ILIKUWA imenyesha mvua siku walipomzika bibi yule wa miaka 54; bibi aliyependa amani na kupinga ugaidi. Picha yake ya mwisho mzuri kama malaika akiwapungia Wapakistani.
Wakamuua. Wamemzika leo. Sasa nimewasha gari. Gari haliwaki. Nikajiuliza hili gari lina mkosi gani, mbona lilikuwa sawa nilipokuja nalo hapa dukani kununua mkate? Kando yangu kila mtu yuko na yake.
Niko katikati ya Uzungu. Ndiyo mtasema hii kalamu inatoka Uzunguni, Ulaya, London. Ukweli uzunguni pakubwa, papana, parefu. Kuna sehemu ukiingia unahisi dunia nyingine. Hakuna mtu weusi. Kuna mitaa London imejazana ?wamatumbi? utadhani uko Soweto, Kiboriloni, Namanga, Kisarawe, Kakamega.
Sasa? Kila nikitazama wananipita Wayahudi wamevalia masuti yao meusi, madevu marefu, kofia nyeusi, hawana la kusema nami; akina mama wao wamevalia magauni ya karne tatu zilizopita wamebeba watoto wawili, watatu; wanazaa kweli watu hawa. Katika kabila la Kizungu ambalo bado linazatiti jadi zake za kale, hawa Wayahudi wasioitambua Krismasi, wasiomtambua Yesu Kristo, wanamchukia vile alivyowasuta kuwa walimuua.
Hawawapendi Waislamu kwa kuwahusisha na ugaidi, wakimwona mtu kapita na kanzu, hijab, baibui au barghashia wanatahadhari mithili ya inzi aliyeona utando wa buibui.
Ilikuwa siku ile walipomzika Benazir Bhutto, ndiyo. Magaidi wakasingizia eti alikwepa risasi akajigonga mwenyewe kichwa. Wewe.
Huna dogo? Kila Mpakistani alikuwa akilia. Waliocheka magaidi na wanajeshi wasiopenda demokrasia. Siku chache baadaye, mwanae dume mwenye miaka 19 akatangaza ataingia katika siasa agombanie ujumbe aliouliwa mamake mpenzi, kama babu yake, Zulfikar Bhutto, aliyenyongwa na wanajeshi mwaka 1979. Sasa siku hiyo gari langu limezimika ghafla katikati ya barabara. Ulaya hakuna msalie mtume.
Iko gari nyuma yangu inanipigia tarumbeta; dereva kafura haoni, hasikii, hajali, hana simile; macho kayatoa ungedhani kapikichwa pilipili. Nikatoka nikamwonyesha kidole gumba kilichoelekezwa chini, nikiimanisha mashine imekufa; ishara nilizozoea za kimataifa. Madereva duniani wanatambua alama za vidole. Alivyokuwa punguani akajifanya hasikii, kaendelea kunipigia honi. Mwekunduuuu.
Gari limekufa, nikasema kwa nguvu tena Kiswahili.
Waaaaaaaaaaaat?
MY CAR IS DEAD.
Ala. Akashika kichwa. Kikono kimeacha kupiga honi, anatafuta sigara, akawaisha.
Nikaanza na mimi kazi ya kusukuma gari niliondoe nje ya barabara.
Ananitazama huku akipiga simu ya mkononi, akiweweseka kwa ghadhabu na matusi. Nahisi alikuwa na misheni sasa dili imefariki kama Benazir Bhutto (alivyotutoka na Pajero lake lililopigwa bomu la Al Kaida) kama hili gari lililogeuka punda aliyekataa kunywa maji. Maana wanasema huwezi kumlazimisha mnyama kula. Kule nyuma madereva wengine wameanza kulundikana, wanatandika honi. Miye kijasho kinanitoka, nishazoea maisha ya ughaibuni, ya kila mtu na lwake.
Natweta. Mara gari likawa nje ya lami, sasa magari yanayokwenda kasi yakiendeshwa na kisirani cha miji mikubwa: mshike mshike, yakanipita, nyuso za London zilizofura, taswira zisizo za subira wala upole. Bongo baada ya miaka michache itageuka hii jehanam ya Ulaya, ya nchi zilizoendelea, nchi tajiri, ya miji mikubwa yenye madereva wasio na utulivu. Subira na utulivu ni suala la shamba, la mikoani, vijijini; subira iliuawa na ubepari. Wee wacha tu.
Basi, gari limekufa. Nikapiga simu kampuni ya usaidizi wa magari. Kununua gari Ulaya si tatizo hata kidogo. Unaweza kufanya kazi wiki moja ukanunua gari. Ndiyo maana somo, ni hili. Kwao wazungu kuwa na gari si hoja kama sisi. Sisi gari ni kitu cha kujivunia maana usafiri wa shida, kuwa na gari ufalme. Utambaji. Faraguzi. Mikogo. Ulaya kuwa na gari si lolote maana magari bei rahisi.
Tatizo li katika sheria. Ukishanunua hilo gari la shilingi laki moja, lazima ulikatie kodi ya barabara (shilingi laki nne kwa mwaka, kama lako gari dogo, kadri linavyozidi ukubwa ndivyo kadri mfuko utakavyotoboka); ulipeleke mahali likapimwe kama kweli linafaa barabarani. Inaitwa MOT. Wanacheki kila kitu: je, taa zote zinawaka; je, mikanda ya usalama inafanya kazi, magurudumu yanakwenda sawa, usukani hautetereki; je, honi ziko poa: mambo chungu nzima. Mengi ni kwa usalama wako dereva na abiria.
Kila mwaka lazima ulipime na kuandikiwa cheti maalum hicho cha MOT. Gharama yake? Kupima ni shilingi elfu themanini hadi laki moja kuendelea. Ukitakiwa ununue kitu (kama gari bovu) basi zitakutoka zaidi. Halafu kuna bima. Hiyo bima ni Al Muhim, walllahi. Ukigonga au ukigongwa lazima uwe na bima.
Ukikamatwa na polisi kama huna bima unapelekwa mahakamani. Sasa ndani ya bima ndipo penye ahueni. Ukiharibikiwa gari unawapigia simu wanakuja kukutengenezea, kama mimi sasa. Kampuni ziko nyingi. Nikapiga simu.
Namba ya gari ?Sauti nyororo ya msichana aliyechangamka.'
Nikampa sista, chiriku aliyentuliza jasho, namba.
Namba ya kila gari nchi hii iko katika tarakilishi (kompyuta ya taifa), wana anuani ya unapoishi, nyumba, mtaa, tarehe ya kuzaliwa, vyote.
Jina lako fulani?
Ndiyo.
Hebu sema tena jina lako zima.
Gari lako rangi fulani, aina fulani?
Ndiyo.
Nini tatizo?
Haliwaki.
Haliwaki kwa vipi.
Limezimika katikati ya barabara halikuwaka tena.
Uko wapi?
Nkaeleza vizuri nilipo : jina la barabara...
Okei. Subiri fundi atakuja si chini ya saa nzima.
Na kweli; baada ya nusu saa kabasi rangi hudhurungi na vimulimuli vikali, rangi chungwa hako kakatamba mbele yangu, kakasimamishwa kando yangu. Upo hapo?
Moja ya sababu kuu madereva nchi zilizoendelea hawasaidiani ni hiyo. Miaka ya kwanza nilipofika Majuu ilinishangaza, utamwona mtu kaharibikiwa gari, hakuna anayesimama kumuuliza vipi shida? Nilishangazwa sana. Sababu ni hiyo.
Huduma zinazotolewa na bima unayolipia wastani wa shilingi milioni moja kwa mwaka (nazungumzia magari madogo ya kawaida, kadri gari linavyokuwa kubwa, kama haya mapajero tuliyonayo Bongo kufuatana na barabara zetu za mashimo, ndivyo bima inavyokuwa aghali), husaidia huduma hiyo. Pia hapa kuna kitu, ubinafsi. Tabia na taswira ya jamii za kibepari ndiyo hiyo. Kila mtu na lwake; shetani anamtafuna aliyeachwa nyuma.
Sasa namsalimia fundi aliyefika na magwanda na madita. Salama ya London, ya kuguna tu. Kuna kamvua karasha rasha , baridi inakita utadhani kiama. Unyama unyama.
Fundi kakunja madita, mdomo umefutuliwa, hajibu salamu yangu.
Nini tatizo?
Uso umemfura, kapiga nane, hataki masihara. Nahisi kichefu chefu.
Namweleza tatizo.
Gari limekatika hivi hivi tu?
Nasema lilikuwa linakwenda kama kawaida, nikapaki kidogo kununua mkate pale juu, kuwasha likawaka likaenda kidogo, likazimika; halikuwaka tena.
Hasemi zaidi. Huyooo anakwenda katika kabasi, anarudi na kadude kakuwashia betri. Nishafungua boneti. Anabandika kale kadude na viwaya waya juu ya betri, kufanya testi.
Namwambia gari ilifanyiwa huduma ya seviss wiki tatu zilizopita, (sidhani ni betri lakini simwambii asije akasema najifanya mjuaji).
Hebu washa.
Nawasha.
Haliwaki wala haliguni; kama yeye, fundi.
Anakwenda tena basini. Anarudi na vijidude chungu nzima katika kakasha.
Namweleza kuna waya hapa chini umelegea, nilikuwa nimeugandisha kwa gundi ya plastiki, nahisi ndilo tatizo. Ananitazama weee. Namfafanulia kuwa nahisi kila nikiwasha moto hauendi katika injini. Ananitazama kama niliyesema jambo la kwanza la maana toka aje. Mafundi wanapenda wakikuona dereva unaelewa kidogo siri ya tatizo lako. Usipojua be wala te, wanakushiti.
Anachokonoa tena, ananiambia niwashe gari. Gari bado inasonya, kimya kama usiku. Huyooo anakwenda zake anarudi na vikorokocho chungu nzima. Anainama na kuanza kazi. Huku kando wapambe wanapita, kila mtu na lwake. Ni saa kumi mchana, lakini kagiza kanaanza kuingia. Majira ya Uzunguni haya. Wakati wa kipupwe usiku huingia mapema.
Nilete tochi? Namuuliza, maana ninayo katika gari.
Haguni wala hasemi kitu.
Ninahisi leo nimekutana na jiwe.
Baada ya dakika kumi, kiza kweli kinaanza kukolea ingawa mawingu yangali meupe; kando watu wanapita pita. Jamaa yangu sasa anakwenda basini anarudi na kibonge cha tochi na makorokocho mengine. Anainamia gari akichokonoa, akikarabati, hana habari na mimi.
Hebu washa gari.
Nawasha.
Bado gari kama yeye halitaki pelete pelete.
Anakwenda tena katika kabasi kake anarudi na kichuma na kachuma na vichuma na vyuma. Sasa anainamia pale akivichoma vile vyuma. Anaviunguza na kuunganisha zile nyaya zilizoachana. Anadondosha umaji maji ule wa rangi ya majivu na dhahabu na kuunganisha ukiwa bado mnyevunyevu. Kila kitu anafanya mwenyewe.
Taa anashika mwenyewe. Kuchoma, anachoma mwenyewe. Kila nikionyesha dalili ya kutaka kumsaidia kwa kumshikia kitu ananipa mgongo. Hautaki msaada wangu. Na mimi kuona vile nakaa pembeni nikiitazama mikono yake ikiwa kazini, kainama, fundi wa barabarani. Pembeni sasa zimeanza sakamoto za London.
Kuna bwana mdogo mmoja. Siku hizi za Krismasi watoto huharibiwa kwa zawadi. Kijana nafikiri ana miaka 15 analo kigari cha mashine kinachotumia betri. Yuko na dada yake wanaendesha kile kigari, kinapiga kelele, kinapukutisha moshi, kinafoka. Kila mtu anayepita kakunja uso lakini hakuna anayesema kitu. Humgusi mtoto wa mtu nchi hii.
Fundi wangu, wala hana habari; yuko kazini. Keshachomea vile viwaya, sasa anamalizia kuunganisha gundi na kuziweka sawa nyaya.
Saa nzima karibu imepita mekanika yuko shughulini, anaoka, anamalizia malizia.
Hebu washa.
Nawasha gari. VRUUUUUUUM.
Duu umetengeneza, nabatasamu. Nayeye kwa mara ya kwanza anatabasamu.
Je, kuna haja ya kubadili hizi nyaya?
Ah, hakuna haja, nishazichomea uzuri.
Zima gari.
Nazima.
Anazifunga nyaya pamoja, anapangusa uchafu wa vyuma vilivyoyeyuka, anaondoa kila kitu, anarudisha katika kabasi kake ambacho bado kanawasha vimuli muli rangi ya chungwa na hudhurungi.
Washa tena.
Nawasha gari. Gari linakubali.
Anaanza kuondoka. Kiburi kile kile, ukimya ule ule.
Ahsante sana , namwambia, nikimpa noti ya paundi ishirini (kama shilingi elfu hamsini).
Anakataa pesa yangu.
Ukweli ni kazi yake na hulipwa mshahara kwa kazi hiyo. Lakini siku za nyuma nimegundua hawa watu hawapendi haya mambo ya kulipwa chai au kupewa ahsante ya vijipesa vya bakshishi. Na bakshishi niliyotaka kumpa wala si ndogo kusema kweli.
Kaonyesha hii hulka ya kizungu ya kuthamini kazi, ya kuja kufanya alilojia kulifanya. Bila kucheka, kutania, lele lele, kupoteza muda. Majuu hiyo.
Barua pepe: kitoto2004@yahoo.co.uk
Blogu: http://kitoto.wordpress.com/
Kutoka gazeti la Mwananchi la Jumapili, 06.01.2008
1 comment:
hii nimeipenda. wenzetu wanafanya kazi bwana acha waendelee tucwaonee wivu. ingekuwa bongo ungedodaje?
Post a Comment