
*Yadaiwa kukua katika nchi za Umoja wa Afrika
*Ipo mbioni kutumika kwenye nchi wanachama wa SADC
*Jumuiya ya Afrika yaazimia kuanzisha Kamisheni ya Kiswahili
VIONGOZI mbalimbali wa Kitaifa, akiwemo Rais wa Serikali ya awamu ya nne, Jakaya Kikwete wamekuwa mstari wa mbele katika jitihda za kuhakikisha kuwa Lugha ya Kiswahili inatumika na kuimarika katika nchi mbalimbali duniani, katika makala hii, Mwandishi wetu ECKLAND MWAFFISI, anaelezea jitihada zinazofanywa na Serikali ili kuweza kufikia malengo yanayokusudiwa.
TANZANIA ni miongoni mwa nchi mbalimbali duniani iliyojiwekea mikakati endelevu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali.
Utekelezwaji wa malengo yanayokusudiwa kwa vitendo kutokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na viongozi wa kitaifa ni hazina kubwa ya maendeleo kwa Taifa la Tanzania na wananchi wake.
Januari 4 mwaka huu, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, ilikutana na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ili kuwapa tathmini ya maendeleo ya utekelezwaji wa mikakati mbalimbali ya wizara hiyo kwa kipindi cha Januari 2006 mpaka Desemba 2007.
Wizara hiyo inakabiliwa na changamoto ya majukumu mbalimbali ya kitaifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanaimarisha na kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili.
Akitoa maelezo yanayohusiana na wizara yake, Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo Bw. Mohamed Seif Khatib, anasema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Serikali kupitia wizara yake imefanya juhudi kubwa za kuhakikisha kuwa matumizi ya lugha ya Kiswahili yanaingizwa katika medani ya kimataifa.
Anasema jitihada zilizokwishafanyika ni pamoja na zile zilizoiwezesha lugha ya Kiswahili kuendelea kutumika katika Umoja wa Afrika na hatimaye kuwa moja wapo ya lugha ya kazi.
Bw. Khatib anasema mchakato wa kuiwezesha lugha hiyo ili iweze kutumika katika shughuli rasmi za Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki unaendelea vizuri.
===========
"Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko katika hatua za mwisho za kufanikisha mchakato wa kuanzishwa kwa kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ambapo Makao Makuu ya Kamisheni hiyo yamependekezwa kuwa nchini Tanzania," anasema Khatib.
==============
Anasema Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), liliendesha kongamano la Kiswahili la Kimataifa la Idhaa ya Kiswahili Novemba mwaka jana, jijini Dar es Salaam na kuhudhuliwa na idhaa 27 kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Lengo la kongamano hilo ni kuimarisha ushirikiano utakaofanikisha kuikuza na kuieneza lugha sahihi, fasaha na sanifu ya Kiswahili katika nchi mbalimbali duniani kote hususan kwa asasi za utangazaji zinazotumia lugha ya Kiswahili ulimwenguni.
Bw. Khatib amefafanua kuwa BAKITA,inaendelea kuandika kitabu cha Kiswahili kwa wageni, hatua ya kwanza na kamusi ya diplomasia na uhusiano wa Kimataifa ili kuweza kurahisisha matumizi ya Kiswahili katika mikutano mbalimbali ya Kimataifa.
Anasema Idara ya Maendeleo ya Utamaduni hapa nchini, imeendelea kuimarisha matumizi fasaha na sanifu ya Kiswahili kwa kuendesha warsha, semina na makongamano mbalimbali kwa wadau wa Kiswahili.
Uimarishwaji huo ni pamoja na uendeshaji wa semina ya wahariri wa vyombo vya habari kuhusiana na matumizi ya sanifu na sahihi ya lugha ya Kiswahili iliyofanyika mkoani Morogoro, Agosti 2006 pamoja na uzinduzi wa mwaka wa Lugha za Kiafrika uliofanyika Desemba 28 mwaka 2006 jijini Dar es Salaam.
Pia idara hiyo ilifanya maadhimisho ya siku ya Kiswahili, yaliyofanyika Februari 2006, na kutoa tuzo mbalimbali kwa watu waliochangia maendeleo ya Kiswahili na kuendesha warsha ya mafunzo ya ukalimani na tafsiri iliyoendeshwa na BAKITA, ili kuboresha stadi na ujuzi wa wakalimani iliyofanyika Novemba 2006.
Bw. Khatib amefafanua kuwa majukumu ya wizara yake ni pamoja na kuandaa sera na sekta ya Habari, Utamaduni na Mchezo, kusimamia utekelezwaji wake na kuandaa mipango ya ukuzaji wa sekta hiyo.
Pia wizara hiyo inahusika kuhamasisha uanzishaji wa vyombo vya habari katika maeneo ambayo hayavutii sekta binafsi, kukuza na kuimarisha fani za sanaa, kuimarisha na kukuza lugha ya Kiswahili pamoja na kukuza na kuimarisha ushiriki wa wananchi katika fani mbalimbali hususan mazoezi, michezo na michezo ya jadi.
"Dira ya wizara yetu ni kuhakikisha kuwa tunakuwa na Taifa lenye raia wenye ufahamu, Taifa linalothamini utamaduni wake na Taifa lenye wananchi mahili na hodari katika michezo," anasema Bw. Khatib.
================
Anasema dhamira ya wizara hiyo ni kuwa na Taifa lenye idadi kubwa ya vyombo vya habari vinavyozingatia sheria, maadili ya taaluma na ya jamii pamoja na kushiriki kikamilifu katika juhudi za maendeleo ya nchi na kudumisha umoja na mshikamano wa Kitaifa.
===============
Bw. Khatib anasema pamoja na mambo mengine wizara yake imeona umuhimu wa kuipitia upya sera ya utamaduni ya mwaka 1997 na sheria zinazounda mabaraza ya Bodi ya Filamu.
Anasema mchakato wa kurekebisha Sheria namba nne ya mwaka 1976 ya Bodi ya Filamu na michezo ya jukwaani na udurusu wa Sheria za BAKITA ya mwaka 1967 na BASATA ya mwaka 1984, pamoja na upitiaji upya wa hati za kuanzisha mfumo wa Utamaduni 'Trust Deed' bado unaendelea ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameridhia kupitiwa upya kwa Sheria za BAKITA na BASATA.
Anasema utafiti mbalimbali umeendelea kufanyika ili kulinda na kuhifadhi maadili ya Utamaduni kwa kufanya utafiti katika mikoa ya Kigoma, Tabora na Shinyanga ili kupata dhamira ya busara inayohitajika katika utungaji wa sheria zinazotumika katika mwenendo wa maisha ya kila siku.
Utafiti huo pia umefanyika katika mikoa ya Mtwara, Rukwa na Ruvuma ili kubaini mila na desturi zinazochochea na kusaidia kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Pia utafiti wa mchango wa lugha za asili katika kukuza istilahi za Kiswahili, umefanyika katika mikoa ya Tanga, Dodoma na Morogoro Septemba na Oktoba mwaka jana.
Bw. Khatib anasema utafiti wa kubaini sanaa na kazi za mikono za asili katika sehemu mbalimbali nchini, umefanyika ambapo awamu ya kwanza ya utafiti huo ilifanyika katika Wilaya za Same, Mbulu na Kigoma Novemba mwaka jana.
Akizungumzia mafanikio ya ujenzi wa miundombinu ya Utamaduni Bw. Khatib anasema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu muhimu ya sekta ya utamaduni hususan ile ya sanaa ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezwaji wake.
Utekelezwaji huo ni pamoja na ujenzi wa ukumbi wa Wazi wa Maonesho unaojengwa katika ofisi za Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) pamoja na kuendelea kwa maandalizi ya ujenzi wa ofisi za Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), ambapo TBC imefanikisha utoaji wa kiwanja miongoni mwa viwanja vyake kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hiyo.
Mafanikio mengine ni kukamilika kwa ukarabati wa banda la BAKITA lililopo katika viwanja vya Sabasaba na maandalizi ya ujenzi wa Jumba la Utamaduni na Kijiji cha Utamaduni katika kijiji cha Kiromo, kilomita sita kutoka mjini Bagamoyo.
Hatua iliyofikiwa ni kupatikana kwa eneo la ekari zaidi ya 100 ambalo lipo katika hatua za mwisho kwa ajili ya kupimwa na kuthaminishwa ili wamiliki wake waweze kulipwa fidia na kisha eneo hilo kumilikishwa kwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo.
Bw. Khatib ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya habari, imewasilisha mapendekezo ya kutungwa kwa sheria mpya kufuatia upungufu wa sheria zilizopo zinazosimamia sekta ya habari na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa sheria hizo.
Anasema sheria hizo zitaondoa kasoro zilizojitokeza ili kuweza kukidhi haja ya wakati wa sasa wa utandawazi, demokrasia na utawala bora.
Mapendekezo hayo ni matokeo ya majadiliano ya muda mrefu, 'usiopungua miaka 10', kwa kuwakutanisha wadau wa sekta ya habari baina ya wenyewe kwa wenyewe na wadau wa Serikali ambapo mapendekezo hayo yamekwisha kuwasilishwa serikalini.
No comments:
Post a Comment