Monday, November 12, 2007

yatikisha taifa.

na Charles Mulinda

KUANZISHWA kwa Mahakama ya Kadhi, moja ya hoja zilizobebwa na Rais Jakaya Kikwete katika ilani ya uchaguzi aliyotumia kujinadi kwa Watanzania ili wamchague kuwa rais, sasa imeanza kutishia umoja wa kitaifa.

Mlolongo wa matukio yanayoambatana na madai ya Waislamu ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo, yameonyesha kuwepo kwa migongano mikubwa ya kijamii ambayo chanzo chake ni tofauti za kidini.

Tayari suala la kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi limesababisha baadhi ya viongozi wa dini nchini kutoa matamshi yanayoashiria uvunjivu wa amani, huku wengine wakikimbilia mahakamani kuzuia kuanzishwa kwa mahakama hiyo.

Wachambuzi wameeleza kuwa, kitendo cha Rais Kikwete kuliweka suala la Mahakama ya Kadhi katika ilani ya uchaguzi iliyotumika kumuweka madarakani, ndiyo chanzo cha mgogoro huu unaotishia kuligawa taifa kutokana na imani za kidini.

Inaelezwa kuwa, Rais Kikwete, inawezekana aliliweka suala hilo katika ilani yake ili kuhakikisha kuwa anapata kura nyingi kutoka kwa waumini wa dini ya Kiislamu bila kujua kwamba athari zake zinaweza kusababisha mgawanyiko wa kitaifa.

Mmoja wa watu waliozungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, alieleza kuwa uamuzi wa CCM, kuahidi kurejesha Mahakama ya Kadhi ndiyo chanzo cha tatizo, na unaweza kusababisha maafa iwapo hautatafutiwa ufumbuzi.

Kwamba Rais Kikwete anapaswa kuvunja ukimya na kulizungumzia suala hili ili kuondoa tofauti zinazoanza kujitokeza katika jamii.

“Chanzo cha mgogoro huu ni CCM kuliweka jambo hili la kuanzishwa Mahakama ya Kadhi katika ilani yake ya uchaguzi.

“Hili ndilo liliwafanya Waislamu mwishoni mwa mwaka jana waanze kuishinikiza serikali kurejesha mahakama hiyo, jambo lililowashitua Wakristo, wakapinga, serikali ikaamua kunyamazisha kelele hizo kwa ahadi kuwa, itatoa ufumbuzi.

“Sasa limeibuka upya, na inaonekana safari hii inaweza kutokea mambo ya ajabu, viongozi wa dini wamefikishwa mahakamani, wengine wanakwenda na mabango kumuunga mkono mwenzao, hili si jambo la kawaida, serikali isipolishughulikia, maafa yanaweza kutokea, unajua hakuna kitu kibaya kama imani,” alisema.

Alirejea tamko la Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA), la kumuonya Mchungaji Christopher Mtikila ambaye amefungua kesi Mahakama Kuu akipinga urejeshwaji wa Mahakama ya Kadhi kwa madai kuwa ni chombo cha jihad na ugaidi, kuwa moja ya mambo yaliyochochea kukua kwa mgawanyiko unaoanza kujitokeza ndani ya jamii.

Kauli hii ya Mchungaji Mtikila ilionekana kuwaudhi Waislamu ambao walieleza kuwa wanafuatilia taratibu kauli hizo, huku BAKWATA ikisisitiza kuwa ingawa haina mpango wa kuingia katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Mtikila, itakabiliana na suala hilo kwa namna yake.

Hata hivyo, jambo linaloonyesha kukua taratibu kwa mgogoro huu, ni kitendo cha viongozi wa dini ya Kiislamu kuitaka serikali kusitisha uhusiano wake na Vatican.

Walieleza kuwa uamuzi huo ulifikiwa na viongozi wa Kiislamu, maimamu, masheikh na viongozi wa taasisi mbalimbali za dini hiyo, na kusisitiza kuwa serikali inapaswa kufuta mara moja Ubalozi wa Vatican nchini kwa madai kuwa upo kwa ajili ya Wakristo pekee.

Kauli hii inaonyesha kuwepo kwa manung’uniko kutoka kwa Waislamu dhidi Wakristo kuwa wanapendelewa kwa kuwa na Ubalozi wa Vatican hapa nchini.

Jambo jingine linaloonyesha kuzidi kusambaa kwa mgogoro ni hatua ya wachungaji wa makanisa mbalimbali kukusanyika nje ya mahakama siku Mchungaji Mtikila alipofikishwa mahakamani kwa tuhuma za uchochezi wakiwa na mabango yaliyokuwa yakihoji uhalali wa kukamatwa kwake.

Baadhi ya mabango hayo, yaliandikwa ‘Mufti pia akamatwe, amevunja amani’, na jingine lilihoji ‘Kwa mujibu wa sheria serikali yetu ina dini?’

Ujumbe huu wa mabango ya wachungaji ambao unaashiria kumuunga mkono Mchungaji Mtikila, umetafsiriwa na wafuatiliaji wa mambo kuwa dalili za mwanzo za sehemu hiyo ya jamii kutoiunga mkono serikali katika baadhi ya mambo.

Kwa sasa, suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi nchini linazidi kupanuka, na jina la Rais Kikwete limeanza kuingizwa katika mzozo huo.

Rais Kikwete ametajwa katika sakata hilo pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, wakidaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika mgogoro huo, ambao sasa unazidi kuchukua sura tofauti.

Kwa upande wake, Rais Kikwete ametajwa akitakiwa kuwaomba radhi Watanzania, kwa kile kinachodaiwa kuwa, dhamira yake ya kutaka kuigeuza Tanzania kikatiba kuwa nchi ya Kiislamu na hivyo kuirejesha katika mzozo wa miaka ya mwanzo ya 1990 uliohusisha juhudi za baadhi ya viongozi kuiingiza katika kundi la nchi wanachama wa Jumuiya ya Kiislamu Duniani (OIC).

Aidha, IGP Mwema amepewa siku 21 kumuomba radhi Mchungaji Mtikila, kutokana na kitendo chake cha kuwatuma askari wamkamate (Mtikila), kumhoji na hatimaye kumfungulia mashtaka ya uchochezi wakati hana kosa.

Juzi, akizungumza na waandishi wa habari Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Mchungaji Mtikila, aliyeibua mjadala unaoendelea kuhusu uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, alitaka tamko la Rais Kikwete la kuomba radhi liambatane na hatua kali za kisheria dhidi ya watumishi wote wa umma, waliohusika kwa namna yoyote katika kitendo hicho cha kuingiza Uislamu katika ilani yake ya uchaguzi, serikali na Bunge.

Aliongeza kuwa sambamba na hilo, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho alidai ni kikundi cha maslahi ya kibinafsi cha watu fulani, nacho kifutwe kama inavyoagiza katiba.

Mtikila alisema, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini (TEC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) na Halmashauri ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT), walikutana na walitaka kutoa tamko la kupinga mapinduzi hayo ili kulinda katiba ya nchi, lakini serikali iliwahadaa wasifanye hivyo bali wangojee tume yao ilifanyie kazi suala hilo.

Hata hivyo, Mtikila alisema, inashangaza kuwa tofauti na ahadi iliyotolewa na serikali kwa taasisi hizo nyeti za kidini nchini, harakati zilianzishwa ili muswada kuhusu Mahakama ya Kadhi upelekwe bungeni bila Wakristo kujua, mpaka Mungu alipowafunulia na kuwawezesha kuwahisha ulinzi wao wa katiba mahakamani.

Alisema yeye hapingi kuanzishwa kwa mahakama hiyo, bali anachopinga ni kuingizwa katika katiba ya nchi ambayo kimsingi inapingana na suala hilo.

Kutoka: Tanzania Daima.

No comments: