinazosema kuwa mtoto mdogo hawezi kuridhia ngono na hivyo mtu anayefanya naye mapenzi huchukuliwa moja kwa moja kuwa ni mbakaji.
Dk. Mwakyembe akasema neno hilo libadilishwe na kuwekwa lingine ambalo halitasababisha mkanganyiko huo.
Akahitimisha mchango wake kwa kuwavunja mbavu waheshimiwa wabunge kwa kumtaka Mheshimiwa Magimbi kulieleza Bunge namna mwanamke anavyoweza kuhasiwa ikiwa atakutwa na hatia ya kubaka mtoto.
Chanzo: Gazeti la Alasiri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment