Monday, December 17, 2007

JK atabiriwa magumu 2008.

Gongola hapa kusoma hiyo tathmini


JARIDA maarufu la The Economist, kwa mara nyingine tena limefanya tathmini yake kuhusu mwelekeo wa kiuchumi wa Tanzania na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kipindi cha mwaka ujao wa 2008 unaojongea.

Tathmini mbili tofauti kuhusu Tanzania, ya kwanza ikichapwa na kitengo cha jarida hilo kinachohakiki mwenendo wa kiuchumi kiitwacho 'Economist Intelligence Unit' (EIU) na ya pili ikiwa katika ukurasa wa 116 wa toleo la kila mwishoni mwa mwaka la 'The Economist-The World in 2008', Rais Kikwete ametajwa kuwa kiongozi ambaye aliingia madarakani na kuwapa wananchi matumaini makubwa ambayo sasa yanaonekana kutoweka.

EIU katika chapisho lake linalopatikana kwenye mtandao wa intaneti, linasema kwa Kingereza; The president, Jakaya Kikwete, and his government will continue to promise much, but on issues such as corruption, policy initiatives will not be matched by effective implementation.

Kwa tafsiri isiyo rasmi, EIU inasema; "Rais Kikwete na serikali yake wataendelea kutoa ahadi nyingi, ingawa katika masuala ya rushwa na uendelezaji wa sera, ahadi hizo hazilingani na matokeo ya kiutendaji."

Mbali ya hilo, jarida hilo linasema kukwama huko kwa Kikwete pamoja na mambo mengine kutasababishwa na yeye kuwa na nguvu kubwa za kimaamuzi peke yake ambayo kimsingi huwanyamazisha mawaziri na kuwafanya wasio na nguvu ya kimaamuzi.

Mbali ya hilo, katika matoleo yake yote mawili, The Economist linasema suluhu ya haraka katika mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar inayotafutwa kupitia mazungumzo kati ya vyama viwili; Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) ni jambo lisilotarajiwa.

Kwa vyovyote vile, utabiri huo wa The Economist, jarida linaloheshimika na kusomwa duniani kote kama utakwenda kama ulivyo kuhusu Zanzibar, basi upo uwezekano mkubwa wa matumaini makubwa yaliyojengeka yakapotea.

Hata wakati mwelekeo ukionekana kuwa mgumu kwa mwaka ujao wa 2008, EIU katika taarifa yake hiyo inaonyesha kuwapo kwa matumaini katika eneo la kukua na kuimarika kwa sekta binafsi.

Katika hili EIU inasema upo uwezekano kwamba, kwa mwaka ujao, msisitizo uliopo sasa wa kukuza uchumi wa soko ukasababisha kuendelea kukua kwa sekta binafsi kutakakoendana na kuimarika kwa miundombinu.

Aidha EIU katika uchambuzi huo, bila kutoa maelezo, inaona kuwapo kwa uwezekano mkubwa wa udhaifu mkubwa uliopo katika sekta ya sheria hivi leo, ukapata tiba katika kipindi hicho hicho cha mwaka ujao.

Katika mwelekeo huo huo, EIU inasema pato la taifa (GDP) ambalo kwa mwaka 2007 limekuwa likikua kwa wastani wa asilimia 6.9 linaweza likabakia hapo hapo mwaka ujao na pengine kufikia kiwango cha hadi asilimia 7.1 katika kipindi cha 2008-09.

Uchambuzi huo wa EIU unaziona sekta za madini na utalii kuwa chanzo kikubwa ambacho kitawezesha uchumi wa taifa hili kuimarika katika kipindi cha mwaka ujao.

Wakati EIU ikitoa mwelekeo huo, The Economist-The World in 2008 linasema; 'Jakaya Kikwete has proved less efficient in office than during his successful election campaign and Tanzanians will increasingly clamour fro delivery of his ambitious platform.'

Kwa tafsiri isiyo rasmi, The Economist inaelezea kuwa; 'Rais Kikwete akiwa madarakani ameshindwa kutimiza yale yaliyomfanya afanikiwe kuwajengea imani kubwa wapigakura wakati wa kampeni, hali ambayo (kuanzia mwaka ujao) itawafanya Watanzania waendelee kupiga kelele kukumbushia ahadi nyingi alizotoa wakati huo'.

Mwelekeo huu wa The Economist kwa kiwango unaelekeana na matokeo ya utafiti yaliyoendeshwa mwezi Oktoba na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) na kutolewa hivi karibuni.

REDET, moja ya taasisi zinazoheshimika ikifanya kazi chini ya Idara ya Siasa ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam katika ripoti yake hiyo ilionyesha kuwa, idadi ya wananchi wanaoridhika na utendaji wa Rais Kikwete kwa wakati huu imepungua kwa tofauti ya asilimia 23 kutoka asilimia 67 za Oktoba mwaka jana, hadi kufikia asilimia 44.4 Oktoba mwaka huu.

Mbali ya hilo, katika utafiti huo, ambao jumla ya watu 1,300 walihojiwa kutoka katika wilaya 26 kote nchini, idadi ya watu walioonyesha kutoridhika na utendaji wa serikali imeongezeka mara dufu kutoka asilimia 7.8 mwaka jana hadi kufikia asilimia 18.6 mwaka huu na hivyo kuufanya mtazamo wa The Economist kutoa mwelekeo unaoendana na hali halisi ya taifa hili kwa sasa.

Hii inakuwa ni mara ya pili kwa The Economist kupitia kitengo chake hicho cha EIU kutoa tathmini dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete tangu ilipofanya hivyo Machi mwaka huu.

The Economist katika ripoti yake hiyo ya Machi 22, mwaka huu ambayo Tanzania Daima iliichapa, Serikali ya Kikwete ambayo wakati huo ilikuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi isiyozidi mitatu, ilitajwa kuwa iliyoanza kupoteza mwelekeo.

Jarida hilo liliandika kuwa, kukosekana kwa mabadiliko yoyote katika kipindi hicho hatimaye kumesababisha serikali ya awamu ya nne iendelee kujenga taswira ile ile ya kukatisha tamaa ya zama za serikali iliyopita iliyokuwa ikiongozwa na Benjamin Mkapa.

"Zaidi ya mwaka mmoja uliopita, Jakaya Kikwete aliukwaa urais kwa kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa urais, baada ya kujipatia zaidi ya asilimia 80 ya kura zote… Watanzania wengi walikuwa na imani kuwa hoja zenye ushawishi mkubwa za wakati wa kampeni zingetekelezwa na kuleta mabadiliko serikalini na utawala mpya ungekuwa na uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko makubwa yaliyokuwa yakisubiriwa kwa hamu.

"Bahati mbaya, ukweli huo umekuwa tofauti, huku serikali ikikumbwa na tuhuma za rushwa pamoja na kukwama kufanikisha kutatua kile kilichokuwa kikionekana kuwa tatizo sugu lisilokwisha la umeme," liliandika The Economist wakati huo.

Pamoja na kusema kwamba, hadi wakati huo hakukuwa na mabadiliko yoyote, jarida hilo lilikiri kwamba, matatizo kama yale ya umeme na rushwa inayoendelea kubakia pale pale yalikuwapo hapa nchini, muda mrefu kabla Kikwete mwenyewe hajaingia madarakani.

Jarida hilo liliandika pia kuwa, kikubwa kilichoonekana kufanywa na Kikwete wakati huo ili kukabiliana na uwezekano wa kuhukumiwa na wananchi, kilikuwa ni kuanza kwake kuweka mikakati ya utekelezaji wa mipango ya wizara moja moja.

Pamoja na kuainisha mikakati hiyo, jarida hilo liliukosoa mwelekeo huo na kuulezea kuwa ni wa kuwahadaa wananchi na unaokinzana na matatizo ya msingi yanayolikabili taifa.

Kwa mtazamo wake lilisema, tatizo la Tanzania haliko katika kukwama kwa miradi iliyoainishwa katika programu za wizara au zilizoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, bali ni kuporomoka kwa ari ya kazi ya watu wengi.

"Mikakati ya sasa inayolenga kujipatia sifa au kuhakikisha serikali inachaguliwa tena katika muhula ujao inadumisha fikra za sasa za serikali hii: Jukumu lake limekuwa kusimamia milolongo ya miradi badala ya kuangalia tatizo kuu linalokwamisha maendeleo ambalo ni ukosefu wa ari ambayo ni muhimu katika kuwezesha utatuzi wa matatizo mengi yanayoikabili nchi," lilibainisha jarida hilo ambalo leo hii limerejea tena japo kwa muhtasari, kutoa maoni yenye mwelekeo huo huo.

Kwa mtazamo wa jarida hilo, mafanikio mema kwa Tanzania hayawezi kupatikana kwa kutekelezwa kwa miradi bali yataletwa na kuwapo kwa mabadiliko ya mfumo wa kiuongozi.

Kutoka Tanzania Daima.

"link" na http://watanzaniaoslo.blogspot.com

No comments: