Na Boniface Meena
WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Joseph Mungai amesema waraka wa mapendekezo ya mwananchi kuwa na uraia wa nchi mbili umekamilika na kufikishwa kwenye Baraka Baraza la Mawaziri.
Hata hivyo, waraka huo utapelekwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata muafaka wa pande zote mbili za Muungano.
Mugai alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya wizara hiyo na vitengo vyake kwa miaka miwili ya serikali ya awamu ya nne.
"Suala la uraia wa nchi mbili mchakato wake unaendelea na suala la vitambulisho vya uraia pia mchakato wake unaendelea na kwamba mchakato huo utagharimu kiasi cha dola Marekani milioni 152 (karibu 15.2 bilioni )," alisema Mungai.
Akizungumzia suala la wakimbizi, Mungai alisema idadi ya wakimbizi nchini imepungua kutoka 615,000 mwaka 2005 hadi wakimbizi 432,583 mwezi Novemba, mwaka huu baada ya zoezi la kuwarejesha makwao wakimbizi kuendelea vizuri.
Hata hivyo, alisema utafiti uliofanyika kuangalia ni asilimia ngapi ya wakimbizi hao wangependa kurudi nchini mwao hasa wale wa Burundi, imeonekana kuwa asilimia 21ya wakimbizi wa Burundi wangependa kurudi kwao na asilimia 79 wangependa kubaki nchini na hatimaye kuomba uraia.
Kwa upande wa magereza, alisema uwezo wa kisheria wa kutunza wafungwa umeongezeka kutoka wafungwa 22,6699 hadi 27,653 pia wafungwa na mahabusu wamepungua kutoka 46,416 hadi 43,262, lakini hata hivyo bado kuna tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu gerezani.
Alisema sababu za msongamano katika magereza ni ongezeko la uhalifu nchini ambalo husababisha ongezeko la idadi ya wafungwa lisilowiana na ongezeko la nafasi za kuwahifadhi pamoja kesi zao kuchelewa kusikilizwa mahakamani.
Kuhusu zimamoto Mungai alisema wizara inajitahidi kuboresha miundombinu ya kikosi hicho ili kiweze kukabilia na na majanga ya moto na mengine.
No comments:
Post a Comment