Saturday, January 12, 2008


Ballali: Maswali 15 Ikulu

M. M. Mwanakijiji

PONGEZI zimemiminika na makofi ya shangwe yamesikika. Wenye kugongeana chupa wamegongeana na waliopongezana ‘ki namna’ zao wamepongezana. Hatimaye Kikwete kafanya kweli.

Kile ambacho watu walifikiri hakitatokea inaonekana kimetokea na sasa hivi shujaa wa Tanzania si mwingine, bali ni Rais Kikwete. Hatimaye yale aliyoyasema kuwa “hana ubia” na mtu kwenye urais kwa watu, yameonekana kweli! Nyimbo za pongezi zitaanza kuimbwa na kelele za ushindi zitaanza kusikika.

Magazeti yakatangaza, “Ballali atimuliwa”, “Ballali afukuzwa”, na yale ya kiingereza yakasema “Kikwete fires Ballali”. Watanzania wakajikuta kwa mara ya kwanza wamejawa na tabasamu. Na mimi nilikuwa mmoja wao. Hata hivyo furaha yangu haikudumu muda mrefu hasa baada ya kupata nafasi ya kuangalia “tamko” la rais lililotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo.

Baada ya kumaliza kulisoma tamko hilo, nilijikuta nimenywea utadhani mtu aliyekemewa mapepo “yakome na kulegea”.

Badala ya kuona majibu ya maswali ya watu wengi kuhusu ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), matokeo yake nilichoona ni maswali mengi kuliko majibu na kwa kadiri nilivyozidi kufikiri, ndivyo nilivyozidi kudadisi na kwa kadiri nilivyofikiri kuwa nimepata majibu ndivyo na msururu wa maswali ulivyozidi na mwisho nikajikuta nimeshika tama na kutikisa kichwa changu kwa kuchanganyikiwa. Hivi tunashangilia nini?

Nikiwa nimezama kwenye mawazo ya tamko hilo ndivyo maswali yalipoanza kunijia na kwa vile sifurahii kubakia na maswali tu kichwani, nikaona bora nimuulize mtu mwenye majibu. Nina uhakika kuwa Katibu Mkuu Kiongozi anayo majibu ya maswali yote nitakayoyauliza hapa ambayo bila ya shaka watu wengine wanayo pia, lakini labda hawatapata nafasi ya kuyauliza na wamebakia nayo kichwani au kwenye gumzo mtaani. Hivyo nimejitwisha mzigo wa kuuliza maswali haya ya ziada ili angalau tujue tunachoshangilia hasa ni nini.

Kwanza kabisa naomba kueleweshwa tu kwanini Katibu Mkuu alitumia neno “kutenguliwa” kuelezea kuondolewa kwa Gavana Ballali kutoka kwenye nafasi hiyo ya juu Benki Kuu. Kati ya maneno mengi ambayo wangeweza kutumia kama vila “Rais amemfukuza kazi”, “Rais kamsimamisha”, “Rais amemwondoa” au “Rais amemstaafisha” n.k, kwanini waliamua kutumia neno kutengua. Hatua aliyochukua rais kumuondoa Ballali ilielezwa hivi na Luhanjo: “Rais ametengua uteuzi wa Dkt. Daudi A. Ballali kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.”

Kimsingi ni kuwa rais amemuondoa Ballali kuwa Gavana wa Benki Kuu. Lakini swali langu ni je, rais amemfukuza kutoka katika ajira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hivyo Ballali si mtumishi wa serikali hiyo? Kwa kuamua kutumia neno “kutengua” kimsingi wanachosema ni kuwa rais amebadilisha uteuzi wa Gavana Ballali”.

Hapa nijaribu kufafanua hii lugha yetu. Kuteua ni tofauti na kuchagua. Kwenye ulimwengu wa siasa, viongozi wa kuchaguliwa ni wale ambao wananchi au wawakilishi wao wanamchagua kwa kumpigia kura (ya aina yoyote ile) na kumpatia nafasi fulani. Kwenye hili, ndipo tunao madiwani, wabunge, wenyeviti wa mitaa n.k Kuweko kwao madarakani kunatokana na uchaguzi.

Wapo vile vile viongozi wa kuteuliwa ambao ni wengi zaidi ambao wanapata nafasi zao baada ya mtu mwenye uwezo wa kuwapatia nafasi hizo anapoamua kwa ridhaa yake mwenyewe kuwapatia nafasi hizo. Watu hao miongoni mwao ni kama Mwanasheria Mkuu, wakuu wa vyombo mbalimbali vya usalama n.k Gavana Ballali ni miongoni mwa “wateuliwa”.

Sasa, jinsi ya kumuondoa aliyechaguliwa ni kutomchagua tena au anapokosa sifa za kuendelea na nafasi hiyo. Kwa kiongozi aliyeteuliwa anaweza kuondolewa aidha kwa kuamua kujiuzulu, kulazimishwa kujiuzulu au pale yule aliyemteua anapoamua kumuondoa na kumpatia nafasi nyingine au anapoamua kumuondoa kazi na kumtupa nje ya utumishi. Sasa, inapotokea kuwa mtu anaondolewa kwenye ajira na kuambiwa akatafute kibarua kingine, mtu huyu tunasema “ametimuliwa” au “amefukuzwa kazi”.

Hata hivyo, inapotokea kuwa rais anaamua kubatilisha uteuzi aliokwisha ufanya, basi anakuwa ametengua uteuzi huo. Hiyo haina maana kuwa mtu ambaye alikuwa anashikilia nafasi hiyo si mtumishi tena wa serikali. Mtu anaweza kutenguliwa uteuzi wake, lakini bado akaendelea kuwa mtumishi katika nafasi nyingine. Mara nyingi neno kutengua linahusu nafasi ile aliyopo na si ajira yake.

Mfano mzuri wa hili ni kuhusu aliyekuwa Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi na Teknolojia, Prof. Brig. Jen. Kohi. Miezi michache iliyopita Rais Kikwete alitengua uteuzi huo na hivyo kumuondoa kutoka nafasi hiyo. Hata hivyo, rais hakuwa amemfuta kutoka katika ajira (kuna taratibu za kumuondoa kiongozi wa ngazi hiyo ya jeshi). Ni kwa sababu hiyo basi, Brig. Jen. Kohi amerudishwa JWTZ ambako bila ya shaka anaendelea na kibarua chake japo si cha “ujiko” kama cha Costech.

Kwa minajili hiyo basi, ninaamini kuwa Rais Kikwete hajamfukuza kutoka katika utumishi wa serikali Ballali, bali alichofanya ni kumuondoa tu kwenye nafasi ya ugavana, huku bado akiwa ni mtumishi wa serikali. Aidha, akiendelea kusubiri uchunguzi wa kisheria dhidi yake au ana mpango wa kumtafutia kibarua kingine. Je, Luhanjo niko sahihi? Je, Rais Kikwete kwa kumuondoa Ballali amemfuta kutoka ajira ya Jamhuri ya Muungano au amemuondoa tu ugavana, lakini bado ni mtumishi wa serikali?

Kama amemfukuza hadi ajira ya Muungano, ina maana kuwa serikali kuanzia sasa haiwajibiki katika kumhudumia huko aliko mgonjwa na ameandaliwa malipo yake yote yanayohusiana na utumishi wake.

Kama hilo ni kweli, hatuna budi kujiuliza kwa vile hadi hivi sasa hakuna ofisa yeyote wa serikali aliye tayari kusema Ballali kalazwa/alilazwa hospitali gani, inawezekana kuwa serikali haijui aliko?

Kama wamemfukuza kutoka kwenye ajira ya serikali, tuna uhakika gani hatua za kisheria zilizoagizwa na rais zitamfikia huko aliko ukizingatia kuwa viongozi walioenda kumtembelea walikuwa wamefungwa vitambaa usoni ndiyo maana hawakuiona hiyo hospitali wala jina la hiyo hospitali?

Lakini tatizo jingine ninaloliona kwenye “kutenguliwa” huku ni kuwa, inawezekana vipi kutengua uteuzi wa mtu aliyetangaza kujiuzulu? Gavana Ballali aliandika barua ya kujiuzulu Desemba 19, na hadi sasa serikali haikukiri kupokea barua hiyo na matokeo yake wanakuja na “kutengua”. Kuna watu wanadhani rais ametengua kujiuzulu kwa Ballali, siyo hivyo, hivi hawasomi magazeti au kuna mtu aliwaficha hiyo barua? Kama barua waliipokea na mtu kawaambia kuwa ni mgonjwa hawezi kazi, sasa unaitengua nafasi yake ili kiwe nini kama si mazingaombwe?

Kinachoudhi ni magazeti ambayo yaliandika “Ballali ajiuzulu” ndiyo hayo hayo yameandika “Ballali atimuliwa”. Sasa hata kama ni kuchanganyikwa ni kweli tunachanganyikiwa kiasi hiki? Ballali kawaambia yeye ni mgonjwa, rais alipozungumza na waandishi siku ile ile ya barua aliwaambia wananchi kuwa Ballali ni mgonjwa, Salva alipoulizwa na yeye alisema Ballali ni mgonjwa, sasa mtu kawaambia mgonjwa na anataka kujiuzulu mnakataa na baadaye mnasema “uteuzi wake umetenguliwa”. Tuwaelewe vipi? Mazingaombwe mengine, inabidi mfanye mazoezi ya ziada!

Naomba tu jibu jepesi, Ballali amefukuzwa toka ajira ya serikali? Au ameondolewa tu ugavana huku hatua nyingine za kinidhamu au kisheria zikisubiri? Maana tunaweza kuwa tunashangilia ushindi hewa!

Nikiachana na Ballali, nirudie tena tamko lenyewe na maswali mengine ambayo bado yamo kichwani mwangu na bila ya shaka kwenye vichwa vya wengine.

Rais ameagiza Bodi ya Wakurugenzi wa BoT kukutana mara moja na "kujadili taarifa ya ukaguzi na kuchukua hatua zipasazo za kinidhamu dhidi ya maofisa wote wa benki, walio chini ya mamlaka yake waliohusika na kusababisha hasara hii kwa taifa." Tatizo ni kuwa, bodi hii ndiyo ilikuwa inatakiwa kuisimamia Benki Kuu! Inakuwaje bodi iliyoshindwa kusimamia fedha zetu leo ndio iwe ya kwanza kuchukua hatua? Je, watu wote waliomo kwenye bodi hiyo hawakuhusika kwa namna moja au nyingine na upotevu huo? Jinsi Mwenyekiti wa Bodi ya ATC alivyoingilia utendaji kwenye sakata la mahujaji ni kwanini tuamini kuwa hakuna mjumbe wa bodi ambaye alihusika na upotevu wa fedha zetu BoT? Kwanini rais asiivunje bodi yenyewe ya BoT na kuunda mpya ambayo ingepewa jukumu hilo?

Kwanini Watanzania waamini kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa BoT watafanya kile walichoshindwa kufanya miaka yote hii?

Kwanini Rais Kikwete kama kweli "amesikitishwa na kukasirishwa" na kitendo hiki, asivunje na kupangua nafasi zote za ajira ya serikali huko BoT (ana nguvu na uwezo wa kikatiba kufanya hivyo) na kuiunda BoT upya? Kwa mfano, mmoja kati ya wajumbe wa bodi hiyo, anatajwa katika mojawapo ya makampuni yanayodaiwa kuchota fedha BoT na yeye yuko kwenye bodi hiyo. Kweli watamkoma nyani giledi?

Kutokana na swali hilo hapo juu, Rais Kikwete anataka kutuambia kuwa mtu pekee ambaye yeye ana uwezo wa kutengua ajira yake Benki Kuu ni Gavana pekee? Au anataka tuamini kuwa kati ya watu wote walioko kwenye nafasi za kuteuliwa Benki Kuu ni Ballali pekee anayehusika na upotevu wa fedha? Ina maana ya kuwa watu wengine wote wa kuteuliwa hawakuhusika na upotevu huu?

Nakumbuka katika kikao kilichopita cha Bunge, jinsi Waziri wa Fedha, Zakia Meghji alivyojaribu kujibu swali kuhusu minara ya BoT. Na pia nakumbuka jinsi alivyojaribu kujibu hoja kuhusu EPA na baadhi ya haya makampuni. Ripoti hii imeonyesha kuwa kuna tatizo BoT na si dogo. Sasa, kwa kiasi gani Wizara ya Fedha imeshindwa kusimamia Benki Kuu na kuruhusu upotevu mkubwa wa fedha kiasi hicho?

Je, wale waliokuwa watumishi wa Wizara ya Fedha wakati wa upotevu huu, wao wamechukuliwa hatua gani? Na hapa nina maana wale ambao hawako chini ya Bodi ya Wakurugenzi wa BoT.

Pia tunaomba kuelezwa ile Kamati ya Fedha ya Bunge iliyopitisha hesabu za BoT za mwaka 2005/2006 walikuwa wanaangalia hesabu gani hizo? Je, wabunge waliokuwa wanapitia hesabu hizo wanaweza kueleza jinsi gani walipitisha hesabu za wizi?

Zaidi ya yote, tunafahamu kuwa hoja za upotevu wa mabilioni ya BoT hazikuhusu EPA peke yake, bali mambo mengine mengi. Na inaonekana jinsi ripoti ilivyotolewa ni kuwa hatua zitachukuliwa kwa wale waliohusika na wizi wa EPA tu na si kwingineko. Tatizo ni kuwa fedha zilizopotea kwa kiasi kikubwa ni nje ya EPA. Kiasi kinachotajwa cha dola karibu milioni 133 hivi ni kiduchu tu ya zile zinazodaiwa kupotea ndani ya miaka kumi hii iliyopita. Makadirio ya chini yanaweka kwenye dola milioni 900 na makadirio ya juu yanakaribia dola bilioni boja na ushee!

Sasa kwanini tunashangilia haka kaushindi kadogo ambako ni ka kutunyamazisha? Kama Rais Kikwete amedhamiria kuisafisha Benki Kuu, kubwa ambalo angeweza kufanya ni kupangua safu nzima ya uongozi na hata ikibidi kuvunja kitengo cha EPA, na kuunda Benki Kuu upya. Nimesema hivi kwa sababu Benki Kuu ndiyo inayotakiwa kusimamia taasisi nyingine zote za fedha. Unapotokea wizi mkubwa na upotevu mkubwa namna hii hakuna jinsi nyingine isipokuwa ni “safisha safisha”. Kilichotokea hakikaribiani na kusafisha safisha, kilichofanyika ni kupangusa tu!

Kwa vile tumeomba msaada wa kampuni ya ukaguzi toka nje na wao wakashirikiana na wataalamu wengine toka nje ya nchi, na kwa vile kuna dalili kuwa kuna uhalifu umetendeka, je, Rais Kikwete yuko tayari kuomba msaada wa kitalaamu toka US Secret Service (walinzi wa fedha za Marekani, pamoja na Rais...) au New Scotland Yard waje kutusaidia kufanya uchunguzi wa miaka yote ambayo Ballali alikuwa Gavana?

Kama kwa mwaka mmoja tu (2005/2006) tumepoteza kiasi hicho cha dola milioni 133, kwa miaka yote aliyokuwa Gavana tutakuwa tumepoteza kiasi gani? Je, tunaweza kuwaomba wataalamu toka nje ya serikali wafanye uchunguzi wa kina na kutoa mapendekezo ya kuboresha Benki Kuu? Hoja ya “Usalama wa Taifa” imepitwa na wakati kwani tuliofikiri wanalinda usalama wa taifa wameacha wizi mkubwa utokee, bora tuwaombe wageni maana fedha nyingi zinatoka kwao!

Kwenye hili tunauliza kwanini Rais Kikwete na serikali yake waliamua kuchagua hesabu za 2005/2006 tu? Kuna madai ya makampuni mengine ya Mwananchi Gold, Tangold, Deep Green, Meremeta n.k ambayo yote nayo yametumia nafasi nyingine kwenye Benki Kuu kuchota mabilioni ya fedha za Watanzania, kwanini raia hataki makampuni hayo yachunguzwe? Akiamuru yote yachunguzwe anaweza kujikuta hana serikali! (samahani nimejijibu mwenyewe).

Rais ameagiza kuwa vyombo vya usalama licha ya kuchukua hatua dhidi ya watu na makampuni (hata kama hayapo tena na yamefilisiwa), pia wahakikishe fedha zilizolipwa bila uhalali zinarudishwa. Je, hili halitukumbushi mawazo yake kuhusu suala la rada kuwa "tutaidai serikali ya Uingereza waturudishie fedha zetu kama tutakuwa tumelipa zaidi kwani BAE ni kampuni ya serikali"? Kama makampuni haya hayapo na yamejitangaza kufilisiwa ni kwa kiasi gani atarudisha fedha hizo?

Luhanjo anaweza kujitolea na kutueleza wananchi makampuni hayo yote yanamilikiwa na nani au aweke hadharani ni nani waliyaandikisha maana baadhi ya majina yake yanatia kero!

Uamuzi mmoja wa rais ambao nilijikuta ninaupongeza ni ule wa kuamuru “shughuli za ulipaji wa madeni katika Akaunti ya EPA zisimamishwe mara moja mpaka hapo taratibu za uhakiki na utaratibu mpya utakapotengenezwa.” Huu ulikuwa ni uamuzi uliochelewa. Hata hivyo, wakati naanza kushangilia hilo, nilijikuta nakutana na habari moja ambayo ilisema kuwa hiyo akaunti ilishasimamishwa. Lakini naomba maelezo toka serikalini.

Juni 29 mwaka jana, serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini ilimsafisha mama Ballali (Anna Muganda) kuhusu tuhuma dhidi yake. Sasa leo serikali inapomnyoshea kidole Ballali, bado inasimamia utetezi wake wa mwaka jana kuhusu mke wa Ballali au uchunguzi wa BoT umewafanya waondoe utetezi ule?

Ninakuomba pia utuulizie kwa Spika ambaye alidai kuwa nyaraka alizozileta Dk. Slaa kuhusu BoT zilikuwa za kughushi na akatishia kumshtaki. Kwanini hadi hivi sasa hajamshtaki? Je, kwa kuangalia hatua alizochukua rais dhidi ya mambo ya BoT inawezekana Spika wetu akakiri makosa na kumuomba radhi Dk. Slaa na kumshukuru kwa niaba ya Bunge lake tukufu huku akiwa ametinga joho lake lililoshonwa Ulaya?

Nina maswali mengine mengi, lakini nikiendelea kuuliza najikuta yanazaa maswali mengine. Kwa kumaliza naomba nitumie mfano wa kabumbu. Timu inapocheza mechi kinachotakiwa ni kuifunga ile timu nyingine. Hivyo, wachezaji wa timu moja wanajitahidi kupachika mabao kwenye lango la ile timu nyingine. Inapotokea kuwa inapopigwa kona kwenye goli lenu, basi wachezaji mnatakiwa kujitahidi kuondoa “hatari” hiyo langoni. Na kubutua mpira kwenda mbali na goli.

Sasa inapotokea pale Kapteni wenu anautuliza mpira ule wa kona gambani, halafu kwa mbwembwe akatishia kuondoa karibu na goli na akawa anaelekea kwenye goli la timu nyingine na nyinyi wachezaji na washangiliaji mkafurahia hatua hiyo, basi mnafanya hivyo kwa haki na kwa busara.

Inapotokea baada ya kufika katikati ya uwanja kapteni wenu akageuka na kuanza kurudi na mpira kwenye goli lake, mnaweza kufikiria anataka kutoa pasi kwa mmoja wa mabeki. Lakini anapoongeza mwendo kumuelekea golikipa wake na kumpiga chenge halafu kwa kisigino akauchomeka mpira kimiani basi hapo inakuwa kasheshe!

Sasa baada ya kapteni wenu kujifunga goli na nyinyi mashabiki mkasimama kushangilia goli mlilojifunga wenyewe basi kuna tatizo mahali. Ukweli ni kuwa goli lile litahesabiwa na mwamuzi. Hata hivyo, endapo kapteni yule akazinduka katika njozi hiyo na akatambua goli lake hili limewasawazishia wageni, basi ni jukumu lake kuongoza jitihada za kupata goli la ushindi.

Na inapotokea kuwa kapteni mwenyewe baada ya kujirudi akaenda kupachika magoli mawili ya ushindi na lile la bima, basi lile kosa la kujifunga linabakia kuwa ni historia na linasamehewa.

Naamini kuwa kwa hatua alizochukua Rais Kikwete, katufunga goli Watanzania, tena la kisigino. Cha kuumiza moyo ni kuwa sisi na akili zetu timamu tumesimama kushangalia goli la kujifunga. Zaidi ya yote hata marafiki zetu (mabalozi) nao wanashangilia sisi kujifunga goli hilo! Nilipoandika mojawapo ya makala za mwisho za mwaka 2007 nilisema mwaka huu mkitaka kutuzuga hakikisheni mnatuzuga tukazugika. Hili ndilo nililokuwa namaanisha.

Rais Kikwete ana jukumu la kuhakikisha anafunga magoli mengine ya ushindi ili tuweze kumsamehe kwa goli hili la kujifunga. Ni kweli kafunga goli na wenye kushangilia wanashangilia. Hata hivyo, sasa tunataka tuone akilifunga goli hilo kwa mafisadi! Tunataka tuone akikata mbuga na kuelekeza mashambulizi yake katika lango la wezi na wabadhirifu! Hapo na mimi nitanyanyuka na kuanza kucheza nikishangilia.

Maswali mengi hapa yametokana na mchango wa wanachama wa: http://www.jamboforums.com

Niandikie: mwanakijiji@jamboforums.com

No comments: