Tuesday, November 06, 2007

Rais Jakaya Kikwete. Picha kutoka www.jakayakikwete.com


Kauli za Kikwete kuiponza serikali.

na Peter Nyanje na Christopher Nyenyembe.

KAULI kuhusu kuunda kamati ya kupitia mikataba pamoja na sheria za madini, iliyotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Rais Jakaya Kikwete, kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa nane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeelezwa kuwa itawasha moto mpya utakaoitia matatani zaidi serikali anayoiongoza pamoja na chama chake.

Watu mbalimbali walilieleza gazeti hili jana kuwa, kauli hiyo kimsingi inathibitisha kuwa kuna matatizo katika mikataba ya madini na sheria yake, hivyo kufuta kabisha utetezi uliowahi kutolewa na baadhi ya watendaji wa serikali, wakiwamo mawaziri, kuhusu mikataba ya madini.

"Rais anaonekana amezungumza kitu tofauti kabisa na wasaidizi wake… tulizoea kusikia kutoka kwa watendaji wa serikali kwamba hakuna matatizo katika mikataba ya madini, huu wa Buzwagi ndio uliokuwa ukitolewa mfano… sasa kama hakuna matatizo, kwa nini rais atake kuunda tume kuipitia upya?" alihoji mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini.

Msimamo huo wa Kikwete, unaweza kusababisha baadhi ya watendaji wa serikali waliotumwa kuitetea mikataba ya serikali kujiona wamegeukwa, na hivyo kupunguza imani yao kwa wakuu wao.

"Sasa hivi watakapotumwa kwenda mikoani kutetea kitu fulani, wanaweza kuwa na wasiwasi kuwa wasije wakatetea na kesho bosi wao akaja kusema kitu tofauti na walivyokuwa wakitetea wao, pia wananchi wataanza kutowaamini… waliutetea sana mkataba wa Buzwagi na mingine ya madini, lakini bosi wao kawaumbua hadharani," aliongeza.

Mhadhiri huyo alionyesha wasiwasi wake iwapo mshikamano ndani ya serikali na chama utaendelea kuimarika, hasa baada ya hotuba hiyo kuonyesha kuwa kilichokuwa kikisemwa na baadhi yao si sahihi.

"Haiwezekani hata mara moja uunde kamati kupitia mkataba ambao ni safi, nasisitiza hilo haliwezekani, alichofanya Kikwete ni kuwaumbua wenzake," alisisitiza.

Aidha, baadhi ya wapinzani wamemuonya Rais Kikwete na kumweleza asitarajie kuwa uamuzi wake wa kuwahusisha katika kamati ya kupitia mikataba na sheria za madini utawanyamazisha.

"Kauli hii ya Kikwete isiwapumbaze Watanzania na kuzima mjadala wa kitaifa unaoendelea hivi sasa kuhusu hatma ya madini yetu na rasilimali nyingine za taifa," alisema John Mnyika, Mkurugenzi wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alipozungumza na gazeti hili.

"Wapinzani hatutanyamaza, wala mjadala kuhusu rasilimali madini hautazimika kwa sababu kauli ya Kikwete imedhihirisha wazi hoja ambazo wapinzani tumekuwa tukisimamia, zilikuwa ni sahihi tofauti na baadhi ya mawaziri na viongozi wengine wa chama chake walivyokuwa wakipita mikoani kubeza," alisema Mnyika.

Aidha, mchambuzi mwingine alisema kuwa kauli hii ya Rais Kikwete kukiriri mapungufu, inadhihirisha wazi umuhimu wa upinzani katika taifa, kwani hoja kuhusu matatizo katika sekta ya madini iliibuliwa na wapinzani.

Kwa upande wake, akionekana kuunga mkono hoja hiyo, Mnyika alisema: "Kauli ya Kikwete inadhihirisha umakini wa hoja aliyoiibua Mbunge Zitto Kabwe, ya kutaka kuundwa kwa kamati teule, wabunge wa CCM wakaikataa, lakini leo mwenyekiti wao wa chama anaeleza wazi nia yake ya kuhakikisha inaundwa kamati inayojumuisha makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo wasomi na wapinzani."

Akifafanua kuhusu wapinzani kuendelea kulivalia njuga suala hilo, Mnyika alisema kuwa kuundwa kwa kamati ni suala moja tu, na la msingi ni kuwa maoni yatakayotokana na kamati hiyo kufanyiwa kazi ipasavyo.

"Uzoefu unaonyesha zipo kamati za kiserikali ambazo ziliundwa, lakini zikatoka na misimamo ya kiserikali badala ya kuwa na misimamo huru itokanayo na maoni ya wananchi walio wengi," alisema na kuongeza:

"Pia zipo kamati nyingi ambazo zimewahi kuundwa huko nyuma na kutoka na maoni mazuri, lakini yakaishia kwenye makabati. Kwa mfano, katika sekta hii hii ya madini zipo tume zilizowahi kuundwa mathalani Tume ya Kipokola ambayo ilikuja na maoni mazuri tu, lakini sehemu kubwa hayajatekelezwa."

Mnyika alisema kuwa kikubwa kinachokosekana ni dhamira ya kisiasa ya kutekeleza maoni ya wananchi na hilo linadhihirishwa na Rais Kikwete mwenyewe aliyetoa ahadi nyingi Desemba 2005, alipozindua Bunge, lakini leo takribani miaka miwili imekaribia bado mabadiliko ya kisheria hayajafanyika, pamoja na hoja hii kuwemo tayari kwenye ripoti za kamati mbalimbali.

"Rais Kikwete anazungumza kwamba kamati hii itatumwa nje ya nchi kwenda kujifunza zaidi, huku ni kuendelea kutumia muda zaidi na fedha za walipa kodi na kuchelewesha kuchukua hatua katika jambo ambalo linafahamika tayari.

"Wataalamu wa Tanzania wenye ujuzi na masuala ya madini pamoja na wanasiasa wenye maono katika sekta hii wapo tayari na wengine wameshatoa maoni yao, vipi hatua zisichukuliwe?" alisema na kuhoji.

Aidha, imeelezwa kuwa hakuna haja ya kamati hiyo kwenda nje ya nchi kujifunza kama ilivyoelezwa na Rais Kikwete, kwani nchini wapo wataalamu wa kutosha kutoa ushauri ambao ukifuatwa, nchi itanufaika na rasilimali zake.

Suala kwamba kauli za viongozi wa juu zinaweza kusababisha mtafaruku katika chama na serikali, limeanza kujitokeza pale baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walipoelezea kukerwa pia na tabia ya Katibu Mkuu wa chama hicho taifa, Yusuph Makamba ya kuwasimanga hadharani viongozi wa kambi ya upinzani.

Makamba alitoa kauli hizo za kejeli dhidi ya wapinzani juzi, alipotakiwa kuwasilisha taarifa ya chama hicho katika kipindi cha miaka mitano ya kazi (2002 hadi 2007) na mwenyekiti wake, lakini yeye aliutumia sehemu ya muda huo kuwakejeli wapinzani.

Baadhi ya wanachama waliozungumza na gazeti hili, walionya kuwa tabia ya kuendekeza siasa, hata kwenye masuala nyeti na muhimu kwa nchi kama hoja zinazotolewa na wapinzani zinavyoonyesha, kunaweza kukigharimu chama hicho.

Mjumbe mmoja alisema inasikitisha zaidi pale kauli kama hizo zinapotolewa katika mikutano ambayo baadhi ya viongozi wa upinzani wanahudhuria baada ya kupata mialiko rasmi.

"Inaonyesha tumewaita ili tuwakejeli… lakini hili si lengo letu, ukiisikiliza na kuichambua hotuba ya mwenyekiti, utabaini kuwa anaheshimu hoja zinazotolewa na wapinzani, na mara zote amekuwa akisisitiza kuwa wapinzani si wa kubezwa… tunamshangaa sana katibu wetu," alisema mjumbe huyo kutoka moja ya mikoa iliyo katika Nyanda za Juu Kusini.

Mjumbe mwingine alisema kuwa licha ya Makamba kuonekana kuwa anawafurahisha wajumbe wa mkutano huo, wengi walikwazwa na maneno hayo ambayo hayaonyeshi ukomavu wa kisiasa na kujenga demokrasia ya kweli katika mfumo wa vyama vingi vya siasa na hulka ya kuvumiliana na kuheshimiana, huku CCM yenyewe ikilalamika kuwa inasakamwa na upinzani.

"Ulifika wakati nilitaka ninyooshe mkono kumuomba Mwenyekiti Kikwete niulize swali kuhusu kero hizo, lakini jirani yangu alinizuia nisifanye hivyo, naomba muandike kuwa Makamba hakuwatendea haki wapinzani walioalikwa, hiyo si demokrasia," alisema kada huyo wa CCM.

John Cheyo, ni mmoja wa viongozi wa upinzani ambaye alihudhuria mkutano huo na aliipongeza hotuba ya Rais Kikwete, lakini anakwazwa na tabia ya Makamba ya kuwabeza wapinzani kila anaposimama kwenye majukwaa kuhutubia tofauti na maneno ya busara yanayotolewa na Mwenyekiti wake.

Kutoka Tanzania Daima.


No comments: