Makongoro Oging’ na Elvan Stambuli
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete hivi karibuni amepangua nafasi za viongozi wa juu katika idara mbalimbali ndani ya serikali yake hali iliyofanya baadhi ya wasomi kusema wazi kwamba baraza la mawaziri linaweza kubomolewa wakati wowote na watakaobaki au kung’olewa sasa wanajulikana.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam wiki iliyopita baadhi ya wasomi na wananchi wa kawaida walisema kuwa wana matumaini makubwa na Rais Kikwete kuiletea maendeleo nchi hii isipokuwa anaangushwa na watendaji wabovu wakiwemo baadhi ya mawaziri ambao ‘wamelala usingizi’ na wamemuomba awabadilishe mapema kabla ya mambo hayajaharibika.....
Aidha waliendelea kusema kuwa hakuna haja ya Rais Kikwete kuwavumilia mawaziri ambao wameshindwa kuchapa kazi kwani wamekuwa wakisababisha serikali yake kulaumiwa na wananchi na baadhi yao sasa wako matumbo moto.
Wasomi kadhaa akiwemo Dk. Azaveli Lwaitama wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa maoni ya wananchi ni kwamba wana matumaini naye Rais Kikwete na kwamba akichukua hatua na kuwathibiti mawaziri au kupanga baraza lake la utendaji wa serikali anaweza kuwaridhisha.
Alisema Rais Kikwete anaweza kuonekana hayupo pamoja na mawaziri wake kwani hata Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe aliposimamishwa bungeni yeye aliunda kamati ya kuchunguza mikataba ya madini na kumuingiza hivyo (Zitto), kuwa na imani kwamba kama utafiti mwingine ukifanyika sasa, watu wanaomuunga mkono Rais wataongezeka.
Aidha baadhi ya wananchi wamesema wanashangazwa na ubabaishaji unaofanywa kuhusu mikataba ya madini ambayo imeiingizia taifa hasara kubwa huku ikiwaneemesha wachache.
Profesa Leonard Shayo akizungumzia mikataba mbalimbali inayosainiwa kwa niaba ya nchi katika taarifa yake mwishoni mwa wiki alisema anashangazwa sana na mikataba ya kiuchumi ya nchi inayowashangaza wengi na kusema kuwa hiyo inatiwa kwa woga wa kutoa mawazo.
“Iweje mfanyakazi wa kawaida wa nchi masikini ya Tanzania awe na mali nyingi kuliko mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa? Tutakuwa na kosa gani kama watu hao tutawaita wezi?,” alihoji Profesa Shayo.
Alisema taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa haina haja ya kusubiri raia wema wawaletee taarifa za wala rushwa badala yake wangetumia mali zilizolimbikizwa kuwa ni ushahidi tosha kwa mtuhumiwa.
Alisema, kiongozi anayeiibia nchi na kujilimbikizia mali atatumia muda wake kupanga jinsi ya kuiibia nchi badala ya kupanga mipango ya maendeleo kiuchumi kwa nchi.
“Ndio maana wakati wa utawala wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere waliojilimbikizia mali walikuwa wakipelekewa fomu kupata maelezo ya vyanzo vya mali zao,” alisema Profesa huyo ambaye ni mtaalamu wa hisabati.
Mhadhiri mwingine ambaye aliombwa jina lake kuhifadhiwa alisema kuwa baadhi ya mawaziri hawafanyi kazi na wanamtegemea Rais Kikwete hali ambayo inamfanya kiongozi huyo wa nchi kuingilia mambo ambayo yanaweza kufanywa na kusimamiwa na mwenyekiti wa serikali za mtaa au mkuu wa wilaya, hivyo kusema wazi kuwa hao hawafai na akashauri wang’olewe.
Alitoa mfano pale rais anapotembelea mikoa hukutana na mambo mengi yanayofanywa kinyume lakini hakuna kiongozi anayekemea kana kwamba hakuna viongozi katika maeneo hayo, hali inayompa kazi ya ziada kiongozi huyo wa nchi.
“Sina imani na baadhi ya mawaziri katika utendaji wao wa kazi, namshauri Rais Kikwete awamulike viongozi kama hao na awabadilishe mara moja kwa sababu katiba ya nchi inamruhusu kufanya hivyo, wale wachapa kazi aendelee nao,” alisema Mhadhiri huyo.
Msomi mwingine Bw. Tanu Gomba mkazi wa Mbezi kwa Msuguli alisema kuwa baadhi ya viongozi wamekuwa hawatimizi wajibu wao na hata kusababisha matatizo na kutakiwa kujiuzulu na umma.
“Baadhi ya viongozi tena mawaziri wizara zao zinafanya vibaya na kusababisha kelele kutoka kwa wananchi kuwataka kujiuzulu lakini huwa hawataki kujiuzulu, imefika wakati sasa tuige mfano wa Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alipojiuzulu Uwaziri miaka ya 1980 kwa kosa lililofanywa na viongozi wa Shinyanga alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,” alisema Gomba.
Hivi karibuni Taasisi ya Elimu na Demokrasia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET) iliukosoa utendaji wa serikali, ambapo ilieleza kuwa Watanzania wameridhika sana na utendaji wa Rais Kikwete kwa asilimia 44.4 wakati wameridhika na Baraza la Mawaziri kwa asilimia 21.8 hivyo kuonyesha kuwa Rais analizidi baraza lake kwa utendaji kazi.
Aidha Rais Kikwete katika ziara yake ya kuutembelea mkoa wa Pwani wiki iliyopita alionesha ukali kwa kuwaonya viongozi walafi wanaojigawia miradi ya wananchi kuwa watakiona cha mtema kuni na atawaanika hadharani.
Siku chache baada ya Rais kuapishwa mwaka 2005 alitoa tahadhari kwa mawaziri na manaibu wao (baadhi yao picha zao zipo uk. 1) kuwa hatawavumilia wale wote watakaokuwa goigoi na alisema anaweza kuwabadilisha ikiwa hapana budi.
No comments:
Post a Comment