Thursday, November 08, 2007


Tuhuma dhidi ya TAKUKURU mitandaoni zichunguzwe.

JUZI gazeti hili liliandika habari kuhusiana na baadhi ya wananchi kulalamikia tabia iliyojitokeza hivi sasa miongoni mwa watu, ya matumizi hasi ya mtandao wa intaneti kwa kutumia ujumbe wenye kashfa na matusi dhidi ya viongozi au taasisi mbalimbali za kijamii.

Wananchi hao pamoja na malalamiko yao, walisema hayo si matumizi mazuri na ni kinyume na nia hasa ya kuwapo kwa huduma ya mtandao wa intaneti katika jamii, kwamba badala ya kuweka ujumbe ambao unaelimisha jamii, hivi sasa hutumika kama chombo cha kueneza uongo na chuki katika jamii.

Baadhi ya watu maarufu wakiwamo wasanii hivi sasa wamekuwa wakibadilishiwa maumbile yao na miili iliyo uchi kubandikwa sura zao na kuonekana kuwa wanapiga picha za uchi na kuzisambaza ndani na nje ya nchi kwa nia ya kujipatia kipato.

Hali hiyo hivi karibuni iliingia katika medani ya siasa, ambapo watu wasiojulikana wamekuwa wakisambaza ujumbe wa kueleza kile wanachokiita ni ufisadi na uchafu unaofanywa na baadhi ya viongozi wa taasisi mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa vya Upinzani na Tawala.

Maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo ni viongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), tasnia ya utalii, madini na biashara; kwa kinachotaka kuenezwa kuwa maeneo hayo yananuka kutokana na ubadhirifu usio na kizuizi.

Nia ya ujumbe huo ni kutaka kuifahamisha jamii kuwa viongozi wa maeneo hayo na hasa TAKUKURU hawafai na wanastahili kuondolewa kwa madai kuwa wanashirikiana na wafanyabiashara wachafu tena wakiwamo wageni katika 'kuiuza' nchi na maliasili zake.

Sisi tunaamini kuwa Serikali imeliona hili na inajua ni yapi madhara yake huko tuendako na hasa kama yanayosemwa humo hayatakuwa na ukweli; hivyo tunachotaka ni kuishauri ichukue hatua madhubuti za kuchunguza tuhuma hizo na kuzipatia ufumbuzi.

Ni kwa kufanya hivyo tu ndipo itakapobaini ukweli na uhalisia wa mambo, ili kama yanayosemwa yana ukweli, basi watuhumiwa wachunguzwe na kuchukuliwa hatua za kisheria na kama hayana ukweli, wanaoeneza uongo nao wachukuliwe hatua ili mtandao wa intaneti uwe mahali pa kujifunza na si kuchafuana au kuzushiana.

Tunasema hivyo, tukiamini kuwa TAKUKURU ni chombo muhimu chenye kustahili heshima kinachotegemewa na jamii katika kupambana na ufisadi na rushwa nchini, sasa kama nacho hakitaaminiwa na wananchi kutokana tu na ujumbe katika mtandao, basi litakuwa ni jambo la hatari sana.

Kutoaminiwa kwa TAKUKURU kwa madai kwamba uongozi wake una kasoro, ni sawa pia na kutoaminiwa kwa juhudi za Rais Jakaya Kikwete na Serikali yake katika mapambano dhidi ya rushwa ambayo yalishaanza kujionesha hata ndani ya chama chake cha CCM ambacho yeye ni Mwenyekiti.

1 comment:

Anonymous said...

Mtandao unasaidia kuondoa ububu uliokuwepo miongoni mwa Watanzania. Mtandao ni njia nzuri ya kukemea maovu kama ufisadi, uzinzi nk yaliyopo katika jamii yetu. Ni kweli wapo wanaotumia vibaya uhuru huo kama ilivyo kwenye magazeti na vyombo vingine. Hata hivyo si vema kuhukumu habari kwa upendeleo tu bila hoja/Uhakika.