Wednesday, January 16, 2008

Kwa nini serikali imewapendelea mahujaji?

M. M. Mwanakijiji

SIDHANI kama upendelo wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwa mahujaji waliokwama wakati wa kujiandaa kwenda Hijja umetokana na udini.

Naamini kabisa kuwa kulikuwa na sababu nyingine iliyomfanya Rais Kikwete na watendaji wenzake kukosa usingizi na kuhakikisha kuwa mahujaji wetu wanawahi ibada ya Hijja na mambo yote ambayo yanatakiwa kufanywa wakati wa Hijja tukufu. Miongoni mwa sababu naweza kusema kwa uhakika kuwa haihusiani na dini ya Kikwete.

Ninaandika hili kwa sababu kulifumbia macho ni kuwapa kibali watawala wetu kuendelea kuwatendea Watanzania kwa ubaguzi na upendeleo usio na sababu yoyote ya msingi.

Nimefuatilia sakata hili tangu mwanzo na kwa karibu nimejaribu kuangalia mwitikio wa serikali. Jambo moja ambalo ni dhahiri ni kuwa serikali imewatendea mahujaji hawa kinyume kabisa na jinsi ambavyo wamekuwa wakiwatendea Watanzania wengine wanaojikuta katika adha ya kukwama kutokana na matatizo ya chombo cha usafiri.

Kama watu wanavyoweza kukumbuka, mahujaji zaidi ya 300 walitakiwa kuondoka nchini kuelekea Saudi Arabia mapema Disemba, ili kushiriki katika ibada hiyo wakiunganika na mamilioni ya Waislamu wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani. Hijja ni mojawapo ya Nguzo Tano za dini ya Kiislamu ambako muumini wa Kiislamu mwenye uwezo wa kwenda Hijja anatakiwa kufanya hivyo angalau mara moja katika maisha yake.

Hivyo utaona kuwa Waislamu wengi kati ya mambo mengi ya imani ambayo wanayafanya katika maisha yao, Hijja huwa kama kilele cha kutimiza yale yaliyoamriwa na Mwenyezi Mungu.

Nguzo nyingine Nne za Uislamu ni Shahda (kushuhudia kuwa Mungu ni mmoja na Muhammad ni Mtume wake), Sala, Zaka, na Saumu. Kwa Mwislamu yeyote kuishi na kutimiza nguzo hizo ni sehemu ya msingi wa imani yake. Kwenye suala la Zaka hata hivyo, Waislamu wa Tanzania wamekuwa wakienda Hijja kila mwaka wakipanga na kujipangia safari zao kama kawaida na wanarudi salama salimini.

Mwaka huu hata hivyo kuna uzembe mkubwa uliofanyika kati ya wale walioaminiwa kusimamia mipango ya safari hii na hasa vikundi vile ambavyo havikutaka kuingia katika mpango wa Bakwata na hivyo kujitafutia usafiri wao wenyewe. Hivyo tunapozungumzia mahujaji waliopendelewa tunawazungumzia wale ambao tu waliamua safari yao kufanywa na taasisi mbalimbali za kidini ambazo si Bakwata.

Taasisi hizo kwa sababu wanazozijua wao waliamua kutumia Shirika la Ndege la ATCL kwa ajili ya kuwasafirisha mahujaji wao. Shirika ambalo limetoka kwenye hali mbaya ya kiuchumi, lenye kidege kimoja, shirika ambalo halifanya shughuli ya kusafirisha mahujaji kwa miaka zaidi ya kumi sasa.

Kidokezo cha sababu hizo kipo kwenye majibu ya ATCL kwa Wizara ya Miundombinu kwenye barua yake ya Desemba 12, 2007. Katika majibu yao kampuni hiyo ya ndege ilieleza wazi kuwa tangu mwanzo haikuwa tayari kuhudumia mahujaji mwaka huu na ya kuwa hakukuwa na mkataba wowote kati yao na kampuni ya RAK Leasing katika kusarifisha mahujaji. Suala la ‘safeguard’ ya maslahi ya mahujaji halikuwapo.

Sababu pekee ni ushawishi wa Mwenyekiti wa Bodi, Mustapha Nyang'anyi, kwa ATCL ndiyo kampuni ikaingia mkenge wa kujaribu kusafirisha mahujaji bila ndege yoyote! Katika majibu hayo yao kwa Waziri wa Miundombinu, kulikuwa na barua iliyokuwa imeandaliwa kupelekwa kwa taasisi za Hijja, lakini barua hiyo ilizuiwa baada ya mwenyekiti huyo wa bodi kuingilia kati.

Majibu ya Bodi yanasema kuwa “Barua ya ATCL yenye Kumb. Na DZ/C.1/99 ya Julai 26, 2007 ilikuwa na lengo la kutoa taarifa hiyo lakini haikufikia walengwa kwa maagizo ya mwenyekiti wa bodi.”


Ni hadi pale mahujaji walipojikuta wamekwama pale Kipawa ndipo siri ikafichuka na ndipo jitihada za kweli za kutafuta utatuzi zilipotokea. Ndipo watu wakamuona Mama Salma Kikwete akienda airport ‘kuwapa moyo’ mahujaji, na baadaye viongozi wa kisiasa n.k wakajitokeza kujaribu kutatua tatizo hilo.

Matokeo yake ni serikali kuingilia kati kwa ahadi ya kuhakikisha mahujaji wanaondoka na ndipo kwa jitihada kubwa mkataba ukaingiwa wa kuwasafirisha mahujaji hao, mkataba ambao na wenyewe ulikuwa na mapungufu yake.

Serikali ikatoa na ahadi kuwa mahujaji watapewa “kifuta jasho” baada ya usumbufu mkubwa walioupata na Rais wakati anazungumza na waandishi wa habari akaahidi kabisa kuwa atahakikisha kuwa mahujaji hawapati matatizo yoyote wakati wa kurudi nyumbani.

Kwa jinsi serikali ilivyoingilia kati sakata hili la kukwama mahujaji na jinsi viongozi wakuu wa nchi hii walivyojishughulisha, bila ya shaka kuna maswali ambayo watu wanayo na mimi ni mmoja wao. Maswali ambayo yameulizwa pembeni lakini miye nayauliza hadharani. Kwa nini?

Ili kuelewa uzito wa maswali haya naomba niwakumbushe kisa kingine cha mapema mwaka jana ambacho leo hii kwa wengi kimeshasahauliwa na hakina maana yoyote. Kwa wengine kisa hiki imekuwa ni ‘mavi ya kale’ ambayo hayanuki. Lakini kwa sisi wengine ambao tunafuatilia utendaji kazi wa serikali, kitendo cha serikali kuingilia kati safari za mahujaji na kutumia fedha zake nyingi (wasizokuwa nazo) kuwasafirisha, kuwalisha na hatimaye kuwarudisha Tanzania. Labda niliweke hili katika mwanga wa kile kisa kingine cha Watanzania waliojikuta wamekwama mahali fulani.

Pale wanafunzi 29 wa Kitanzania walipojikuta wanakatishwa masomo yao na kwa mabavu serikali ikaamua kuwarudisha nyumbani huku ikidai “walienda kule kwa maamuzi yao, na serikali haikuhusika kuwapelekeka” na baadaye kutuma barua za mkataba wa mikopo ili warudi nyumbani, mkataba ambao una miezi sita ambapo vijana wale watadaiwa, na hivyo kukatishiwa masomo yao huku wakiwa hawana uhakika wa kuendelea na masomo nyumbani. Watanzania tulikubali maelezo hayo ya serikali na tukawapa kibali cha uonevu.

Wanafunzi wale wakaomba kila aina ya msaada kutoka kwa viongozi wao na kutoa ushahidi wote waliokuwa nao kuwa hawakwenda kwa kujitakia na ya kuwa walikuwa wamekubaliwa mikopo ya kwenda kusoma; hakuna aliyesikia hata kuamua kulizungumzia isipokuwa kutupiana mpira.

Si Kikwete aliyesema Msolla keshalizungumzia na si Msolla ambaye naye akasema Rais ameshalitolea maelezo. Si Lowassa kiongozi mahiri, shujaa, aliyetamba bungeni aliyejitokeza na kukutana na wazazi wa watoto hawa! Serikali ikanawa mikono kabisa na kwa kumtumia Gesimba akazungumza na kuwakana watoto hawa hadharani huku mapovu yanamtoka kwa jazba! Wananchi tukakubali.

Cha kushangaza ni jinsi gani tumeshindwa kuoanisha na kulinganisha mambo haya mawili na kuona upendeleo mkubwa wa serikali kwa mahujaji. Sakata la wanafunzi Ukraine lilikuwa na sababu kubwa zaidi ya kuingiliwa kati na serikali kuliko suala la mahujaji. Hebu tulinganishe matukio haya na kuona upendeleo mkubwa uliokuwa na chembe za kibaguzi wa serikali kwa mahujaji.

Serikali ilisema wanafunzi walienda kule “kibinafsi” na ya kuwa serikali haikuhusika hata kidogo na walijaribu kuwazuia wasiende lakini “hawakusikia”. Msingi mzima wa serikali kujitoa ni kuwa “haikuhusika” na suala la vijana hawa.

Hebu turudi kwenye mahujaji. Mahujaji walikuwa wanaenda Saudi Arabia kwa sababu binafsi au la? Jibu ni ndiyo. Walikuwa wanaenda kwa sababu binafsi. Ni nani aliwaandalia mipango ya safari ya kwenda huko kwa Hijja? Jibu ni taasisi mbalimbali zenye kujishughulisha na mambo hayo. Kimsingi mahujaji walikuwa wanaenda kwa sababu zao za kidini na serikali haikuhusika hata kidogo katika kutoa mwaliko, kupanga, na kuandaa safari zao!

Kwa upande wa wanafunzi kule Ukraine waliamini ahadi ya serikali kuwa watatumiwa fedha zao za masomo na hivyo watangulie fedha zikifuata. Wakatumia fedha zao kukata tiketi na kuondoka. Mahujaji wakapewa ahadi na mwenyekiti wa ATCL kuwa ndege itapatikana na kutokana na ahadi hiyo waliamini kuwa mambo yatakwenda yanavyopaswa. Wanafunzi 29 wakaenda Ukraine, mahujaji wakaenda airport. Wote wakasubiri ahadi zitimizwe.

Ahadi zikachelewa. Wanafunzi waliokuwa Ukraine wakaanza kuulizia fedha zao na ahadi yao. Wakajaribu kila njia kutaka serikali iwakumbuke na kuwatambua, matokeo yake Profesa Msolla akaongoza shambulio la ukanaji na kuwang'aka vijana hawa. Vijana wakaenda hadi Ubalozi wa Uingereza mjini Kiev na kwa wiki nzima wakapigwa na mvua na baridi. Serikali ya Rais Kikwete akawalia ngumu!

Mahujaji wakapiga kambi airport na wakajaribu kutafuta kila aina ya msaada ili waondoke. Msaada kwa vijana Ukraine wakanyimwa, mahujaji si tu walitembelewa na mke wa Rais bali msururu wa vigogo ukawatembelea na ahadi lukuki!

Matokeo yake, vijana Ukraine wakaambiwa na serikali yao kuwa wakitaka hata kurudi nyumbani lazima watie saini barua za kuomba mkopo wa nauli na fedha hiyo lazima irudishwe baada ya miezi sita. Vijana hawakuwa na ujanja isipokuwa kukatisha masomo, kusaini barua za ‘kujichinjia’ na hatimaye kurudishwa nyumbani bila ahadi ya kuendelea na masomo wala nini. Waliporudi nyumbani wachache walioweza kuendelea na masomo waliweza lakini wengine wakaachwa solemba na kuhangaika mitaani!

Mahujaji hata hivyo, wakapewa ahadi na Rais wa nchi, kuwa “watakwenda Hijja” na jitihada zote zitafanywa. Ikaundwa ‘taskforce’ ya kushughulikia hilo na hatimaye mahujaji si tu walisafirishwa bali pia kugharimiwa. Serikali ikawalipia tikezi bila kutaka mkopo na kumwaga mamilioni ya shilingi huko walikokwenda na kuwahudumia kwa kila namna.

Wenyewe (kama alivyosema Naibu Katibu Mkuu Omari Chambo) walikiita hicho ndicho “kifuta jasho”. Hata wakati wa kurudi, serikali si tu ilituma watu Saudi Arabia bali ilihakikisha hata matatizo ya ukosefu wa ‘slots’ au ndege usingezuia hivyo, wakashirikiana na serikali ya Saudia na hatimaye kuwarudisha mahujaji nyumbani. Rais Kikwete akatimiza ahadi yake kuwa mahujaji hawatapa matatizo yoyote yale wakati wa kurudi. Tukashukuru Mungu.

Hata hivyo katika mambo hayo mawili kuna kitu kimoja ni dhahiri. Serikali iliwabagua vijana wetu Ukraine na kuwapendelea mahujaji. Ni kwa nini basi? Kwanza jibu liko kwenye namba; vijana 29 si namba ya kumkosesha waziri mkuu au Rais usingizi ila mahujaji zaidi ya 300 kwa hakika waliwaumiza kichwa. Hivyo serikali haikutaka kusababisha manung'uniko makubwa kwenye jamii hii hasa ukizingatia familia zaidi ya mia tatu zilizokuwa na wasiwasi ukilinganisha na familia kama 30 tu. Hivyo serikali haikujali wanafunzi.

Pili ni suala la unyeti wa sakata lenyewe. Suala la mahujaji ni suala la imani wakati wanafunzi ni suala la elimu. Kwa wale waliopata nafasi ya kumsikiliza Sheikh Ponda Issa Ponda na baadhi ya viongozi wa dini walivyokuwa wanazungumza kuhusu “kufanya maandamano” serikali haikuwa tayari kukabili ghadhabu ya Waislamu hasa ukiwa na watu kama “mtafutwa” Ponda Issa Ponda.

Manung'uniko ya baadhi ya jumuiya za Waislamu yakaanza kuenea ambapo tetesi za “njama” zikaanza tena. Tayari kulikuwa na suala la Mahakama ya Kadhi na sasa sakata la Hijja kuibuka hakukuwa na mtu serikalini aliyetaka hilo litokee. La wanafunzi Ukraine halikuwasumbua sana kwani lilihusu “elimu tu” na siyo imani ya watu.

Jambo la tatu hata hivyo ni madai ya “undugunaizeshen” uliofanyika. Mitaani ikaanza kusikika kuwa kati ya watu waliokuwapo kwenye msafara wa hija ni baba mkwe wa Rais Kikwete pamoja na ndugu kadhaa wa viongozi wengine. Hadi hivi sasa serikali haikukana hilo na mimi ninaamini kwa ukimya wao wamelithibitisha.

Kama Rais Kikwete alitaka amani nyumbani hakuwa na ujanja isipokuwa kuingilia kati ama sivyo “kula hakuliki na kulala hakulaliki” pale Ikulu. Rais ilimbidi aingilie kati kumwepushia aibu na adha baba mkwe.

Kimsingi tulichoshuhudia ni kitendo cha ubaguzi wa wazi na upendeleo usio na sababu kwa mahujaji kuliko Watanzania wengine wanaopatwa matatizo wakati wa usafiri. Mbona wakati treni imekwama kutoka Kigoma kuja Dar kwa karibu wiki nzima hatukusikia waziri mkuu kenda kuwaangalia au mpango wa kifuta jasho au hata kununuliwa “kuku” wa Itigi na minofu ya Saranda? Ni lini sera ya “kifuta jasho” imeingizwa serikali wananchi wanapopata matatizo ya usafiri na kwanini ianzie kwa mahujaji? Je, kuanzia leo hii wananchi wanaotaka kusafiri na vyombo vya serikali na wakajikuta wanakwama kutokana na makosa ya vyombo hivyo watarajie kulipiwa hoteli, msosi, na kujikimu kwingine, kama sivyo kwa nini?

Kama serikali imeona kuwa ni lazima ijihusishe katika masuala ya namna hii na ya kuwa hata kama mtu akijipangia mambo yake ya binafsi ambayo yanahusisha kwa namna moja au nyingine “ahadi” ya serikali kuwa anastahili msaada basi serikali itangaze kuwasamehe mkopo wa tiketi vijana wetu waliorudi nyumbani toka Ukraine na kuwaomba radhi kwa kuwatelekeza, kuwasusa na kuwakatishia masomo yao kimabavu.

Fedha iliyotumika kuwagharimia mahujaji kwa karibu wiki tatu ingeweza kuwasomesha vijana wote 29 kwa karibu miaka yote iliyobakia! Kama serikali yetu inajali wananchi wake basi ikiri kutowatendea haki na ya kuwa hata wale ambao walikatishwa masomo na sasa wameshindwa kurudi shuleni basi wasamehewe na waahidiwe kuendelea na masomo mwaka huu bila kuumizwa na masharti mapya ya mikopo kama walivyofanyiwa sasa.

Vinginevyo, tulichoshuhudia kwenye sakata la wanafunzi Ukraine na mahujaji pale Kipawa ni matumizi mabaya ya madaraka na uonevu mkubwa kwa watu wasio na sauti. Sisi sote hatuwezi kuwa katika kundi moja na ndugu wa vigogo ili na sisi tupate neema!

Nisieleweke vibaya, tatizo langu si mahujaji kusaidiwa kwani mwenye njaa hana mwiko. Tatizo langu ni msingi wa kuamua kuwasaidia wao na kuwakatilia watu wengine kwenye matatizo kama hayo. Kwa nini serikali ilibagua hivyo? Kama nilivyosema hapo juu siamini msingi ni dini kwani katika kundi la wale wanafunzi asilimia kubwa walikuwa ni waislamu na si wote toka bara. Mmoja ni mtoto wa Shehe!

Serikali ya Rais Kikwete kwa kufanya kitendo hiki cha kibaguzi na upendeleo wa wazi imeonyesha udhaifu mkubwa wa kuongoza na matokeo yake ni kutengeneza kiwango kipya kabisa.

Kuanzia hivi sasa Watanzania wa madhehebu yoyote wakikwama Kipawa serikali lazima iingilie kati! Si kukwama Kipawa tu bali piwa wakikwama pale Relwe au kwenye vituo vingine vya kusafiria ambako chombo cha serikali kilitakiwa kuwasafirisha.

Si kuwasaidia usafiri tu, kuanzia sasa Watanzania wote wanayo haki ya kudai kulipiwa gharama ya chakula na malazi wanapokwamishwa na vyombo vya serikali! Vinginevyo, serikali itueleze kwanini mahujaji walipewa upendeleo?


Niandikie: mwanakijiji@klhnews.com

No comments: