Friday, December 21, 2007

Sina mpango kwa sasa kubadili Baraza la Mawaziri- Kikwete


HabariLeo; Friday,December 21, 2007 @00:01.

Rais Jakaya Kikwete.

RAIS Jakaya Kikwete leo ametimiza miaka miwili kamili tangu aingie madarakani, huku akisema kwamba kwa sasa hana mpango wa kubadili baraza la mawaziri. Akizungumza katika mahojiano na wahariri yaliyofanyika Ikulu Dar es Salaam, Rais Kikwete alisema Serikali na Baraza la Mawaziri lililopo viliundwa kwa kuzingatia mahitaji ili kuwezesha kutoa huduma vizuri zaidi kwa wananchi, na kwa muda huu haoni haja ya kulibadili.

“Tuone huko mbele ya safari, kama yale ambayo yalitufanya tuwe na mfumo huu sasa hivi na muundo huu wa serikali tutakuwa tumeyatekeleza, tutafanya marekebisho,” alisema. “Uvumi huu (wa kubadili mawaziri) ni uvumi tu. Kama kuna haja ya kubadili mawaziri tutabadili. Kama hakuna haja tutaendelea. Kwa sasa ni uvumi tu au ni matakwa ya watu,” alisema na kuongeza kuwa, kama Rais ana mamlaka ya Baraza la Mawaziri anaweza kulibadili wakati wo wote.

Katika mahojiano hayo ambayo yamechapishwa ndani ya gazeti hili, Rais Kikwete alizungumzia masuala ya nyanja mbalimbali, ikiwamo mtazamo wake juu ya utekelezwaji wa ahadi ya Maisha Bora kwa Watanzania wote, rushwa, marekebisho ya mikataba ya madini na mengineyo, ufanisi wa Shirika la Umeme (Tanesco), Shirika la Reli (TRL), Shirika la Ndege (ATC), kukwama kwa mahujaji, mfumuko wa bei, hali ya siasa, soka, ugonjwa wa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali, ambaye anapatiwa matibabu nchini Marekani na suala la kuhamia Dodoma.

Akizungumzia rushwa, Rais Kikwete alisema kumekuwa na matatizo katika kushughulikia rushwa kubwa kutokana na unyeti na ugumu wa kufanya upelelezi wake, lakini kuna mafanikio yamepatikana katika kutafuta ushahidi wa suala la kashfa ya rada, baada ya kushirikisha asasi mbalimbali za ndani na nje.

“Tuna hiyo (kesi) moja tumeishughulikia. Kuna nyingine ambazo wanaendelea kuzishughulikia. Sasa nasema hivi, uchunguzi wake ni uchunguzi unaochukua muda mpaka tufike mahali tuseme sasa tunayo kesi tunaweza kuipeleka mahakamani…siku (ile kesi ya rada) itakuwa imeanza hapo mahakamani zitakapotoka zile facts unajua kwamba it has really taken a lot of work (kazi imefanyika),” alisema Kikwete.

Kuhusu dhana ya Maisha Bora, Rais Kikwete alisema serikali yake imefanikiwa kuweka misingi kwenye maeneo kadhaa na kilichobaki sasa ni ujenzi wa matofali juu ya msingi huo. “Niko confident (nina hakika) kwamba tutakapofikia 2010 watakapokuwa wanatufanyia tathmini, hukumu yetu itakuwa safi sana, kwa sababu mambo mengi yako yanakwenda, yapo on going (yanaendelea). Sababu si kila kitu kitatokea katika mambo yote sababu ahadi zetu ni za miaka mitano, siyo kwamba sasa katika miaka hii miwili mambo yote yamekamilika,” alisema.

Rais pia alizungumzia hali ya siasa nchini, kwa kusema ni shwari na kwamba mazungumzo juu ya kuondoa mpasuko wa Zanzibar yanakwenda vizuri. Alisema pia kwamba msimamo wa serikali yake ni kupokea mawazo na ushauri wo wote wa maana kutoka kwa ye yote. “Serikali tupo tayari kusikiliza. Tutasikiliza mpinzani. Tutasikiliza NGOs (asasi zisizo za kiserikali), tutamsikiliza hata mtu binafsi tu.

Mimi nasikiliza sana hata kwenye simu zangu wakiniletea mimi nikisikia ni jambo la maana nalifanyia kazi. Nalichukulia hatua. Nadhani ndiyo wajibu wetu. Rais Kikwete alizitetea TRC na ATC kwa kusema kwamba ni mapema mno kutaka mashirika hayo yafanye kazi kwa ufanisi kwa vile ndiyo kwanza yanaendelezwa chini ya mfumo mpya wa uendeshaji.Hata hivyo, alidokeza kwamba serikali iko katika hatua za mwisho za kubadili sheria inayoipa Tanesco mamlaka ya kuwa taasisi pekee inayoruhusiwa kusambaza umeme nchini.

Chini ya mpango huo, alisema kampuni binafsi na hata za nje zitaruhusiwa kuzalisha na kusambaza umeme. Alitahadharisha kwamba katika suala la kupitia upya mikataba ya madini na mengineyo iliyofikiwa na serikali na asasi nyingine, Rais Kikwete alisema jambo hilo linapaswa lifanywe kwa umakini, lakini lisichukuliwe kwamba kuna kutafuta mchawi kwani baadhi ya wahusika wa miaka ya 1970 ama tayari wamestaafu, wamekufa au walifanya hivyo kwa makosa ya kutofahamu au kutokuwa na ujuzi na uzoefu.

Kwa mujibu wa Rais, uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda Dodoma uko pale pale na ndiyo maana baadhi ya wizara ziko huko na nyingine zitafuata. Kuhusu ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Redet) iliyotolewa hivi karibuni kuhusu jinsi utendaji kazi wake na wa mawaziri unavyokubalika kwa wananchi, Rais Kikwete alisema ni ripoti nzuri na kama kioo ambacho kinaisaidia serikali kujitazama na kujipanga upya kwa hatua zinazofuata.

Mahojiano hayo yalimpa pia Rais fursa ya kueleza kwamba anaamini kuna maeneo ambayo inabidi yafanyiwe marekebisho katika utoaji wa mikopo kwa wajasiriamali ijulikanayo kama Mabilioni ya JK kwa kuhusisha taasisi na benki nyingine zaidi ya NMB na CRDB pekee.



No comments: