Wednesday, January 02, 2008
Orodha ya wauza 'unga' kwa JK
Majani ya midaharati aina ya "coca" (Erythroxylum coca)
na Hellen Ngoromera (Tanzania Daima)
JESHI la Polisi limekamilisha kazi ya kuwachunguza watu kadhaa, wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Habari ambazo Tanzania Daima imezinasa kutoka ndani ya jeshi hilo, zinabainisha kuwa baada ya kukamilisha kazi hiyo, iliandaliwa orodha ya watu zaidi ya 100, ambao ushahidi unaonyesha kuwa wanajihusisha na biashara hiyo.
Na sasa orodha hiyo, inayohusisha watu 34 walioonekana kuwa ni 'vigogo', imeshakabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Miezi miwili iliyopita, katika mkutano wao na waandishi wa habari ulioitishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema, na kuwashirikisha watendaji wake, jeshi hilo lilisema lina orodha ya watu 225 wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa hizo kwa nchi nzima.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Naibu Kamishna wa Polisi (ACP), Peter Kivuyo, alilihakikishia gazeti hili kuwa ni kweli orodha hiyo imeshakabidhiwa kwa rais.
Alisema kuwa katika orodha hiyo, yapo majina 34 ya vigogo, ambao ushahidi umewafanya polisi waamini kuwa wanajihusisha na biashara hiyo haramu.
Kwa mujibu wa Kamishna Kivuyo, taarifa na orodha ya watu hao iliwasilishwa Ikulu Novemba 30 mwaka jana, na kuwa idadi ya majina ya watu waliotajwa kufanya biashara hiyo imeongezeka.
"Tumeshaiwasilisha taarifa hiyo kwa Rais Kikwete tangu Novemba 30 mwaka huu, idadi ya watu waliotajwa kujihusisha na dawa za kulevya imeongezeka, vigogo waliotajwa kwa nchi nzima ni 34," alisema Kivuyo ambaye anashughulika na vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Miezi ya hivi karibuni Kivuyo alikaririwa akisema kuwa jeshi hilo lilikuwa limepokea orodha ya watu 225 kutoka maeneo mbalimbali nchini, wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Alisema 78 kati yao wakiwa ni wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, haijafahamika iwapo orodha hiyo inahusisha majina ambayo awali Rais Kikwete alisema ameikabidhi kwa jeshi hilo ili ifanyiwe uchunguzi kabla ya kupata taarifa zitakazowezesha kuchukuliwa kwa hatua.
Mara kadhaa, Rais Kikwete amewahi kunukuliwa kuwa amekuwa akipokea taarifaa mbalimbali kuhusiana na wahalifu na wala rushwa na yeye amekuwa akizifikisha kwa taasisi zinazohusika kama vile Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru).
Mapema mwezi Aprili mwaka jana, Kivuyo alionyesha mbele ya waandishi wa habari kitabu kilichoelezwa kuwa na orodha ya watu wanaotuhumiwa kuhusiana na biashara hiyo na kusema kuwa majina hayo yalikuwa yakichunguzwa.
Pamoja na mambo mengine, Kivuyo alisema kuwa kitabu hicho kilikuwa na orodha ya majina pamoja na taarifa ya kila mtuhumiwa kuonyesha anahusikaje na biashara hiyo.
"Hiki kitabu kina kila kitu… ni sula tu la muda, lakini ukweli ni kwamba wahusika wote wapo humu na hata mali wanazomiliki. Pia tunaendelea na zoezi la kuwapata wengine," alikaririwa Kivuyo akisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment