Monday, November 26, 2007

Watu weusi tuna akili ndogo?


**********************

na Padri Privatus Karugendo.

JAMES Watson, mwanasayansi maarufu sana duniani na mshindi wa nishani ya Nobel katika tiba mwaka 1962, ameleta mjadala mkubwa baada ya kudai kwamba mtu mweusi ana akili ndogo kuliko mtu mweupe. Kauli yake hiyo imeshikiwa bango na wapinzani wa ubaguzi wa rangi kwa kuwa inamdhalilisha mtu mweusi.

Huyu si mtu wa kwanza kusema hivyo, tofauti ni kwamba yeye ameisemea kisayansi zaidi. Siku za nyuma waziri mkuu mmoja wa Japan alipata kusema maneno kama hayo kwamba anatilia shaka uwezo wa mtu mweusi. Waziri mwingine wa Japan na yeye alishanukuliwa kusema hivyo hivyo. Wote baadaye waliomba radhi lakini ujumbe ulifika.

Chika Onyeani katika kitabu chake cha Capitalist Nigger naye anashangaa ni kwa nini Mwafrika atukanwe namna hiyo na mawaziri wa Japan lakini bado waendelee kununua bidhaa toka Japan. Anaelezea pia kwamba jamii yote ya watu weusi inafanana kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano ukikutana na Mmarekani mweusi aliyezaliwa na kukulia Marekani au Carribean au Afrika kwenyewe, bado wana tabia zile zile ambazo zinatia shaka kama kweli akili za Waafrika si ndogo kwa kiasi fulani.

Ukianza kuangalia matokeo mbalimbali yanayotokea Afrika, kuanzia enzi za miaka ya nyuma, unaanza kuwa na wasiwasi kuhusu hali na uelewa wa mtu mweusi. Historia inatuambia kwamba, hadi karne ya 16 kiwango cha maendeleo kati ya Ulaya na Afrika kilikuwa sawa.

Tunaambiwa pia kwamba miaka ya 1960 baadhi ya nchi za Kiafrika zilikuwa mbele kimaendeleo au katika usawa mmoja na nchi za Asia ambazo leo ziko mbali kimaendeleo. Bado unajiuliza ni wapi kwenye matatizo? Kwa nini Waafrika waachwe nyuma kila leo?

Inavyoelekea ni kwamba bara la Afrika linakuwa kama kigezo kizuri cha kupima maendeleo na mabara mengine. Ripoti za umasikini duniani zinaonyesha kwamba umasikini duniani umepungua kwa kiasi kikubwa lakini kwa Afrika unaonyesha kuongezeka. Mbaya zaidi hakuna ishara ya watu hao kutoka katika utando huo wa umasikini walikonasa kabisa.

Idadi ya watu waliopungua umasikini kidunia unatokana na kukua kwa uchumi wa China na India, nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Kwa hivyo, uwezo wao wa kupunguzia watu wao umasikini unachangia takwimu za kidunia zionekane nzuri lakini kwa Afrika hakuna mabadiliko mazuri.

Ukipima baadhi ya kauli za hawa tunaowaita wabaguzi utagundua kuna ujumbe wanawasilisha. Kama tukichukulia Tanzania kama mwakilishi wa Waafrika, tunaweza tukajadili baadhi ya hoja na kujipima ni kweli tuna akili ndogo kijenetiki au mazingira yetu yanatufanya tuwe na uwezo mdogo wa kutumia akili zetu au tujiulize ni wapi tumeteleza?

Tanzania hii ina rasilimali nyingi sana lakini bado hatujaweza kufika popote pa maana. Tunasaini mikataba ya hovyo kabisa ambayo inampa mgeni mamlaka ya kuchukua rasilimali jinsi anavyotaka huku wenyeji tukibaki hoi kabisa. Tuna mapori ya kutosha na mito na maziwa ya kutosha lakini bado tunaagiza chakula nje ya nchi.

Tuna watu wanajilundikia mabilioni ya fedha benki huku watu wa kijijini kwake hawana maji ya kunywa. Kuna watu wananunua samani za mabilioni ya Shilingi kwenye nyumba walizojengewa na Serikali wakati ambapo Shule ya Sekondari ya Azania, iliyopo katikati ya jiji kuu la nchi, ina wastani wa tundu moja la choo kwa wanafunzi 300!

Shule karibu zote mpya zilizojengwa, kuanzia za msingi hadi za sekondari, zina uhaba mkubwa wa vyoo. Hivi ni vitu vya msingi kabisa lakini bado hatujaweza kuvitatua.

Bado tunazipa likizo ya kodi kampuni kubwa huku tukifuatilia vikodi vidogo vidogo vya wafanyabiashara wadogo au hata wachuuzi. Kampuni kubwa zinaruhusiwa kubeba hasara na kuipeleka kwenye mahesabu ya mwaka ujao kwa miaka kadhaa lakini hiyo hiyo kampuni inayopata hasara inaendelea kufanya biashara!

Sasa hivi tunasifiwa kwa kuweza kufuatilia kodi kwenye biashara ndogo ndogo huku tukiwa hatujafanya lolote la maana kwenye kodi za makampuni makubwa. Uwezo wa Serikali wa ukusanyaji hupimwa na kuongezeka kwa kodi za makampuni makubwa (Corporate Tax) na si kuongezeka kwa kodi za mapato zinazotokana na kuajiri watu wachache.

Ni lazima tukae chini tujiulize: Kunani katika akili zetu? Tunavuna madini ya Tanzanite lakini hatuwezi kuyauza. Tunasema tuna mafuta lakini tukitaka kuyachimba tunamwita Mzungu, japokuwa tumekuwa tukizalisha wahandisi na wanajiolojia kila mwaka. Lazima tujiulize kama elimu yetu ina mushkeli au la!

Sasa hivi tunajigamba kuwa na vyuo vikuu karibia 30 lakini bado tunaagiza vijiti vya kuchokonolea meno kutoka Malaysia. Ni lazima tujiulize tulipoteleza. Ni lazima wakati mwingine tujiulize kama kweli hatuna mushkeli kwenye akili zetu.

Maamuzi yenye maslahi ya taifa yanachukua muda mrefu kuchukuliwa. Wananchi wamekuwa wakipigia kelele suala la Richmond lakini imechukua miezi kadhaa kuchukua uamuzi wa kulichunguza. Kampuni iliyoshindwa kazi.

Katika hali ya kawaida, ilibidi maamuzi ya haraka yachukuliwe na taarifa ipatikane ili wananchi waondoe hisia mbovu. Wapi? Imechukua miezi ndio maamuzi yanatoka. Ni dhahiri mazingira haya yataifanya hata taarifa yake itiliwe shaka.

Maamuzi yenye maslahi ya taifa yanatakiwa yachukuliwe mapema ili kusafisha hisia mbovu. Wenzetu wanaosemwa kuwa na akili kuzidi sisi leo wameweza kushughulikia mambo yenye maslahi ya taifa na kuondoa umimi kwanza. Ni lazima tujitathimini na kujiuliza kama kweli tuko sawa na wengine.

Kwenye makala yangu ya juma lililopita, nilitoa hoja kwamba tunajipima kwa viongozi wetu.Katika hali ya kawaida kiongozi wa watu maskini ni lazima aishi maisha yanayofanana na watu wake; maisha ya kimaskini. Lakini kama kiongozi wa watu maskini anaishi kwenye utajiri unaopindukia, ni lazima kuna kasoro.

Magari zaidi ya 30 yenye thamani ya Shilingi milioni 60 kila mmoja, kupita katika vijiji vya watu maskini kwa kisingizio cha kukagua maendeleo, ni jambo la kuleta mashaka kama kweli hatujateleza mahali au kuzua wasiwasi juu ya ubora wa akili zetu.

Viongozi wetu wanapokwenda kuomba pesa kule nchi za nje, wanafikia na kuishi kwenye mahoteli ya kitalii. Kwa nini akili zetu zisitiliwe shaka? Kiongozi wa watu maskini, anayekwenda kuomba misaada ya watu maskini, anafikia hoteli ya kitalii!

Yamekuwepo malalamiko ya chini chini ambayo kwa namna fulani ni matusi, kwamba wale wanaotoa pesa wakija kuzifuatilia, wanasafiri kwa usafiri wa kawaida. Kama ni ndege wanapanda daraja la tatu, lakini viongozi wetu wanasafiri daraja la kwanza!

Ipo mifano mingi inayoonyesha dalili nyingi za kuwafanya wenzetu wawe na mashaka juu ya ubora wa akili zetu. Mheshimiwa Ndesamburo, juzi, bungeni, alitoa ushuhuda kwamba asilimia 98 ya watu walio na simu za viganjani wanazitumia kutongoza wanawake, kuzungumza umbea, kutuma ujumbe wa mapenzi na kupanga mipango ya ujambazi. Labda asilimia mbili ndio wanatumia simu kwa mipango ya biashara na maendeleo.

Hili ni jambo la kushangaza kwani Tanzania ni kati ya nchi zinazosifika Afrika kwa kuingiza kwa wingi simu za viganjani na makampuni ya simu hizi yanapata faida kupindukia.

Siku za karibuni Benki ya Dunia ilitoa taarifa ya mamilioni ya dola zilizotolewa barani Afrika kwa ajili ya kukuza kilimo lakini wanashangaa na kujiuliza; mbona mapinduzi ya kilimo kwa bara la Afrika hayajafanikiwa kama ilivyotokea Asia?

Najua vyombo hivi navyo vina unafiki wa kutosha kwa sababu wanatumia nchi masikini kujineemesha pia. Lakini cha kujiuliza mbona fedha za namna hiyo zimefanya mapinduzi sehemu nyingine? Kwa nini zisifanye mapinduzi Afrika? Kwa nini tukubali kutumiwa kama nguruwe wa majaribio na sisi tusifaidi kama nchi nyingine?

Tunapaswa kujitathmini hapa. Mara nyingi sana wanaharakati wanaopingana na misaada ya nje huwalaumu watoaji kwamba wanakuja na misaada yao kuja kuitumia huku kwetu wakijineemesha wenyewe. Mimi huwa nauliza kama umeona msaada hautafaidisha taifa kwa nini uukubali?

Kwa hivyo tunawalaumu pia wanaopokea misaada isiyo na tija. Lakini wanaopokea wanaangalia maslahi yao binafsi kwamba watafaidi wao na si taifa. Wenzetu wa Asia wanawarudishia wataalamu wa Benki ya Dunia na IMF fedha zao kama wakigundua hazitakuwa na manufaa, na ndio maana kuna ushahidi wa kitaaluma kwamba mikopo na misaada mingine imeweza kusaidia sana kuleta mapinduzi Asia. Sisi bado tunalia. Tujiulize tatizo lilipo.

Tutalaani wabaguzi hawa, tutashika mabango na kuandamana lakini kabla ya kwenda tujiulize sababu ya kukwama kwetu. Tusikimbilie kulaumu Wazungu kama chanzo cha matatizo yetu.

Kuna wale rafiki zangu wanaolaani ukoloni na ukoloni mamboleo. Malaysia na Ghana zilikuwa zote koloni la Uingereza na zilipata Uhuru mwaka mmoja (1957). Wamalaysia walikuwa wanakwenda Ghana kujifunza kilimo cha mawese. Leo hii Ghana inajifunza kila kitu toka Malaysia kikiwemo kilimo cha mawese!

Tanzania ni mika 46 ya Uhuru sasa. Tuache kuendelea kulia na kulalamikia ukoloni. Sisemi haukuleta madhara lakini tutalia mpaka lini? Tunachukua hatua gani za kuondoa hayo makovu? Au hatua zenyewe ni hizo za kuwaita tena wakoloni waje kuwekeza kwa kuwasamehe kodi?

Hawakatai kuja. Watakuja watatula halafu watatutukana. Hawasemi hadharani lakini wanasemea chinichini kwamba hawa Waafrika ni wajinga.

Wazungu wengi wanaobishana na kauli ya Watson si kwamba wanasikitika sana. Wanaonyesha usoni kwamba wamechukia lakini moyoni wanasema ni kweli hawa wana ujinga wao mkubwa. Wanatutetea ili waendelee kutuvuna. Hawataki tukae chini na kujitathmini tulipoenda mrama.

Nachukia sana kuitwa kiumbe dhaifu hasa kiakili. Nachukia kwa sababu naupenda Uafrika na weusi wangu. Nawapenda Waafrika wenzangu. Nachukia sana wanapoambiwa kwamba wana ubongo dhaifu. Lakini nahisi kuna mahali kama watu weusi tumeteleza.

Kuna ushaidi unaoonyesha kwamba tumefanya mambo ambayo akili zetu zinatakiwa zihojiwe. Kama mtu anaiba mabilioni ya fedha za umma kwenye nchi masikini na kuyaweka Ulaya au kuwekeza mahali popote, huku kukiwa na wananchi wanaokufa kwa kukosa dawa ya Malaria, basi, tuna ulazima wa kujiuliza tuliko na kasoro.

Kama viongozi wanawaibia wanachi wao waliowachagua kuwawakilisha bila aibu yoyote inabidi tuhoji akili zetu. Kama wananchi nao wanaridhika na hila za viongozi wao bila kuchukua hatua madhubuti, basi tuhoji akili zetu.

Kama kijenetiki tuna akili ndogo, basi, hatuna cha kufanya labda ufanyike utaratibu wa kutuunganisha kijenetiki na hao wenye akili zaidi. Kama akili ndogo zinatokana na kukataa kutumia uwezo tuliopewa basi tunaweza kujirekebisha.

Hata kama Watson ataomba radhi kama wale mawaziri wa Japan walivyofanya, atakuwa ameshapeleka ujumbe mzito wa watu weusi kujichunguza! Ujumbe huu ni mzito kwa taifa letu la Tanzania.

Kutoka gazeti la Raia Mwema.

No comments: