Friday, January 11, 2008


Heko Rais, sasa tunamtaka

Balali ajibu maswali

Maulid Ahmed
HabariLeo; Thursday,January 10, 2008 @21:01

NASHAWISHIKA kuamini kuwa juzi katika taarifa za habari za televisheni na redio, Watanzania wengi walitega masikio na macho yao kusikiliza uamuzi mzito wa Rais Jakaya Kikwete juu ya ripoti ya ubadhirifu uliofanyika huko Benki Kuu (BoT).

Kwa upande wa magazeti, nilishuhudia siku ya pili kila watu wakipitisha macho kwenye magazeti kupata habari hizo, wengine ikiwa ni kupata kiundani zaidi habari hiyo na wengine kwa mara ya kwanza. Ilimradi tangu juzi imekuwa gumzo mitaani juu ya uamuzi mzito ambao naamini mzuri aliowahi kuufanya Rais katika kipindi chake cha miaka miwili.

Rais Kikwete amethubutu kutopoteza muda na kuiweka hadharani ripoti hiyo ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo iligundua upotevu wa Sh bilioni 133 kutokana na ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young.

Upotevu wa fedha au wizi huo wa fedha zetu umefanyika kupitia katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA), hatujui sehemu nyingine katika benki hiyo. Kwa leo sitaki kuingia huko. Uamuzi wa Rais naamini umerudisha imani ya wananchi pamoja na upande wa vyama vya upinzani ambao walikuwa wa kwanza kuibua ubadhirifu huo.

Watu wamezoea kusikia ukaguzi na uchunguzi mbalimbali unaofanyika na ripoti zake kutotolewa hadharani tena kwa muda mfupi kama ilivyo hili, hali iliyofanya iaminike kuwa viongozi wanaficha ripoti mbalimbali kwenye makabati na hawafanyii kazi.

Si aghalabu pia kusikia kiongozi anayefanya ubadhirifu akafukuzwa kazi na wengine kuamriwa kuchunguzwa na kuwajibishwa kwa haraka kama ilivyotokea kwa ripoti hii ambayo hapo awali Dk. Wilbrod Slaa ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema alivyodai kuwa upotevu huo umewahusisha vigogo wengi kupitia kampuni hewa.

Kwa hali ya kawaida na imani za Watanzania wengi zilivyo baada ya kusikia tuhuma hizo, walikuja na suluhisho kuwa ripoti hiyo ingeishia makabatini na rais asingethubutu kuwaadabisha Gavana Mkuu, Dk. Daudi Balali na wengine. Ametudhihirishia amethubutu. Rais Kikwete ametuonyesha Watanzania kuwa yeye hana muhali na mtu na kweli kura za wananchi hazijapotea, anasimamia na kulinda mali za wananchi.

Binafsi naona huo uwe mfano wa kuigwa na watendaji wake, wakiwemo Mawaziri kwa kutumia madaraka waliyopewa kutoficha maovu hasa yenye maslahi kwa wananchi na kuweka hadharani ili wananchi waelewe kinachoendelea. Vilevile wawachukulie hatua wote wanaofanya ubadhirifu walio chini yao ili nchi hii iwe safi na imani za walio wengi zirejee juu ya serikali yao kwa kiwango kikubwa.

Ikiwa Rais Kikwete amethubutu kwenye hili kubwa basi bila shaka sasa tusubiri na ripoti nyingine kubwa za tuhuma mbalimbali zikiwekwa hadharani na yeye mwenyewe na wasaidizi wake kama ripoti ya Richmond ambayo Spika wa Bunge, Samuel Sitta ameshakabidhiwa na kamati aliyoiunda kufuatilia suala hilo.

Mbali na uamuzi mkubwa huu wa Rais, Watanzania sasa wanataka kuona Balali ambaye anaweza kujibu maswali mengi juu ya upotevu wa fedha hizo akirejeshwa nchini aje kujibu na arejeshe fedha za walipa kodi ambazo zililipwa kisanii kwa wachache.

No comments: