Friday, December 28, 2007

Umeme bei juu.
na Ratifa Baranyikwa.

MAMLAKA ya Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi ya Maji na Nishati (EWURA), imeridhia Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 21.7 ya bei ya sasa kwa watumiaji wa Tanzania Bara, badala ya asilimia 40 iliyoombwa na shirika hilo.

Kwa upande wa gharama za kuunganisha umeme kwa wateja wapya, EWURA imeridhia ongezeko la kati ya asilimia 66 hadi 215.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Haruna Masebu, alisema kuwa bei hizo za umeme na gharama za maunganisho zitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2008.

Masebu alisema kuwa maamuzi hayo yametokana na maoni ya wadau mbalimbali, yaliyotolewa na kufuatia kikao cha bodi ya wakurugenzi wa EWURA, kilichojadili na kufanya uchambuzi kwa kina juu ya ombi la Tanesco na maoni hayo.

Awali, TANESCO iliwasilisha ombi la kutaka kuongeza bei ya umeme kwa wastani wa asilimia 40 na ongezeko la kati ya asilimia 66 hadi 281 kwa gharama za maunganisho kwa kipindi cha miaka miwili ya 2008 na 2009.

Kwa mujibu wa Masebu, Ewura pia imeridhia shirika la mafuta na umeme Zanzibar kupandishiwa gharama za umeme kwa asilimia 168.

Alipoulizwa ni kwa nini Zanzibar imepandishiwa kwa kiasi hicho kikubwa ukilinganisha na Tanzania Bara, Mkurugenzi wa marekebisho ya Uchumi wa EWURA, Felix Ngamlagosi, alisema kuwa gharama za umeme kwa upande wa Zanzibar zimekuwa ndogo kwa muda wote ukilinganisha na upande wa Tanzania Bara ambako zimekuwa zikipanda kila mara.

Masebu alisema kuwa ongezeko hilo lina mantiki na ni halali na kwamba uchambuzi uliofanywa ulizingatia gharama ambazo Tanesco inazitumia katika kuzalisha umeme, gharama za uendeshaji, matengenezo, uwekezaji mdogo na hivyo isingekuwa vema kuikatalia Tanesco kupandisha gharama hizo.

"Ilikuwa ni lazima Tanesco ipandishe gharama, kwani isingefanya hivyo uchumi wake ungeshuka na hivyo kulifanya shirika kuyumba na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo," alisema.

Aidha, alisema kuwa kutokana na ongezekop hilo, mwakani Tanesco inatarajiwa kukusanya sh bilioni 56.4 zaidi ya kiwango inachokusanya hivi sasa na kwamba imekubaliwa fedha hizo zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya mfumo wa usambazaji umeme nchini.

"Tafsishi tuliyofanya ilihusisha tathmini ya masuala ya kiuchumi na ya kiufundi pamoja na kufanya mikutano ya tafsishi katika miji mitano, ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Mbeya na Dar es Salaam ili kupata maoni kutoka kwa wadau," alisema.

Masebu alisema kuwa nyongeza iliyoidhinishwa itaiwezesha pia TANESCO kulipia gharama za uendeshaji na ukarabati wa miundombinu bila kujumuisha gharama za uchakavu.

Aidha, itaiwezesha TANESCO kupata fedha za kununulia vifaa kwa ajili ya kuwaunganisha wateja wapya.

"Tanesco itafanya utafiti wa kina wa kutambua viwango vya upotevu wa umeme wa kiufundi na kibiashara katika mfumo wake, utafiti huo utalenga kupata mkakati wa kupunguza upotevu wa umeme kutoka viwango vya sasa hadi kufikia viwango vinavyokubalika, taarifa ya utafiti itawasilishwa ndani ya miezi 12 tangu kutolewa kwa agizo hili," alisema.

Aidha, alisema kuwa ndani ya kipindi cha miezi sita, Tanesco itapitia upya uamuzi wake wa kusitisha matumizi ya mitambo yake ya dizeli na wa kutofanya matengenezo muhimu ya mashine zake zilizoko katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kutoa taarifa kwa EWURA.

Kwa upande mwingine, alisema kuwa ifikapo Machi 1, 2008, TANESCO itawasilisha kwa EWURA mpango wa ukarabati na uboreshaji wa mitambo kutokana na kiwango cha gharama kilichoidhinishwa.

Pia, ifikapo Machi 31, 2008, TANESCO inatakiwa iwe imewasilisha EWURA uthibitisho kwamba imeanza kufunga makasha ya dira za umeme zenye teknolojia ya kiusalama zinazozuia wizi wa umeme.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, TANESCO pia itatakiwa kuwasilisha taarifa mbalimbali EWURA kuhusu wateja ambao wana nia ya kuchangia upanuzi wa miundombinu ya usambazaji umeme, pia kutoa taarifa zake za fedha kila wakati zitakapokuwa zinahitajika EWURA.

Taarifa hizo zitazingatiwa na EWURA katika kufanya tathmini ya uhalali katika maombi yote yajayo ya TANESCO ya kurekebisha bei za huduma.

Alisema kuwa Tanesco tayari walishapatiwa taarifa za viwango vilivyoidhinishwa na iwapo shirika hilo halitaridhishwa na maamuzi hayo, lina haki ya kukata rufaa.


Kutoka Tanzania Daima.


No comments: